MADIRISHA ya usajili hutumiwa na klabu za soka kwa namna mbalimbali. Zipo ambazo athari zake huwa chanya au hasi na si rahisi kuonekana.
Pia madirisha hayo hutumiwa na klabu kadhaa kufanya usajili lakini hutokea mashabiki wa klabu husika na wadau wa soka kwa jumla wasielewe walichukua wachezaji fulani. Hii ni kwa sababu zipo klabu ambazo mbali na kusajili wachezaji kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao, husajili tu ili kufanya biashara.
Hivyo husajili wachezaji chipukizi sana na kuwatoa mikopo kwa klabu nyingine ndogo ili wakomae huko kabla ya kuja ama kuwachukua baadaye au kuwauza kwa klabu walimo au nyingine.
Klabu kama Chelsea wamejirundikia wachezaji sampuli hiyo wanaofikia 40 wakati Manchester City wanao 28 na wamewatoa kwa mikopo maeneo mbalimbali. Sasa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) halifurahii hali hii, hivyo limeamua kuja na kanuni mpya.
Fifa watazuia klabu kama Chelsea kujirundikia wachezaji wengi chipukizi wenye vipaji vya soka kwa mtindo wanaofanya sasa. Kuweka sawa kanuni za usajili umekuwa mpango wa muda mrefu wa Rais wa Fifa, Gianni Infantino haoni kwa nini klabu zijirundikie wachezaji hivyo.
Mpango wa Fifa ni klabu isiwe na wachezaji zaidi ya sita walio nje kwa mkopo, lakini ili hayo yapite, lazima ligi za nchi mbalimbali, klabu na wawakilishi wa wachezaji washirikishwe kwenye majadiliano na kutoa uamuzi kwa njia ya wengi wape. Chelsea msimu huu tu wanao wachezaji 40 huko nje, wakijaribu kutengeneza fedha kutokana na vipaji hivyo. Hata hivyo, Chelsea wanabisha kupeleka wachezaji nje ili kutengeneza fedha, badala yake wanadai ni kuwapa wachezaji hao wadogo muda wa kucheza na kuendelea kisoka.
Kamati ya wadau wa soka wa Fifa inasema hicho wanachofanya klabu kama Chelsea ni ukoloni wa kibiashara na unatakiwa kukomeshwa na kanuni hizo mpya zitakazoweka ukomo wa juu. Inatarajiwa kanuni hizo mpya zitawekwa mezani baadaye mwezi huu.
Mpango huo ukipita itakuwa na maana Chelsea watafungua ‘gulio’ kubwa la kuuza wachezaji wake. Itabidi Kocha Maurizio Sarri na benchi lake la ufundi wakae chini na kuchagua kina nani wabakishwe halafu wapange bei ya hao wengine.
Wapo hata mashabiki wa Chelsea wasiowajua wachezaji wao sampuli hii walio kwenye klabu nyingine wakiwa ama wamecheza mechi chache kabisa na Chelsea au hawajacheza kabisa. Watatakiwa kuuza wachezaji zaidi ya 30 katika muda mfupi ili kutii kanuni hizo mpya. Wachezaji wa Chelsea walio nje kwa mkopo na klabu waliko katika mabano ni makipa Nathan Baxter (Yeovil Town), Eduardo (Vitesse Arnhem) na Bradley Collins (Burton Albion).
Mabeki ni Baba Rahman (Schalke), Jake Clarke-Salter (Vitesse Arnhem), Michael Hector (Sheffield Wed), Tomas Kalas (Bristol City), Todd Kane (Hull City) na Matt Miazga (Nantes). Wengine ni Kurt Zouma (Everton), Kenneth Omeruo (Leganes), Trevoh Chalobah (Ipswich), Dujon Sterling (Coventry), Reece James (Wigan Athletic), Jay DaSilva (Bristol City), Ola Aina (Torino), Fiyako Tomori (Derby), Fankaty Dabo (Sparta Rotterdam).
Viungo wa Chelsea waliotolewa kwa mkopo ni Lewis Baker (Leeds United), Victorien Angban (Metz), Kenedy (Newcastle), Nathan (Atletico Mineiro), Josimar Quintero (Lleida Esportiu), Danilo Pantic (Partizan Belgrade), Mario Pasalic (Atalanta) na Ruben Sammut (Falkirk).
Wengine ni Charlie Colkett (Shrewsbury Town), Jacob Maddox (Cheltenham), Kasey Palmer (Blackburn), Kyle Scott (Telstar), Mason Mount (Derby), Tiemoue Bakayoko (AC Milan), Charly Musonda (Vitesse Arnhem) na Kylian Hazard (Cercle Bruges).
Washambuliaji ni Joao Rodriguez (Tenerife), Michy Batshuayi (Valencia), Ike Ugbo (Scun thorpe), Izzy Brown (Leeds) na Tammy Abraham (Aston Villa).