BAADA ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kulaumiwa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza utaratibu wa zabuni ulioipa ushindi kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond Development LLC kuwa iliisafisha wakati imeonekana ina uozo, Mkurugenzi wake Mkuu Edward Hosea ameitetea taasisi hiyo na kuisafisha kuwa ilifanya kazi yake kwa mujibu wa sheria inayoiongoza taasisi hiyo.
Hosea alisema kazi ya taasisi hiyo ni kupambana na rushwa na si kupambana na mikataba mibovu kama ilivyoonekana kwenye ripoti hiyo kuwa kulikuwa na tatizo la mikataba mibovu.
Mkurugenzi huyo ambaye amekuwa kimya tangu kutolewa kwa ripoti hiyo wiki iliyopita, alisema kuwa taasisi yake inafanya kazi kwa kufuata sheria ya rushwa ya mwaka 1971.
Kuna watu wakubwa wenye madaraka, vitendea kazi, uwezo, wenye fedha na wenye magazeti wanayoyatumia kujifanya vipofu wa sheria kwa sababu wangeisoma sheria wasingenihusisha na suala la Richmond, alisema Hosea.
Mkurugenzi huyo ambaye alikuwa anahudhuria mkutano wa kawaida wa wakuu wa taasisi za kupambana na rushwa kwa Afrika Mashariki unaofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, alipoulizwa juu ya uvumi uliozagaa kuwa amejiuzulu alisema, ningejiuzulu nisingesimama hapa.
Mimi namuamini Rais, nikiwa kama mteule wa Rais nipo tayari kwa shughuli ya uamuzi wowote dhidi yangu ili sheria ichukue mkondo wake
la msingi the rule of law must be observed.
Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Mwenyekiti wake Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilisema kuwa Takukuru katika taarifa yake kwamba Taifa halikupata hasara kutokana na Richmond ililenga kuficha ukweli.
Hivyo iliishia kujikanganya kwa kukiri kuwapo kwa mapungufu lakini yasiyokuwa na athari. Taarifa hiyo imengoa hadhi na heshima ya chombo hiki muhimu cha kitaifa kurejesha heshima ya umma mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi hiyo yafanyike, alisema Mwakyembe katika ripoti yake.
Source: Habari Leo, Feb 16, 2008.