Afungwa miezi 6 kwa utapeli wa kutumia jina la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Bahati Malila kifungo cha miezi sita jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matano, yakiwamo kughushi cheti kilichoonyesha kuwa kimeletolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Pia Mahakama hiyo imemuachia huru mshtakiwa Godfey Mtonyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitishwa pasipo kuacha shaka kwamba alihusika katika mashtaka hayo.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Richard Kabate akitoa hukumu hiyo jana Novemba 30, 2023 amesema hakuna shaka nyaraka zilizoghushiwa zilikutwa na mshtakiwa Malila hivyo kwa mujibu wa sheria, kosa la kughushi adhabu yake ni miaka saba.

"Kuwasilisha nyaraka za uongo adhabu yake ni miaka saba na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ni miaka saba, ambapo katika mashtaka hayo mshtakiwa Mtonyo hajakutwa na hatia, Mahakama hii inamuachia huru," amesema Kabate.

Hata hivyo, kwa mshtakiwa Malila, amesema Mahakama hiyo inamtia hatiani kwa makosa matano na kila kosa anatakiwa kwenda jela miaka mitano.

Kabate amesema Mahakama hiyo inamuhukumu mshtakiwa Malila kwenda jela miezi sita kwa kuwa ameshakaa gerezani miaka minne kwa kuzingatia maombi aliyoyatoa ya kumpunguzia adhabu hiyo.

"Nimezingatia maombi yake ya kumpunguzia adhabu kwa kuwa amekaa gerezani miaka minne na ni mkosaji wa mara ya kwanza na anajutia makosa yake, hivyo atakwenda jela miezi sita," amesema.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo. Naye Mshtakiwa Malila, aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia ya watoto wawili na anajutia kosa lake hivyo anaomba huruma ya Mahakama.

Baada ya hoja hizo, Hakimu Kabate amesema anamuhukumu kwenda jela miezi sita, badala ya miaka mitano kwani mshitakiwa amekaa gerezani miaka minne, hivyo anampunguzia muda ambao amekaa Gerezani.

Kwa mujibu ya hati ya mashitaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 13, 2020 katika eneo la Msasani, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, ambapo washtakiwa hao wakiwa na nia ovu walighushi vyeti vitatu vya mchango wa utoaji wa msaada vyenye tarehe ya Januari 13, 2020 vikionyesha vimetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Katika mashtaka ya kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa inadaiwa kuwa Januari 14, 2020 washtakiwa wakiwa wanafahamu hilo ni kosa, waliwasilisha nyaraka za uongo kwa Biao Lin Tang ambazo ni vyeti vya utoaji wa msaada vyenye tarehe Januari 13, 2020 vikionyesha vimetolewa na Waziri Mkuu.

Pia, inadaiwa Januari 14, 2020 katika eneo la Msasani, Kinondoni mkoani Dar es Salaam kwa lengo ovu washtakiwa walijipatia dola za Marekani 10,000 sawa na Sh22,950,000 kutoka kwa Biao Lin Tang kwa kudai kuwa zinaenda kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom