Mzee Mwanakijiji, hebu turudi nyuma...Flashback 1995, kuna mambo mawili yalitokea;
1. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustino Lyatonga Mrema, baada ya kugundua anayo nafasi finyu ya kuteuliwa kugombea Uraisi kupitia CCM, alihamia NCCR - Mageuzi. Mrema hakuwa ametoa mchango wowote katika harakati za mageuzi na badala yake ndiye kinara aliyeongoza majeshi ya Usalama kupinga mageuzi kwa njia ya virungu, mabomu ya machozi na risasi za moto. Wako waliopigwa na kuteswa, wako waliopata ulemavu wa kudumu, wapo waliopoteza kazi na kufungwa na familia zipo zilizosambaratishwa na kusahaulika. Mwaka 1995 ndio mwaka uadui kati ya vyombo vya usalama na raia ulipozaliwa na ni huyo huyo Mrema ambaye awali aliapa kwamba akihamia upinzani laana imkute. Wakati huo tuko wengi wetu tulipinga sana Mrema kukaribishwa NCCR - Mageuzi lakini hatukusikilizwa hadi wengine tukakata tamaa kabisa na kuachana na siasa.
2. Dr. Wilboard P. Slaa aliwekewa mizengwe baada ya kushinda katika kura ya maoni kwa asilimia kubwa tu akiwa CCM na hivyo kuamua kuhamia Chadema na huko akateuliwa kugombea Ubunge. Alishinda kura na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Karatu na akatokea kuwa moja katika wabunge machachari walioichachafya CCM hadi kujizolea sifa nje na ndani ya bunge. Baada ya muda aliweza kuaminiwa na kila mwanachadema na baadaye uteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Mzee Mwanakijiji, kwa bahati mbaya CCM ni zaidi ya chama cha siasa. CCM ni zao la chama dola na ilirithi kila kitu kilichomilikiwa na chama dola, chama kilichoshika madaraka na chama kilichokuwa na mamlaka ya mwisho katika maamuzi yaliyolihusu taifa hili. Serikali ilikuwa chini ya CCM, Bunge lilkuwa chini ya CCM, mahakama zilikuwa chini ya CCM na vyombo vyote vya dola vilikuwa chini ya CCM. Kuipinga CCM kulitafsiriwa kama uhaini na katiba ya nchi ilifanyiwa marekebisho kwa kuangalia na kutanguliza matakwa ya CCM. CCM ilitumia kila njia kuzuia upepo wa mageuzi na hata pale ilipoonekana wazi kwamba kwa mara ya kwanza wanajaribu kupambana na kile kinachowazidi uwezo, walihakikisha wanayapokea hayo mageuzi kwa maneno lakini si kwa moyo wala matendo.
Waliendelea kuhatamia kila kitu walichokimiliki kama vile vyama vya upinzani havikuwepo, waliendeleza mfumo ule ule kwa nguvu zile zile, wakijilinda kwa mbinu zile zile za wakati wa chama kimoja. Kusema kweli hadi leo hali hii haijabadilika; kinadharia tunavyo vyama vya upinzani lakini kimfumo tunacho chama kimoja, CCM. Mijadala ndani ya Bunge Maalum La Katiba mwanzoni mwa mwaka huu yalizidi kuthibitisha kwamba hatuna upinzani nchini, tunavyo tu vyama vinavyotambulika vitabuni kama vya siasa lakini mchango katika mustakabi wa taifa haupewi umuhimu wowote na CCM. Wakikataa kuunga mkono pendekezo lolote la serikali CCM haijali itaendelea na utekelezaji kama kawaida na wakileta za kuleta, vyombo vya dola vipo kuwadhibiti na kuwatia adabu, kama alivyosema Pinda, wamechoka kuwa wavumilivu hivyo hamna namna na dawa ni kupiga tu.
Mzee Mwanakijiji, CCM kama ilivyo, ni ndoto kuamini kwamba kuna siku itakubali kuachia madaraka kupitia sanduku la kura hata kama wananchi watakuwa wamewachoka. Hii ndiyo sababu wengine tunasema, adui wa nchi hii kwa sasa si Kikwete, si Nape, si Kinana, si Makonda, si Lowassa, si Pinda, hapana, adui wa nchi hii ni mfumo unaoiwezesha CCM kubaki madarakani hata kama haina tena sifa wala uwezo. Katika kipindi kifupi kilichopita serikali yetu imeimarisha sana vyombo vya Usalama, imeagiza mabomu ya machozi, maji ya kuwasha, silaha za moto na vitu kama hivyo. Ukitazama kwa undani, tahayari hizi zote ni katika mipango ya kwadhibiti wananchi na zimetokana na woga, woga wa CCM kuketishwa benchi, woga wa mafisadi kukosa pahala pa hifadhi, CCM na woga wa kuwajibishwa na wananchi kwa vitendo vyao.
Mzee Mwanakijiji, najua yote haya unayafahamu. Najua unajua tahadhari yote hii inatokana na nini. Mwaka 2010 kabla ya Uchaguzi alitokea mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jeneral Shimbo, akiwaonya wanachi kuwa tayari kuyapokea matokeo kama yatakavyotangazwa na Tume na kwamba atakayekaidi atashughulikiwa. Siku chache baadaye akatokea Mhariri Mkuu wa Magazeti ya serikali akiapa kwamba katu upinzani hauwezi kutwaa madaraka ya nchi hii. Haya yalikuwa ni matamshi ya hatari sana katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa hawa wachochezi. Badala yake tumeshuhudia wakiongezewa myadhifa ndani na nje ya nchi. Swali kubwa hapa ji je kama wananchi tunao uhuru gani wa kujichagulia nani atuongoze?
Mzee Mwanakijiji, CCM kama ilivyo imejizatiti kweli kweli kwa lolote lile kuhakikisha hakiyumbishwi na mtu, kikundi au chama, wako tayari kutumia kila mbinu, kila nyenzo na kila silaha kujilinda hata ikiwa ni pamoja na kuvunja katiba. Kwamba kuna medium, hata kama ni mtu, inaweza kusababibisha kwa namna fulani kulisambaratisha hili zimwi, mimi ni katika wale watakaoikaribisha hiyo medium. Zaidi ya hapo hakuna namna, labda kwa kuchukua silaha na kuingia msituni
kitu ambacho sikiafiki hata kidogo. CCM ikipasuka vipande vipande kama ninavyoomba mimi, siku hiyo hata mimi nitamwagika mtaani kushangilia, wewe je? Bila hivyo tuanze tu kunyoa tukjitayarisha kwa maumivu kama yale yale tulioaminishwa yangeisha mwaka 1985, 2000, 2005 na 2010.