CCM CHAMA CHANGU TUKUBALI MSIGWA AMETUPIGA 3–0!
📝 Naandika haya kama mwanachama mwaminifu wa Chama Cha Mapinduzi anayependa kuona chama chetu kinaendelea kushinda kwa hoja, sera na utekelezaji wake. Lengo langu si kukikosoa chama changu kwa kukidhoofisha, bali kukikosoa ili kijirekebishe.
🤔 Kwa mtazamo wangu, katika ziara hii tumepoteza mwelekeo wa kisiasa. Tumetumia nguvu nyingi kumjibu mtu mmoja badala ya kujibu hoja zinazowasilishwa kwa wananchi.
Chama changu kinashindwa kujibu hoja za Heche? 📢
👥 Kadri mikutano ya John Heche inavyoendelea, ndivyo anavyozidi kupata uungwaji mkono. Ukiwasikiliza wananchi na kuangalia namna wanavyopokea hoja zake, utaona wazi kuwa anazungumza mambo yanayowafanya wafikiri.
❓ Lakini sisi tunafanya nini?
📊 Badala ya kujibu hoja zake kwa sera, takwimu na mafanikio ya serikali yetu, tunaonekana kushambulia watu binafsi. Serikali yetu imefanya mambo mengi mazuri. Kwa nini tunashindwa kuyasema kwa nguvu na kwa lugha inayowafikia wananchi?
📌 Kwa mfano:
1️⃣ Kwanza, Heche anasema serikali ya CCM imeshindwa kutumia rasilimali za Taifa kuwakomboa Watanzania kiuchumi kwa zaidi ya miaka 60 ya Uhuru. Hata hoja hii hatuijibu kwa nguvu na takwimu.
2️⃣ Pili, anaendelea kudai kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haina uhalali wa kisiasa kwa sababu, kwa mtazamo wake, haikuchaguliwa moja kwa moja na wananchi. Badala ya kutoa majibu ya kikatiba na kisiasa, tunaonekana kukwepa hoja, jambo linalowafanya baadhi ya wananchi kuendelea kuamini simulizi hizo.
Halafu tunampa Msigwa umuhimu usiohitajika 🎯
🗣️ Wakati viongozi wangu wa Chama Cha Mapinduzi, wakiongozwa na Comrade Kihongosi pamoja na Comrade Ally Hapi, wakijitahidi kumshughulikia Peter Simon Msigwa kwa hoja kwamba ameondoka baada ya kukosa cheo, Msigwa mwenyewe anaendelea kusisitiza kuwa aliondoka CCM kutokana na matukio ya mauaji ya Oktoba 29.
💔 Anasema hawezi kuendelea kuishi akiwa sehemu ya dhambi ya damu za watu wasio na hatia.
❓ Swali langu ni moja tu:
⚖️ Ni kiongozi gani wa chama changu aliyesimama kujibu hoja hiyo moja kwa moja?
🥅 Chama changu tunapiga penalti nje ya goli. Teknolojia haidanganyi. Je, kweli tunaweza kutumia nguvu na rasilimali nyingi kiasi hiki kwa sababu ya mwanachama mmoja aliyeamua kuondoka? Hii inatuma ujumbe gani kwa wananchi?
📍 Mifano ipo wazi:
1️⃣ Tunatafuta na kukodisha screen kubwa ili wanachama watazame mkutano wa CHADEMA na kumsikiliza mwanachama aliyetuacha. Je, chama chetu hakina ajenda zake tena? Tunamsubiri Heche aseme ndipo tujibu?
2️⃣ Nilikuwepo kwenye maandalizi ya kuwapokea viongozi wetu hapa Iringa. Kulikuwa na uratibu wa bodaboda, mafuta na posho kwa vijana ili kupamba ujio wa viongozi. Je, nguvu zote zile zilikuwa kwa ajili ya kumjibu Msigwa pekee? Mbona utekelezaji wa Ilani ya CCM haukuwa ajenda kuu?
3️⃣ Tumetumia karibu robo tatu ya muda wa mikutano yetu kumzungumzia mtu aliyeamua kuondoka mwenyewe. Hivi leo kina David Silinde, Mwita Waitara, Dkt. Kitila Mkumbo, Patrobas Katambi, Pauline Gekul, Joshua Nassari, Peter Lijualikali, Dkt. Vincent Mashinji, Caristus Lazaro, Bananga na wengine wengi, kama wangeachwa walipokuwa, leo wangekuwa wanachama wa CCM?
🚶 Msigwa kuondoka ni haki yake ya kisiasa. Tulimpata mchezaji mzuri lakini hatukujua kumtumia ipasavyo. Sasa kwa nini gharama zote hizi?
📩 Nimekuwa nikipeleka maoni yangu ndani ya chama mara kwa mara, lakini mara nyingi hayasikilizwi. Leo nimeamua kuyaandika hapa kwenye kundi letu la WhatsApp ili tuyatafakari kwa pamoja.
🏛️ Chama kikubwa kama CCM hakipaswi kuonekana kinamfuata mtu mmoja. Kinapaswa kuongoza mjadala wa kitaifa kwa sera, hoja na mafanikio ya serikali yake.
📢 Tukubali ukweli. Katika mapambano ya hoja, hisia hazitoshi. Tunahitaji majibu ya kisera, takwimu, mawasiliano bora na uwezo wa kuwashawishi wananchi. Tukitumia muda mwingi kushambulia watu badala ya kujibu hoja zao, tunawapa nafasi ya kuonekana wanashinda mbele ya umma.
⚽ Kwa mtazamo wangu, katika awamu hii ya ziara tumepigwa 3–0. Lakini mechi bado haijaisha.
💡 Tujitathmini, turekebishe mkakati wetu, tutoke kwenye vikao vyetu tukiwa na hoja zenye nguvu, na tuwaeleze wananchi kwa ufasaha utekelezaji wa Ilani ya CCM na kazi zinazofanywa na serikali yetu.
🌿 Kidumu Chama Cha Mapinduzi. Kidumu chama tawala.
Comrade Ally Ismail Kombo