HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa tamko zito la kutomtambua Rais Jakaya Kikwete, kwa madai kuwa ameingia madarakani kwa wizi wa kura (uchakachuaji).
Msimamo huo ulitangazwa jana mkoani hapa na viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, ambapo walisema utakuwa ni unafiki kumhalalisha kiongozi aliyeingia madarakani kwa uchakachuaji wa kura.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Slaa, ambaye alikuwa mgombea urais wa CHADEMA, alisema wakati wa utangazaji wa matokeo, CHADEMA waliiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwataka kusitisha zoezi hilo, kwa sababu lilikuwa na kasoro nyingi, ikiwamo ya wizi wa kura, lakini NEC haikuwasikiliza.
Alibainisha kuwa NEC ilifanya kazi kwa uzembe na usiri na ilishiriki kuiba kura zake na kubadilisha matokeo kwa lengo la kumsaidia mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kikwete kupata ushindi mwembamba wa asilimia 61.
Alisema wananchi wamekoseshwa fursa ya kuongozwa na kiongozi waliyemtaka, kwa sababu Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu haukuwa huru na wa haki, hivyo hawaoni sababu ya kumtambua kiongozi aliyetokana na matokeo ya uchakachuaji.
"Nawashukuru Watanzania kwa kunipa kura zile zilizotangazwa na NEC, lakini leo napenda kuutangazia umma kuwa simtambui Rais Jakaya Kikwete kwa sababu kura zilizompa ushindi zilipatikana kwa msaada wa wizi na si matakwa ya wananchi," alisema.
Dk. Slaa ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuzungumza na vyombo vya habari tangu kutangazwa kwa matokeo ya urais, alisema lengo la demokrasia ni kupatikana kwa kiongozi aliyetokana na matakwa ya wananchi, lakini NEC na vyombo vya usalama viliamua kumpendelea mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Alibainisha kuwa wamefikia hatua ya kutomtambua Rais Kikwete, kwa sababu utaratibu uliopo hivi sasa wa kisheria na kikatiba, hautoi nafasi kupinga matokeo ya uchaguzi katika mahakama au chombo kingine kinachoundwa kikatiba.
Alisema NEC inalindwa kisheria na hata kama inachakachua matokeo ya uchaguzi kwa makusudi kwa lengo la kumnufaisha Rais Kikwete na chama chake.
Alibainisha kuwa katika mazingira hayo ya kisheria na kikatiba, njia pekee waliyonayo kuonyesha kutoridhika na ukiukwaji wa makusudi wa nguzo kuu za uchaguzi huru na wa haki, ni kuheshimu dhamiri zao kwa kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa na NEC hivi karibuni.
Aidha, alisema Usalama wa Taifa ni mafisadi wa kutumia rasilimali za taifa kwa kusaidia wizi wa kura kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Alisema anao ushahidi wa kutosha kuwa Usalama wa Taifa walifanya kazi hiyo ili kumnufaisha mgombea wa CCM, Kikwete ambaye alitangazwa mshindi katika nafasi ya urais kwa kupata kura milioni tano.
Dk. Slaa alisema matokeo ya uchaguzi yalibadilishwa kwa lengo la kumbeba Kikwete na kuongeza kuwa ushahidi huo hawezi kuupeleka Usalama wa Taifa kama alivyotakiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jacky Zoka, bali ataupeleka mahakamani kama akifunguliwa kesi ya kuikashifu idara hiyo nyeti.
Alibainisha kuwa hawezi kuupeleka ushahidi huo kwa chombo hicho kwa sababu chenyewe ndicho kilichoshiriki kufifisha demokrasia kwa kuchakachua matokeo ya urais, ili Kikwete aibuke na ushindi dhidi ya yeye (Slaa).
"Wanataka niwapelekee ushahidi, nifanye hivyo kwa nini wakati wao ndio ninao watuhumu? Wasijidanganye kuwa nitafanya wanachokitaka, kama wanaona wao si mafisadi, wakanishitaki mahakamani, huko ndiko nitawaonyesha," alisema.
Alibainisha kuwa kitendo cha Usalama wa Taifa kuwasambaza vijana wao mikoani kwa lengo la kuisaidia CCM na mgombea wake ni kosa la jinai, kwa sababu wao wamepewa jukumu la kuangalia usalama wa raia wote na wala si kutetea masilahi ya chama fulani.
Aliongeza kuwa CHADEMA haimuogopi yeyote, hivyo Usalama wa Taifa wasijidanganye kuwa wanao uwezo wa kuwatisha, ili wasiibue vitendo viovu vinavyofanywa na taasisi za umma kwa lengo la kulinda masilahi ya watu fulani.