Barua ya wazi kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi

KILIO KIKUU

New Member
Jun 3, 2023
1
0
MH. RAIS,
POLE KWA MAJUKUMU MAZITO UNAYOKABILIANA NAYO TANGU UTWISHWE JUKUMU HILI ZITO LA KUONGOZA VISIWA HIVI VYA ZANZIBAR pale wakazi wa visiwa vya Unguja na Pemba walipokuchagua kuwa kiongozi wa visiwa hivi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Hadi sasa sisi wakazi wa visiwa hivi tunaziona jitihada zako kuu na za dhati kuboresha maisha ya wakazi wa visiwa hivi.

Pamoja na nia yako njema ya kutatua kero na changamoto mbalimbali za wakazi wa wananchi, wapo viongozi mbalimbali wanaokwamisha jitihada zako kwa urasimu na maslahi binafsi na badala ya kukusaidia wewe kwa nafasi ulizowaamini na kuwateua kuzisimamia kutatua matatizo ya wananchi wao wanazitumia nafasi hizo kuzidisha maumivu kwa wananchi, mfano ni viongozi waandamizi wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa Zanibar[ ZANZIBAR SOCIAL SECURITY FUND (ZSSF)] ambao kwa barua hii tunawalalamikia kwako.

Tangu mwaka 2019 sisi wafanyakazi wa Kampuni ya ulinzi ya Group 4 Security Tanzania Ltd (G4S) ambao kwa nyakati tofauti tulihamishiwa hapa Zanzibar kuja kufanya kazi kutoka Tanzania Bara kabla ya Julai 2017 tukiwa tayari ni wanachama wa mifuko ya jamii bara, pesa zetu za michango yetu zilitumwa kwa mfuko wa ZSSF kimakosa. Fedha hizo ni kadri ya Tsh. 170000000/= zikiwa ni malimbikizo ya michango ya wanachama 39 ya miaka 3 ambapo wengine kati yetu walishaachishwa kazi na wanaendelea kuteseka kwa ukosefu wa ajira na maisha magumu huku pesa zao zikiwa zimeshikiliwa kimakosa na chombo cha serikali yao ambacho nia ya kuanzishwa kwake si kuibia wananchi bali kuwapa nafuu baada ya wao kustaafu ama kuugua au wanapofariki kuwasaidia wategemezi wao. Sisi kwa upande wetu binafsi si wanachama wa ZSSF bali ni wanachama wa NSSF na kwa sheria ya mifuko ya jamii hatupaswi kuwa wanachama wa mifuko zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja .

Michango hiyo ni ya tangu Julai 2017 hadi Julai 2019. Kampuni yetu imetuma wajumbe mbalimbali kwenda kuwaomba ZSSF kuzirejesha fedha hizo bali h wamekuwa wakitoa ahadi hewa tu za kutupa matumani hadi mwezi wa mwezi wa nne mwaka huu waliposema wazi kuwa kwa sasa hakuna ufumbuzi juu ya michango yetu hiyo. Swali ni je, kwa nini wameshindwa kuzirejesha fedha hizo ili hali wanavyo vielelezo wazi juu ya uanachama wetu kwa mfuko wa NSSF? Je, ikiwa fedha hizo si zao kwani sisi si wanachama wa ZSSF wao wanazifanyia nini? je, hawajiulizi kuhusu hatma ya sisi wafanyakazi na kesho yetu iwapo tutakosa kazi na kuhangaika wakati wao wanakaa na fedha zetu au kwa kuwa fedha hiyo haina mwenyewe waliamua kuzigawana na kuzitumia kinyume cha sheria hivyo wameamua kutumia mbinu hiyo kutufanya tukose haki yetu na jasho letu?

Kwa barua hii Mh. Rais H.A. Mwinyi tunaomba uingilie kati na kutuauni ili tuweze kuipata haki yetu tuliyonyang`anywa na mfuko wa hifadhi za jamii Zanzibar. Tumejitahidi kwa njia zote kupata haki yetu lakini tumekwama na sasa tegemeo letu ni wewe, tafadhali twaomba utufute machozi tuliyolia kwa kitambo kirefu sana.

Mwisho tunakuombea hekima, afya bora na maisha marefu upate kuyatekeleza yote uliyowaahidi wakazi wa visiwa hivi kupitia ilani ya CCM. Ikiwa utahitaji vielelezo tupo tayari kukupatia Mh. Rais ili kukupa wepesi wa kutatua kero yetu na wengi wetu tupo hotel ya Neptune Pwani Mchangani.

Tunatanguliza shukrani za dhati kwako.
 
Back
Top Bottom