Bandari inatosha kuendesha uchumi, tunahitaji maamuzi ya kimapinduzi tusirudie yale ya TICTS

Scol

New Member
Dec 6, 2022
2
2
TANZANIA imekuwa kiungo muhimu kwanchi zisizokuwa na bandari katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Bandari zake za Dar es Salaam, Tanga naMtwara zimekuwa lango muhimu la bidhaa na biashara kwa nchi za Zambia, Zimbabwe, DRC, Malawi, Burundi, Rwanda na hata Uganda.

Hivi Karibuni nikiwa Nchi za Falme za Kiarabu Dubai, ambapo nilipata bahati ya kutembelea Bandari tatu za Dubai, nilifanikiwa kushuhudia mazao ya kilimo na ufugaji kama matikiti maji, vitunguu, nyanya, mchicha, viazi na hata kondoo yakishushwa katika Bandari moja ya Dubai kutokea Somalia, hali hii ilinifanya niwakumbuke wakulima wenzangu hapa nchini.

Nikajiuliza maswali kadhaa kwamba mbona nasisi tunavyo vyote hivi? Kwani tunakwamba wapi? Kichwani mwangu najawa na mawazo mengi sana kuhusu Bandari zetu na hapa leo naomba uniruhusu niangazie eneo hili.

RIPOTI ya Kituo cha Utafiti cha Research on Poverty Alleviation (REPOA-2008), Inaeleza kuwa sekta ya uchukuzi Tanzania inaweza kuchangia sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania kuliko sekta yoyote endapo itawekezwa kikamilifu. Kwamba inaweza kuchangia kuliko sekta za Utalii, Madini naKilimo. Ni sekta yenye uwezo wa kuchangia Zaidi kuliko sekta yoyote nchini.

Bila shaka ukweli huu unatokana na sababu kubwa tatu; Kwanza ni hoja ya Benki ya dunia kwamba Tanzania ni lango la Afrika kutokana na nafasi yake kijiografia (One of Global Gate way). Pili ni kutokana na ukweli kwamba Zaidi ya asilimia 90 ya Biashara duniani zinafanyika kupitia Bahari( World Economic Forum Report 2018). Na tatu, asilimia 90 ya biashara nchini Tanzania inapita bandari ya Dar es Salaam( World Bank 2013). Ndio maana nitaanza kwa kujadili nafasi ya Bandari na nini kifanyike.

Matumizi ya akili ni uwezo wa kubadilisha maliasili kuwa mali. Kwamba faida yoyote tuliyopewa na Mungu kwa maana ya maliasili ,haiwezi kubadilisha maisha yetu bila kutumia akili kugeuza maliasili kuwa mali.

Pengine ndio sababu katika mataifa 13 makubwa zaidi kiuchumi duniani, asilimia 62 ya utajiri wao inatokana na ubora wa rasilimali watu(Human Capital) , asilimia 25 inatokana na ufanisi wa Taasisi na asilimia 5 tu inatokana na maliasili (Oxford Review , Vol 1 2014).

Huu ndio msingi wa hoja ya kwanini tunahitaji maamuzi ya kimapinduzi kubadilisha nafasi yetu kijiografia kuwa utajiri kwa Taifa letu. Kama Taifa tunastahili zaidi kutoka kwenye bandari kulinganisha na tunachopata sasa. Hivyo maamuzi makubwa kuwa na bandari kubwa kutosha nafasi yetu kijiografia pamoja na mapinduzi makubwa kufanya bandari yenye ufanisi sio uamuzi wa kuendelea kusubiri.

Kumekuwa na mikakati na hatua nyingi zimechukuliwa kuanzia awamu ya 3 mpaka 5 chini ya viongozi tofauti kufanikisha mapinduzi ya Bandari.
Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba bado kuna mengi ya kufanya na pengine kwa uzoefu wa awamu zilizopita, awamu ya 6 inasimama nafasi muhimu kufanikisha hili kwa ukubwawake.
Nasema bado kwasababu, wakati Tanzania ikiwa nchi ambayo inapakana na nchi nyingi zinazotegemea bandari ya Dar es salaam, Bado bandari yetu hii imendelea kuwa ndogo kwa mbali kulinganisha na washindani wetu kamaBandari ya Mombasa.

Takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kwamba wakati Bandari ya Mombasa ilipitisha mzigo wazaidi ya tani milioni 34, Bandari ya Dar es Salaam ilipitisha mzigo wa takribani tani milioni 17. Hii ni kusema kwamba bandari ya Mombasa isiyo kwenye nafasi nzuri kulinganisha na yetu inapitisha mzigo mkubwa zaidi yetu.

Katika taarifa yake Mkurugenzi wa Bandari, Bwana PLASDUCE MBOSSA, aliyoitoa kwa wahariri wa vyombo vya habari Mwezi Oktoba mwaka huu , 2022, alisema kuwa mamlaka ya Bandari inao mpango kabambe wa mwaka 2022-2045, kuhakikisha tunakuwa na bandari kubwa na bora zaidi katika ukanda huu. Kama nimemuelewa sawasawa, Mkurugenzi anaama kuwa mpango huo kabambe unazungumzia ukanda wa afrika kusini ya Jangwa la sahara ambapo bandari kubwa kuliko zote ni Durban iliyopo Afrika ya Kusini.

Naam, huu ni mpango mzuri ukitekelezwa. Nasema ukitekelezwa kwasababu hatujawahi kuwa masikini wa kupanga. Changamoto ya muda mrefu ipo kwenye kuamua na kutenda. Hasa katika mambo magumu kama haya ambayo kwa kiasi kikubwa yanatoa ushindani dhidi ya nchi zingine na hivyo ujasusi mwingi kuhusika kukabiliana hata kufikia maamuzi na kutenda. Kwenye ulimwengu wa kibiashara leo washindani duniani wanatumia njia nyingi zingine mpya na ambazo hazikuzoeleka wala sio zakawaida (unconventional ) kukabili washindani wao.

Nchi nyingi zenye nafasi ya bandari zinaendelea na mikakati ya kujizatiti zaidi. Mikakati hiyo nipamoja na namna ya kujijenga kiushindani ili kuvuta mzigo kutoka bandari washindani.

Moja ya ripoti ya uchambuzi kuhusu namna ya kuboresha bandari ya Durban afrika ya kusini kwa jina la Is Durban Port Expansion really necessary? Katika uchambuzi huo wa mwaka 2013, pamoja na mambo mengine, walichambua nafasi ya kila mshindani wa Durban mwaka 2013 na kukadiria nafasi yake miaka 20 ijayo. Yaani mwaka 2033.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, lengo la Bandari ya Durban nikufikia uwezo wa tani milioni 341 kutoka uwezo wa tani milioni 105 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 300, wakati bandari ya Dar es salaam ikikadiliwa kuongezeka kutoka uwezo wa tani takribani milioni 21 mpaka tani milioni 31.5 sawa na ongezeko la asilimia 50.

Mombasa ilikadiriwa kuongeza uwezo wake kutoka tani milioni 25.2 mpaka tani milioni 55.2, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200. Huku Bagamoyo ambayo mwaka 2013 walionesha uwezo wake ni sawa na hakuna (insignificant), ilikadiriwa kuwa mwaka 2033 itakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa tani milioni 52.5 au zaidi ya uwezo wa bandari ya Dar es Salaam. (Haya yalikuwa ni makadirio yao mwaka 2013 wakati mjadala wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ulikuwa umepamba moto)

Aidha ripoti hiyo ilionesha kuwa mbali ya bandari hizo, washindani wengine wa Durban na uwezo wao kufikia mwaka 2033 ni Beira Msumbiji ni tani milioni 15.7, Maputo (Msumbiji) milioni 10.5, PortLouis (Mauritius) tani milioni 35.5 na Walvis bay(Namibia) tani milioni 27.6. Haya ni makadirio ya kufikia mwaka 2033.

Naam, tunayo changamoto kuhakikisha nafasi yetu katika ushindani huu. Kwamba wakati sasa bandari ya Durban mwaka 2021 ikipitisha shehena ya tani zaidi ya milioni 79, naMombasa zaidi ya tani milioni 34, Tanzania bado ilibaki ikipitisha shehena ya tani milioni 17 tu.

