na Mobini Sarya
NAIBU Waziri wa Miundombinu, Dk. Makongoro Mahanga, ametaka wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambao wanavujisha siri za shirika hilo kutafutwa na watakapobainika washughulikiwe mara moja.
Pamoja na kukiri kwamba taarifa hizo ni za kweli, aliwataka wafanyakazi hao kuacha tabia hiyo na kwamba wanapoona kuna tatizo, washirikiane na menejimenti ya ATCL, ili liweze kutafutiwa ufumbuzi.
"
Ni lazima tushirikiane na menejimenti, tuwabaini wale wachache wanaoendekeza majungu, ili tuwashughulikie. Hawawezi kuwa na malalamiko halafu wanayapeleka kwenye vyombo vya habari na kwenye mtandao, bila kufuata utaratibu," alisema Dk. Mahanga.
Naibu waziri huyo ametoa kauli hiyo siku moja baada ya wafanyakazi wa shirika hilo kumjia juu kupitia chama chao cha wafanyakazi, baada ya kutoa kauli bungeni wiki iliyopita akiwatuhumu kuwa wambea na wenye majungu.
Dk. Mahanga alikuwa akizungumza jana jijini Dar es Salaam, katika Uwanja wa Ndege wa zamani, baada ya kupokea ndege mpya aina ya Airbus A320 iliyokodiwa na ATCL.
Alisema kauli aliyoitoa bungeni ilikuwa inawalenga wafanyakazi wachache wanaotoa siri za kampuni hiyo nje.
Alisema wafanyakazi wengi wa ATCL ni wachapakazi na ndio wamefanikisha ujio wa ndege hiyo, lakini kuna wachache ambao kazi yao ni kutoa nje nyaraka za kampuni kuhusu mabaya yanayotendeka, ili yachapishwe kwenye vyombo vya habari.
"Sikueleweka vizuri nilipotoa kauli ile, lakini nilikuwa naamanisha zile taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari...ukiona nyaraka au taarifa zimechapwa kwenye mitandao ya habari utakuta ni kweli zipo ndani ya ATCL, ndiyo maana nasema kuwa wapo wafanyakazi wanaotoa siri nje," alisema Makongoro.
Hata hivyo, aliwapongeza wafanyakazi wa shirika hilo kwa kufanikiwa kuileta ndege hiyo iliyokodiwa kwa dola 37,000 za Marekani kwa mwezi kutoka Kampuni ya WALLIS Trade, kwa mkataba wa miaka sita.
Aidha, alisema huo ni mkakati wa serikali kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inakuwa na ndege nyingi za kujitegemea ambazo zitasaidia kupambana kibiashara kama yalivyo mashirika mengine ya kimataifa.
Hivi karibuni Dk. Mahanga alinukuliwa bungeni akisema kuwa wafanyakazi hao ni waongo, wambea na wanakuza majungu katika sehemu zao za kazi. Kutokana na kauli hiyo, wafanyakazi hao kupitia Chama chao cha wafanyakazi ‘COTWU', walipingna kauli hiyo.
Wafanyakazi hao walieleza kuwa kauli hiyo ya Mahanga imewasikitisha na kuwafadhaisha.
Awali, jana baada ya kuwasili ndege hiyo, Mkurugenzi wa shirika hilo, David Mattaka, alisema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba watu 150 ni kutekeleza maagizo waliyopewa na serikali ya kuhakikisha wanaimarisha mtandao wa ndani.
Alisema ndege hiyo ipo katika hali nzuri na itaanza safari zake kwenda Afrika Kusini na baadaye wataanza kuitumia kutoka Dar es Salaam hadi Dubai.
"Leo ni siku ya furaha, maana katika anga yetu ndege moja imeongezeka," alisema Mattaka na kuwaomba Watanzania wawe na utamaduni wa kusafiri kwa kutumia ndege za ATCL, ambazo kwa sasa zipo sita, tatu za kukodi na nyingine za kununua
http://www.freemedia.co.tz/daima/2008/5/2/habari2.php