Mapema leo, uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ulikutana na ujumbe wa African Women Leaders Network uliokuwa ukiongozwa na aliyekuwa Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, akiwa ameambatana na aliyekuwa Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde.
Ziara ya ujumbe huo nchini Tanzania inalenga kukutana na makundi mbalimbali, ikiwemo vyama vya siasa na asasi za kiraia, kwa lengo la kukusanya na kufuatilia taarifa kuhusu matukio yaliyotokea kabla na baada ya tarehe 29 Oktoba 2025.
Kwa upande wa CHADEMA, ujumbe uliongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Mhe John Heche, akifuatana na Katibu Mkuu, Mhe John Mnyika; Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe Amani Golugwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Wakili Ali Ibrahimu; pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Mama Suzan Lyimo.
Katika kikao hicho, CHADEMA iliwasilisha msimamo wake rasmi kama ulivyoazimiwa na Kamati Kuu ya chama , na kueleza kwa kina matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kutokea kabla, wakati na baada ya tarehe 29 Oktoba 2025.
Chama kinasisitiza umuhimu wa uchunguzi huru na wa haki, uwajibikaji kwa wote waliohusika, pamoja na kulindwa kwa misingi ya demokrasia, haki na utawala wa sheria nchini.