ACT Wazalendo: Vitita vipya NHIF vinageuza huduma ya afya kuwa biashara, Serikali ifute vitita vipya

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
ACT Wazalendo tumeguswa na taharuki za wananchi kutokana na taarifa za utata juu ya upatikanaji wa huduma za afya kupitia Mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF). Wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2024 tulishuhudia mivutano mikali kati ya Serikali na watoa huduma za afya binafsi (Vituo binafsi).

Mvutano uliosababisha vituo hivyo kusitisha kupokea wagonjwa wanaotumia bima ya NHIF na kutangaza kuwaondoa waliokuwa wanaendelea na matibabu katika hospitali hizo. Wiki hii tumeona taarifa mitandaoni na baadae kuthibitishwa na NHIF wenyewe juu ya kuondolewa kwa dawa 178 na vifaa tiba 15 katika Kitita kipya cha NHIF.

ACT Wazalendo tunaamini kwamba kiini cha hatua zinazochukuliwa, taharuki na migogoro inayojitokeza kila uchao kuhusu mahitaji na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote ni kutokana na sera mbovu ya Serikali ya kutaka kukwepa wajibu wa kuhudumia wananchi na vilevile kutaka kulimbikiza faida kupitia afya za wananchi wake.

Kwahiyo, Bima ya afya imejengeka katika msingi mbovu wa kisera ambao unaruhusu kutoa huduma kulinga na uwezo wa wananchi badala ya mahitaji aliyonayo. Ndio maana mara kadhaa tumeona hatua za Serikali kudhibiti huduma zinazotolewa na BIMA kwa kuanzisha vifurushi (matabaka), kupandisha gharama, kuondosha baadhi ya huduma na kuzuia matumizi kwa baadhi ya hospitali.

ACT Wazalendo tunarejea wito wetu wa kuitaka Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya matibabu bure kupitia huduma ya bima ya afya kwa wote bila vifurushi au vitita kwa kuunganisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa kila mtanzania. Ili mwananchi anapochangia hifadhi ya jamii awe anapata huduma ya afya moja kwa moja. Watanzania waunganishwe na NSSF ili kupanua fao la matibabu kutoka idadi ya sasa ya asilimia moja.

Ndg. Shangwe Mika Ayo
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.
14 Machi 2024.
 
Back
Top Bottom