na Sitta Tuma na Janet Josiah, Bukoba
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kuitikisa nchi kwa maandamano na mikutano yake ya hadhara kuzidi kuungwa mkono na umati mkubwa wa watu katika kila mkoa kinakopita.
Baada ya kuiteka mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga, jana chama hicho kiliuteka kwa kishindo mji mzima wa Bukoba kwa mapokezi, maandamano na mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wingi wa watu ambao kwa mujibu wa wenyeji wa hapa, haujapata kutokea huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.Willbrod Slaa, akitoa tamko la msisitizo akisema moto wa maandamano ya kudai mabadiliko sasa hautakoma, utaendelea nchi nzima.
Dk. Slaa aliwataka wakazi wa mji huo kumbana waziri mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu kashfa mbalimbali za ufisadi na uzembe zinazoikabili serikali yake. Pinda anatarajiwa kuanza ziara yake mjini hapa leo.
Alisema CHADEMA itaendelea kufanya siasa kwa kuwafuata wananchi walipo na haitabakia kutegemea Bunge kama anavyotaka rais Kikwete wafanye kwani tayari chombo hicho cha wananchi kanuni zake zimechakachuliwa ili kudhibiti wabunge wa chama hicho.
Awali maelfu kwa maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba walitanda na kufunga barabara na mitaa ya mji huo kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana walipoanza maandamano makubwa ya kuelekea viwanja vya mashujaa mjini hapa kulikofanyika mkutano mkubwa wa hadhara. Maandamano hayo yalifanyika katika staili ya makundi huku kila kundi likichomoza katika mitaa tofauti na lingine na kujaza watu katika uwanja huo.
Baadhi ya waandamanaji hao walionekana wakiwa na mabango mbalimbali yaliyosheheni ujumbe wa kuilaani na kuipinga vikali serikali ya rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati mji wa Bukoba ukiwa ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa sana na janga la ugonjwa wa Ukimwi nchini, wananchi hao walionyeshwa kukerwa kwao na serikali ya CCM na katika moja ya mabango yao walisema hivi: Keri ya ukimwi kuliko CCM.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa, alipokewa kwa nyimbo zilizokuwa zikimtaja kuwa yeye ndiye rais halali wa nchi hii.
Rais, rais, rais, rais
., ulisikika umati wa watu ukiimba katika maandamano hayo.
Dk.Slaa aliingia kwa kishindo Bukoba baada ya kuachiwa huru na polisi mjini Kahama walikokuwa wanamshikilia akidaiwa kuwa alifanya mkutano bila kupata kibali wilayani Maswa.
Akizungumzia kukamatwa kwake katika mkutano huo wa hadhara jana, Dk. Slaa alisema walionikamata walitumwa wanikamate kwa sababu Kikwete ananiogopa, lakini sasa hawatuwezi, CHADEMA haikamatiki
Kabla ya tukio la kukamatwa kwa Dk Slaa juzi usiku askari polisi waliizingira hoteli ya Panich aliyokuwa amefikia kiongozi huyo.
Baada ya kufikishwa katika kituo cha polisi Mnadhimu huyo wa polisi alimhoji Dk Slaa: kwanini jana usiku ulikataa kuja polisi kama ulivyotakiwa? Dk Slaa alijibu Nilihofia usalama wangu kwa sababu watu waionifuata hotelini sikuwatambua kwa sababu walikuwa wamevaa nguo za kiraia.
Mnadhimu Kamugisha alimuuliza tena kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani kwamba kwanini juzi alifanya mkutano Imalampaka bila kibali cha polisi? Dk Slaa alijibu, nadhani mnafahamu kwamba chadema tunafanya maandamano na mikutano mikubwa ya hadhara na kila eneo tunalokwenda majimboni kuna ratiba, halafu ninyi mnauliza mambo kama haya hapa lakini juzi kiongozi wetu alipigwa jiwe na polisi hamjawakamata wahusika
Mbali na Dk Slaa kukamatwa na kuhojiwa na polisi wa wilaya hiyo ya Kahama kwa zaidi ya saa 1:30 wabunge wengine wawili wa CHADEMA, Chiku Abwao na Rachel Mashishanga pia walishikiliwa kwa mahojiano na jeshi hilo. Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Diwani Athumani (RPC) alipoulizwa sababu za jeshi lake kumkamata Dk Slaa wilayani Kahama badala ya kumkamatia wilayani Maswa alikofanyia mkutano huo, alisema waliogopa kumtia nguvuni wilayani Maswa kwa kuhofia uvunjifu wa amani.
Kafulila aifagilia CHADEMA
MBUNGE wa Kigoma Kusini David Kafulila (NCCR-Mageuzi) amemshangaa Rais Jakaya Kikwete kuogopa kazi nzuri inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kuzungumza na wananchi.
Licha ya kumshangaa rais Kikwete kwa hofu aliyonayo amekipongeza CHADEMA na kusema chama chake kinajipanga kwenda kwa wananchi kwa kuwa ni utekelezaji wa kazi za siasa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya NCCR-Mageuzi Dar es Salaam jana, Kafulila aliyewahi kuwa kada wa CHADEMA, alisema hofu ya kupinduliwa aliyonayo rais inatokana na watawala kushindwa kutimiza wajibu wao na kusababisha wananchi wengi kukata tamaa.
Mbunge huyo aliweka wazi msimamo wake kwamba licha ya kutofautiana kwenye baadhi ya mambo na chama alichokuwepo mwanzo alisema kazi nzuri inayofanywa na CHADEMA mikoani inastahili kuigwa na vyama vingine.
Alisema sababu ya kutoweka kwa hali ya amani nchini sio wanasiasa bali ni watawala kushindwa kutimiza wajibu wao hivyo ni rahisi kwa waliokata tamaa kufanya lolote watakaloona inafaa. Rais Kiwkete ni rais wetu namheshimu lakini katika hili natofautiana nae
CHADEMA wapo mikoani wanazungumza na wananchi, hiyo ni kazi ya chama chochote cha siasa binafsi nawapongeza, mimi na chama changu tunawaunga mkono. Wapo sahihi kabisa.
Hata sisi tutakwenda kwa wananchi tutafanya mikutano, unajua kuvunjika kwa amani ni matokeo ya watawala kushindwa kutimiza wajibu wao sasa wananchi wanakata tamaa wanaamua kufanya yao, alisema Kafulila.