Hii habari ndivyo ilivyoripotiwa na Habari Leo:
Habari Leo
Kamati ya Wahadhiri wa dini ya Kiislamu nchini, wamekanusha habari iliyotangazwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, iliyodai kuwa kuna kikundi cha dini ya Kiislamu kinachotumika kuchafua jina la mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa nchini kwa kutumia nembo ya udini na ukabila.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Chifu Hussein Msopa, alizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, na kutoa tamko la kukitaka kituo hicho cha utangazaji kuiomba kamati hiyo radhi kwa kipindi kisichopungua siku saba kuanzia jana.
"Sisi tulikuwa kwenye mkutano wetu siku hiyo, hatukualika vyombo vya habari tulikuwa tukijadili masuala matatu; OIC, Kadhi na ukabila," alisema Msopa, na kuongeza kuwa katika ajenda hizo, walilazimika kuachana na ajenda mbili ambazo ni OIC na Kadhi kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete aliwasihi wananchi kuiachia serikali masuala hayo.
Alisema kitu cha kushangaza ni pale televisheni hiyo ilipofuatilia kwa siri mkutano huo bila kualikwa, na kurusha mjadala na mawazo ya baadhi ya wajumbe badala ya kusubiri nini kiliamriwa au baada ya kikao, kitu kilichowatia shaka juu ya usalama wao.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema taarifa hiyo ilipotosha umma na kuleta uzushi na uhasama baina ya Waislamu na Wakristo wanaoitakia mema dini hiyo, baada ya kueleza kuwa kikundi hicho kinachotumika kumchafua mfanyabiashara huyo, kinafadhiliwa na mtu aliyejulikana kwa jina moja la Manji.
"Tunatamka kwamba endapo ITV hawatatuomba radhi kwa siku hizo saba… tutahamasisha Waislamu na Wakristo nchi nzima kuacha kutazama taarifa yoyote ndani ya kituo hicho, pia kusitisha ushirikiano wowote wa kibiashara na Kampuni za IPP, na mwisho tutaomba dua na kulaani kituo hicho," alisema Msopa.
Alisema kamwe Waislamu hawataacha kujadili suala la ukabila ambalo linazidi kuota mabawa nchini siku hadi siku, na kufanya baadhi ya sekta na idara za serikali kuendeshwa kikabila na bila ufanisi, sababu zinazopelekea migomo, maandamano na hata uzalishaji na huduma mbovu.
Juhudi za kumtafuta msemaji wa ITV ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile, hazikuzaa matunda, baada ya Katibu Muhtasi wake, kueleza kuwa anahudhuria mkutano, na kwamba hatazungumza na mtu ye yote. Kwa mujibu wa maelezo ya Msopa, taarifa hiyo ilitangazwa na kituo hicho Novemba 3, mwaka huu na kurudiwa siku iliyofuata, pamoja na kuonyesha picha za wahadhiri hao wakihudhuria kikao hicho.
My Take:
Angalia kile wanachotishia kukifanya baada ya siku saba na kile ambacho nilikiripoti jana kuwa kilirekodiwa kabla ya kipindi hicho kurushwa (kwamba uamuzi wa kufanya kinachotishiwa kufanywa baada ya siku saba ulifanyika kabla ya habari hii kutoka hewani- inawezekana vipi?). Je siyo kwamba baada ya siku saba watakukwa wanatekeleza hiki:
a. Kuwaonesha waislamu kuwa Bw. Reginald Mengi na Freeman Mbowe ndio maadui wakubwa wa maslahi ya Waislamu nchini.
b. Kwamba Mengi na Mbowe wana mkakati wa kuhakikisha kiongozi anayekuja ni kutoka kabila la Wachagga. Katika hili la dhidi ya "Uchagga" wanamkakati walikuwa wana uhakika wa kutobughudhiwa na polisi kwenye mikutano ambayo waliipanga kuifanya hasa wakiamini kuwa IGP Said Mwema yuko upande wao. Hata hivyo mmoja wao aliapa kuwa aliwahi kuambiwa na Dr. Nchimbi kuwa Mwema ni Mchagga (sijui kwa upande wa mama) na hivyo wasitarajie sana.
c. Walioleta mpango huo wamemhusisha kiongozi wa juu serikalini kuwa ndiye aliyewatuma kutekeleza mpango huo hasa kuonesha kuwa vyombo vya IPP vinatumika kueneza Ukristu, kukandamiza Waislamu, na kuinua Wachagga. Hili litaelezwa ili Waislamu waanze kuvisusisa vyombo vya habari vya IPP.
d. Kuendelea kuwahusisha Mengi na Mbowe katika vifo vya Chacha Wangwe na Gavana Ballali.
Sasa baada ya siku saba mkisikia habari ni hii itakuwa ni kwa sababu ITV wamekataa kuomba radhi au kwa vile uamuzi huo tayari ulishachukuliwa? Kwanini wasitishie kwenda mahakamani kama wanavyofanya wengine?