Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Tawi la Olosiva, Kata ya Oloirien, Wilaya ya Arumeru Magharibi, kimetangaza rasmi kumvua uanachama ndugu Odero Charles Oderos kufuatia ukiukwaji wa katiba ya chama.
Kwa mujibu wa barua ya tarehe 23 Aprili 2026, uamuzi huo umefikiwa baada ya mhusika kushindwa kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili pamoja na kukataa kushiriki katika vikao vya chama licha ya kuitwa mara kadhaa.
CHADEMA imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia Katiba ya chama ya mwaka 2006, Toleo la 2019, hususan ibara ya 7.2.11(e) pamoja na ibara ya 5.4.3.
Aidha, kikao halali cha Tawi kilibaini kuwa mhusika alikiuka masharti ya chama na kwenda kinyume na maadili na miongozo iliyowekwa, jambo lililosababisha kuchukuliwa kwa hatua hiyo ya kinidhamu.
Pamoja na uamuzi huo, mhusika amepewa haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa taratibu za chama kama zilivyoainishwa katika katiba yake.
Hatua hii inaonesha msimamo wa chama katika kuhakikisha wanachama wake wanazingatia nidhamu, uwajibikaji na misingi ya chama hicho.