Battle: Dar es Salaam vs Nairobi

Battle: Dar es Salaam vs Nairobi

Sunset boulevard..... .
646cec6021a54ed55a8c871616b4621a.jpg
 
12

FEB 2018

NA MWANDISHI WETU

HABARI

Nipashe

Vifaranga toka Kenya kuteketezwa Namanga

MAMLAKA ya Mapato (TRA) imekamata na kutaifisha vifaranga vya kuku 5,000 vilivyokuwa vikiingizwa juzi nchini kupitia mpaka wa Kenya, katika mji wa Namanga mkoani Arusha na sasa vitateketezwa.



Vifaranga hivyo ni sehemu ya bidhaa mbalimbali zilizokamatwa na TRA zikiingizwa nchini kwa magendo, ikiwa ni pamoja na mayai kasha 416, tani moja ya sukari na chumvi, majani ya chai mifuko 18 na mirungi kilo 16.

Hii ni mara ya pili katika miezi minne kwa TRA kukamata vifaranga vya kuku mpakani hapo baada ya 6,400 vilivyoingizwa kutoka Kenya kupitia mpaka wa Namanga kuteketezwa kwa kuchomwa moto Oktoba, mwaka jana na mamlaka za wilayani Londigo.

Akizungumza baada ya kukamata bidhaa hizo, Meneja Msaidizi wa Forodha mkoani hapa, Edwin Iwato, alisema vifaranga hivyo ni mali ya Andrew Lymo.

"Tumewakamata wafanyabiashara watatu ambao ni Joseph Sekino akiwa amepakia tani moja ya sukari na chumvi na majani ya chai mifuko 18 kwenye gari T785 AWV, Innocent Minja akiwa na mayai kasha 416 na mirungi kilo 16 kwenye gari T 443 CQU na Andrew Lymo akiwa na vifaranga vya kuku 5,000 kwenye gari T441 DHW; wote wakitokea nchini Kenya kuja mkoani Arusha," alisema Iwato.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, alisema bidhaa zote haramu zilizokamatwa, ikiwamo vifaranga, zitateketezwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema zile zinazofaa kwa matumizi ya binadamu zitagawiwa kwa taasisi mbalimbali za Serikali zenye uhitaji kwa mujibu na taratibu zilizowekwa na TRA.

Uteketezaji wa vifaranga 6,400 kwa kuvichoma moto uliibua malalamiko kutoka kwa jamii na watetezi wa haki za wanyama Novemba, mwaka jana.

Zoezi hilo lililosimamiwa na maofisa kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na TRA, lilikuwa kwa mujibu wa sheria hata hivyo.

Ofisa Mtendaji kutoka Chama cha Kutetea Wanyama (ASPA), Livingstone Masija, alilaani utaratibu uliotumika wa kuteketeza vifaranga hivyo kwa kuvichoma moto.

Alisema kitendo hicho ni cha kikatili na cha kinyama ambacho hakiwezi kuvumilika.

Lakini Ofisa Mkuu wa kituo cha wanyama cha kanda ya kaskazini, Dk. Nyasebwa Malangu, alitetea hatua iliyochukuliwa na TRA na TFDA akisema ilikuwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Aprili 11, mwaka jana serikali ililieleza Bunge mjini Dodoma, kuwa hakuna mwekezaji aliyeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai nchini kwa ajili ya biashara, na katika kusimamia hilo kuanzia mwaka 2013 vifaranga 73,000 vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria vimeteketezwa.

Kauli hiyo ilitolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kuzuia uingizaji wa mayai kutoka nje kutokana na mayai hayo kuharibu soko la ndani.

Alisema kuanzia mwaka 2006, serikali iliweka katazo la kuingiza kuku na mazao yake nchini, ili kudhibiti ugonjwa hatari wa mafua ya ndege.

Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2007 na 2010 zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji katika maeneo ya mpakani, bandari na viwanja vya ndege.

Uteketezaji wa vifaranga hivyo Oktoba pia ulikuwa mjadala mkali katika mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Facebook na Twitter.
 
Back
Top Bottom