Unayosema ni kweli, tangu tuweke mkataba wa Buzwagi na sasa wa Richmond, naona mashambulizi ndiyo yanakuwa makubwa zaidi. Hata hivyo hilo huja na territory. Tungekuwa hatuna maana kama tusingetarajia mawimbi ya mashambulizi yao.
Walianza na email ya "Dr. Slaa", na sasa wanashindwa hata kuficha kucha zao, kwani wamezitoa kuparua mtu yeyote ambaye kwao ni tatizo. Wanataka kumfanya Zitto awe hoja ya msiba wa Mbatia na hivyo kupoteza mwelekeo wa kujadili kiini cha matatizo ya ajali nchini mwetu. Hawataki kuona mapungufu ya serikali isipokuwa wanataka kulazimisha watu waone mafanikio yake.
JF itaendelea tena bigger and better.. wiki ijayo tutakuwa na mambo mazito ambayo Inshallah, siyo tu yataendelea kuliamsha taifa bali pia kulithubutisha Taifa zaidi na zaidi. Hapo ndipo tofauti ya kijiko na chapeo itakapoonekana.
Ndiposa, mstari wa maamuzi unazidi kuchorwa ardhini na ukuta wa tofauti za kifikra unazidi kupandishwa. Hatimaye kambi mbili zinazohitajika hapa JF zitakuwa dhahiri zaidi. Sasa wamefikia mahali pa kufuatialia nani "anampenda nani"! Hoja lazima zijibiwe kwa hoja, na hoja zenye nguvu lazima zishinde.
Tutaendelea pasipo hofu, husuda, woga, au kusita kwa namna yoyote kuonesha ni jinsi gani hoja zao ni dhaifu, kwani zinajengwa kwa msingi dhaifu. Kwa hili, kundi la tatu litaendelea kufuatilia na kuamua kutokana na hoja. Mapambano haya tuliyaingia kwa hiari, na hatutakoma, hatutarudi nyuma, hatutakatishwa tamaa na yeyote yule hata kama atajivika vazi la kondoo! Tumewapinga watawala wetu, tutawapinga na wapambe wao!!
Tutaendelea kuwakosoa na kukosoa sera zao potofu, na kukebehi mwelekeo wao wa kibabe! Hatutawaonea aibu, hatutawaficha, na wakati utakapofika (na hauko mbali) wale wote waliohusika na kulibaka taifa letu, na kuchota mali ya wana na mabinti zetu, huku wakiendelea kupepea vibendera vyao, wakizungukwa na wapiga saluti, huku wakiimbiwa nyimbo za pongezi na wakicheua mafuta ya mali za Watanzania, watasimama Mahakamani! Iwe katika mahakama ya sheria au mahakama ya watu, kwa hakika watajibu, iwe kwa hiari au kwa nguvu za sheria!!
Wale waliomua kuchagua upande wa watawala wetu na kuwatetea na kuwalinda, na kuwapaka rangi ili wapendeze, huku wakiwamwagia manukato na marashi wakati wamevunda na wao wanakaribishwa! Hatutalia mada zetu zikifutwa au kuhamishwa, hatutalalamika kwa kujaza posting zile zile watu wasipotujibu, na MoDs wakiamua kufanya lolote hatulia kama watoto waliodekezwa!
Tutaheshimu jambo forums, tutalinda kanuni ya msingi wake, na tutaitetea pasipo majigambo yoyote yale. JF itadumu, na hasa baada ya wimbi la pili la mapambano lijalo.
kwani unabii wa kuanguka kwa CCM utatimia, kwani uko mbioni, na unafanya hima kutimia!
M. M.