Kama ambavyo Afrika ya kusini iliweza kukadiria miaka 20 kutoka mwaka 2013 kufikia 2033, ndivyo hivyo itahitajika kwetu kufanya intellijensia hiyo kukadiria bandari washindani wetu ndani ya mpango kabambe wa 2022 – 2045. Ili bandari ya Dar es salaam, leo ifikie uwezo wa Durban itahitaji kuongeza uwezo takribani mara 4.

Kama mwaka 2033, Durban inakadiriwa kuwa na uwezo wa zaidi ya tani milioni 341, huku Tanzania ( Bagamoyo na Dar) ikiwa na jumla ya 3.tani million 84, maana yake lazma kuongeza uwezo sasa kwa takribani mara 5 ya uwezo wetu ili kufikia miaka hiyo tuweze kufikia ndoto ya kuwa bandari kinara katika ukanda wa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Ukitazama kwa jicho la kawaida, kuifanya Tanzania kufikia ndoto hiyo kubwa ni wazo lisilowezekana. Ndio maana inahitaji mawazo yasiyo ya kawaida kufanikisha hilo kuanzia sasa. Leo bandari ya Dar es Salaam, imeondoka kwenye jinamizi la karibu miongo miwili ambalo lilikuwa moja ya visiki kwa ufanisi wa Bandari hiyo. Mkataba wa TICTS. Mkataba wa miaka 20 kuanzia mwaka 2002 chini ya awamu ya 3.

Kama nchi tumepoteza pakubwa kupitia mkataba huu. Nakumbuka mwaka 2013, katika ripoti yake Benki ya Dunia ya Opening the Gate: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania walifanya tafiti kuhusu ufanisi wa Bandari ya Dar ambapo pamoja na mambo mengine, ilibainika hasara kubwa ambazo ni matokeo ya kiufanisi katika usimamizi na uendeshaji. Ilibanika kuwa; Nchi jirani zinazotumia bandari hii zilikuwa zikipoteza zaidi ya dola million 830 ambayo sawa na Trillion 2 huku Tanzania yenyewe ikipoteza mapato ya zaidi ya dola bilioni 1.8 sawa na zaidi ya Trillion 4 kutokana na ufanisi duni.

Naam, tunahitaji kufanya mapinduzi ya bandari kwa faida ya Tanzania na nchi jirani. Nchi za Malawi, Zambia, DRC, Rwanda, Burundi ,Zambia na Uganda wote wanaweza kutumia bandari ya Dar es salaam kwa kiasi kikubwa zaidi ya sasa.

Baada ya Mkataba wa TICTS kumalizika ni fursa ya kuingia mkataba mkubwa kwa maslahi mapana ili kufanya upanuzi wa bandari sanjari na uendeshaji kuifanya ya ushindani katika ukanda huu. Yapo mengi ya kuzingatia kufikia Bandari ya ndoto yetu.

Inahitaji mtaji na teknolojia kubwa kufikia malengo makubwa. Ni ngumu kutekeleza kwakutumia kodi zetu. Ni ushauri kutekeleza miradi mikubwa kama hii kwa njia ya PPP ili kupunguza presha ya kutumia makusanyo ya serikali kwenye miradi mikubwa ambayomatokeo yake ni baada ya muda mrefu .

Huo ndo uzoefu wa nchi nyingi Duniani zilizofanya mapinduzi makubwa ya Bandari zao mfano Dubai, India, Singapore. Serikali inaweza kuingia makubaliano na nchi au Kampuni kubwa Duniani ambazo zimefanikiwa katika mapindizi ya Bandari.

Kwa kuhitimisha Makala yetu wiki hii, ni vyema tukajikumbusha kwamba tumebahatika kuwa na ukanda mrefu wa Bahari ya Hindi wa zaidi ya Kilomita elfu moja 340 ambao unatoa fursa ya kuwa na Bandari zaidi ya moja ambapo tunaweza kuendeleza Bandari ya Dar es salaam, Tukajenga Bandari kubwa Bagamoyo, Tanga na Mtwara.
Na kimsingi hivi ndivyo walivyofanya Dubai ambayo ina bandari 3 zilizo karibu - Jebel Ali, Mina Rashid na Al Hamriyah - chini ya DP World ambazo zote zinafanya kazi kwa kushirikiana. Bandari hizi zinasafirisha kontena si chini ya milioni 22 kwa mwaka.
 
Back
Top Bottom