Wadau, sio BAKWATA peke yao walioishtukia serikali.Hata viongozi wengine wa dini wameshtuka.
Pitieni iyo nakala chini. Muone watu walivyochoka kudanganywa.
Padri: Viongozi wa dini msinunuliwe na serikali
*Awataka kuwa mstali wa mbele kulikomboa taifa leo
*Aonya miaka mitano ijayo hali ya nchi itakuwa mbaya
Na Tumaini Makene
WAKATI viongozi wa dini wanakutana na serikali jijini Dar es Salaam jana na leo, padri mmoja wa Kanisa Katoliki ameibuka na kuwatakja viongozi wasikubali kununuliwa wala kurubuni badala yake waweke msimamo wa kuleta mabadiliko nchini.
Huku akihoji kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kutawala mpaka lini wakati maendeleo ya nchi yanazorota, Padri Baptiste Mapunda ambaye amekuwa mmoja wa watu walio mstari wa mbele katika kutoa maoni na kuchambua mwenendo wa utawala na watawala nchini, amesema kuwa wakati umefika wa kukiambia ukweli CCM kuwa kimeshindwa kuendesha nchi, kuwakemea mafisadi na kuwaletea maendeleo wananchi.
Padri Mapunda ambaye ni mmoja wa viongozi wa Kanisa Katoliki nchini ambao wamekuwa wakizungumzia hadharani masuala mbalimbali ndani ya nchi, amewaambia wananchi kuwa muda wa kutumia kura zao vyema kuleta mabadiliko umefika, huku akiwataka kuacha kuhongwa fulana, pilau, pombe, kofia na vitenge, akisema uongozi haununuliwi, bali hupewa mtu anayefaa.
Katika taarifa yake aliyoituma kwa Majira juzi, Padri Mapunda ambaye kwa sasa yuko nchini Kenya kwa Masomo ya Uandishi wa Habari, alisema kuwa kura ni silaha kubwa ambayo haipaswi kuchezewa inayoweza kuleta mapinduzi ya siasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Katika uchambuzi wake huo alioupatia kichwa cha habari kisemacho "Viongozi wa Dini msiweke Mkataba na CCM wala kuhongwa", Padri Mapunda alisisitiza kuwa viongozi wa dini zote nchini wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuliokoa taifa, kwani hali itazidi kuwa mbaya kama Watanzania wataendelea kuongozwa kwa mtindo uliopo sasa.
"Ninashangaa ujasiri wa CCM kuwaita viongozi wa madhehebu ya dini na kuwaandalia semina. Semina hii inatia shaka kwa muda kama huu. Kwanza lazima ijulikane miezi michache ya nyuma serikali ya CCM ilikuwa na 'madharau makubwa sana' kwa viongozi wa dini kufuatia matamshi na nyaraka mbalimbali walizotoa.
"Serikali imekuja kugundua kwamba viongozi wa dini wanashika watu wengi sana kuliko wanavyofanya wao katika majukwaa ya kisiasa. Dini ni suala nyeti sana katika jamii, kama mtu hajui basi ni kipofu," alisema Padri Mapunda huku akitoa mfano wa jinsi viongozi wa dini nchini Kenya wanavyotishia kukwamisha Rasimu ya Katiba mpya.
Pia alitoa mfano wa wa Uingereza ambako kilichokuwa chama tawala cha Labour kimeondolewa madarakani kwa kupigwa dafrao katika uchaguzi na kilichokuwa chama pinzani cha Conservative, huku akiwataka viongozi wa dini waache kukibeba CCM ili watu washuhudie kiyama chake na akahoji "CCM inataka itawale miaka 100?"
Aliwataka viongozi wa dini watumie nafasi yao kikamilifu na wala wasiwe sehemu ya kuendeleza ufisadi nchini. Akiongeza kuwa nchi inanuka kila aina ya ufisadi, akisema kuendelea kuiacha CCM itawale ni kufuru kwa Watanzania na kwa Mungu.
"Viongozi wa dini msikubali kuhongwa wala kuweka mikataba ya kurudi nyuma na kupoozwa. Mkumbuke kuwa miaka mingine mitano ijayo hali ya Tanzania itakuwa mbaya sana kama tutaendelea na serikali hii kwa mtindo huu uliopo sasa. Mimi yangu macho nataka kuona viongozi wa dini sasa waongoze mapambano ya kuleta mapinduzi katika nchi ya Tanzania.
"Nafasi ya viongozi wa dini popote pale inajulikana, msiwe sehemu ya kuendeleza Ufisadi nchini, bila viongozi wa dini nchi leo hii ingekuwa wapi? Mmeona Uingereza wamefanya demokrasia ya kweli, Labour wameng'olewa madarakani. Na CCM inataka itawale miaka mingapi 100? Huku ni kutafuta kufuru kwa Mungu na Watanzania kwa ujumla. Semina inayoendelea sasa hivi kati ya CCM na viongozi wa dini iwe ya kuiambia ukweli CCM kwamba sasa ikubali kwamba imeshindwa kuendesha nchi na kuwaletea maendeleo wananchi.
"Imeshindwa kabisa kuwakemea mafisadi. Kwangu, itakuwa ni aibu kubwa kama viongozi wa dini watakula njama na CCM ama kupoozwa makali yao, naamini mtasimama kidete katika uchaguzi ujao. Acheni kuibeba CCM halafu tuone kiama chake," alisema Padri Mapunda.
Aliwataka Watanzania kutumia haki ya kura zao kuleta mabadiliko nchini na kuachana na zawadi za kupita wanazohongwa wakati wa uchaguzi na viongozi wanaosaka madaraka, "Dawa ni moja tu, kama ukipewa rushwa ya kura, chukua, lakini kamwe usimpe kura maana amejidhihirisha kuwa HAFAI kabisa kuwa kiongozi, uongozi haununuliwi bali unapewa na watu wakiona unafaa."
Pia alizungumzia suala la viongozi wenye umri mkubwa kung'ang'ania madaraka akiwataka vijana kuacha kuwavusha wazee katika nafasi mbalimbali, kwani dunia ya leo inahitaji vijana katika uongozi.
"CCM lazima ishikishwe adabu, kwa mara zote karibu na uchaguzi inajaribu kunyenyekea sana kwa viongozi wa dini. Mimi nasema ni wakati wa kufanya unabii, nchi inazaidi kudidimia...Na kwa upande wa vijana, nawaasa acheni kuwavusha wazee katika nafasi mbalimbali. Pitisheni vijana wenzenu katika nafasi mbalimbali.
"Dunia ya leo inahitaji vijana Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon aliyenyakua madaraka ana miaka 43 tu, mpo hapo vijana? Sasa hawa wazee wengi nchini Tanzania kwa nini wanang'ang'ania madaraka? Kuna nini ndani ya uongozi?" alihoji Padri Mapunda.
Source:
http://www.majira.co.tz/index.php?o...ticle&id=171:padri-viongozi-wa-dini-msinunuli