Date::5/23/2009
Udhalilishaji huu Bongo Star Search haukubaliki
Fidelis Butahe
MWANZONI mwa mwaka huu niliandika makala kuhusiana na vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na majaji wa shindano la kutafuta vipaji vya uimbaji la Bongo Star Search (BSS) uliokuwa unaongonzwa na aliyekuwa mtangazaji wa kituo cha televisheni cha EATV, Salama Jabir.
Niliandika makala hayo kuwataka waandaaji wa shindano hilo ambao ni Kampuni ya Benchmark Production kuweka majaji ambao watakuwa msaada kwa vijana mbalimbali watakaojitokeza kuonyesha uwezo wao wa kuimba.
Msaada kwa maana kuu mbili ya kwanza ni kuwapa moyo washiriki ambao wataonekana kuwa na nia ya kuimba lakini hawana uwezo, pili kuwaonyesha njia nzuri za kufuata washiriki ambao wataonekana kuwa na vipaji. Na pia kuwapa moyo wale wote watakaojitokeza katika usahili.
Kipindi hicho kwa kuwa shindano hilo lilikuwa halijaanza niliwatolea mfano majaji wawili ambao walikuwepo katika shindano hilo mwaka jana ambao ni Salama Jabir na mtayarishaji wa muziki Master Jay.
Mfuatiliaji gani wa shindano la BSS asiyewakumbuka majaji hawa wawili jinsi walivyokuwa wakiwaumbua na kuwadhalilisha washiriki wa shindano hilo wa mwaka jana na mwaka juzi.
Nasema ni udhalilishaji kwa sababu washiriki walioonekana kutokuwa na uwezo mzuri wa kuimba walitukanwa live na majaji hawa bila kujali kuwa kipindi hicho kinarushwa hewani na mamilioni ya Watanzania wanakitizama.
Mshiriki mmoja wa mwaka jana ambaye alifanikiwa kuingia kumi bora alipandwa hasira na kuzungumza maneno machafu mara baada ya kuambiwa na Salama Jabir kuwa hana uwezo wa kuimba na alifika katika hatua hiyo kwa bahati za mwenyezi Mungu.
Mambo kama haya yameonekana mapema katika hatua za mwazo za usahili kujirudia, na hata kutaka kuleta mtafaruku kati ya Chief jaja Madam Rita na P Funk katika usahili wa Mwanza. Na sio Mwanza pekee bali katika mikoa mbalimbali ambayo wamesha zunguka kutafuta vipaji.
Majaji hao wamejisahau kuwa rais Jakaya Kikwete hivi sasa yupo katika mapambano ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anaishi katika maisha bora, hao vijana ambao wamejitokeza katika usahili ni dhahili wanakwenda kushindana ili waibuke washindi na kujinyakulia fedha na zawadi mbalimbali zitakazowasaidia katika maisha yao, wanapodhalilishwa namna hii na majaji hapo tunaijenga Tanzania tunaibomoa?
Sikushangaa juzi serikali ilipotoa tamko la kusikitishwa na kulaani vikali udhalilishwaji unaofanywa na majaji wa BSS kutokana na tabia yao ya kutumia lugha chafu isiyostahili kutumika mbele ya jamii iliyostaarabika.
Tamko hilo lilitolewa na Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Ghonche Materego alisema wao kama wasimamizi wakuu wa sanaa nchini wanalaani vikali vitendo vinavyofanywa na majaji wa BSS.
Alisistiza kuwa majaji hao ambao ni Rita Paulsen, Master Jay na P Funk wamekuwa wakivuka mipaka kwa kuwadhalilisha washiriki kitu ambacho ni kinyume na maudhui ya programu hiyo kwa mujibu wa maobi ya Benchmark Production.
Tangu kuanza kwa shindano hilo kumekuwa na malalamiko mengi yanayotolewa na washiriki wa shindano hilo pamoja na mashabiki na watizamaji wa BSS juu ya lugha zinazotolewa na majaji hao lakini kwa mwaka huu malalamiko haya yamezidi na kuvuka mipaka.
Master Jay na P Funk ni wafanyabisahara na wanamiliki studio za kurekodia muziki, siamini kama huko kwenye studio zao wanawadhalilisha wasanii kama wanavyofanya katika shindano hilo.
Kama ni njia ya kunogesha kipindi basi wahusika hawana budi kubadilisha njia hiyo, tunajua kuwa majaji hawa wanapata changamoto kubwa ya kukutana na vijana wengi kwa muda mfupi lakini hicho kisiwe kigezo cha kuwatukana na kuwatolea lugha chafu.
Materego alisema itakachokifanya BASATA ni kukutana na uongozi wa Benchmark Production kujadili suala hilo na kama wahusika wataendelea na unyanyasaji watasimamishwa na kufutiwa kabisa leseni ya programu hiyo.
Sasa hili ni suala jingine, itakuwa bora wafungiwe kama wakiendelea na udhalilishaji huu kwa sababu upo uwezekano wakaibuka washindi ambao watakuwa hawajali udhalilishwaji wanaofanyiwa na majaji hao kwa sababu wenye vipaji vya kuimba na kutunga wanaweza wakashindwa kuonyesha cheche zao na pengine kujiengua katika shindano kwa kuogopa kutukanwa na majaji hawa au kotojitokeza kabisa.
Mwaka juzi Jumanne Iddi ndio alikuwa mshiriki wa kwanza wa BSS kuibuka kidedea na kujizolea zawadi nyingi pamoja na kupata ofa ya kurekodi nyimbo katika studio ya Benchmark, washiriki wengine waliotinga katika hatua ya tatu bora ni Leah Muddy na Kala Jeremiah.
Mwaka jana mshiriki kutoka Bagamoyo, Misoji Nkwabi aliibuka mshindi huku nafasi ya pili ikinyakuliwa na mkali wa kubadilisha sauti na kupiga gitaa, Rogers Lucas huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na 'dogo' Aboubakar Mzuri ambaye hivi sasa anatamba na nyimbo ya Samahani.
Ni wazi kuwa washindi hawa walikumbwa na wakati mgumu sana mbele ya majaji hawa na inawezekana kulikuwa na washiriki wenye vipaji zaidi ya washindi hawa lakini kutokana na udhalilishaji wa majaji walishindwa kuonyesha cheche zao jukwaani.
Rais Kikwete aliahidi kutoa ajira milioni moja baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, BSS ilivyoanzishwa mwisho wa siku ni lazima mshindi apatikane, sasa kama ushindi wenyewe ndio huu wa kudhalilishwa sidhani kama kuna haja ya kuendelea kuwepo kwa majaji wa namna hii ndani ya BSS.
Mwisho
0754 597315
butahefidelis@yahoo.com