666-NYAYO ZA KUZIMU--31-
"nitume mimi!"
mzee Rama alirudia kauli yake huku akimtamzama mzee Patili machoni,macho yao yaliyokua yanatazamana yalihakisi hali ya shari,tabasamu alilokua nalo mzee Rama halikua la wema,lilificha uadui mkubwa wa wivu ndani yake na pia malengo makubwa ya kimapinduzi.
Mzee Patili aliwageukia wanakijiji huku akiwa na sura ya kufikiri akasema...
"ameamua kujitolea,siwezi nikamzuia,maombi yetu yawe nae aweze fanikisha kile tulichodhamiria."
baada ya kusema hayo maneno aliingia ndani na kuchukua fimbo fulani akamkabidhi mzee Rama kwenye mkono wa kuume kisha akamshika bega na kumpa maelekezo madogo juu ya ile fimbo,jinsi gani atakavyoitumia kumlinda,pia akamtakia safari njema.Mzee
Rama baada ya hayo maelekezo alimuaga mkewe na wanae huku akiwahaidi ya kwamba atarudi,akamfuata kijana mmoja aitwae Sadiki ambae ndie wa kwanza kumrubuni juu ya mzee Patili kisha akamuambia waende pamoja,alikubali na safari ikaanza.
Mzee Rama aliamini ya kwamba ile ni moja ya fursa adimu aliyokua anaitafuta kwa muda mrefu,japokua ni ya hatari lakini hakujali hilo,aliweka maisha yake rehani,eidha afe au afanikiwe kumpindua mzee Patili.
Safari ilitawaliwa na ukimya wa hali ya juu kutokana na kila mmoja wao kutoruhusu mdomo wake ufunguke,mwanga mwanana wa mwezi uliokuwepo uliwafanya waone wakanyagapo hivyo kutokua na hitaji la koroboi,mioyo yao ilikua inasema na mungu wao lakini ilikua ni zaidi ya hivyo kwa mzee Rama aliekua anasema na akili yake hasa juu ya nini atakachofanya afanikishe lengo.
Huku safari ikiendelea wingu zito taratibu lilianza kufunika mwezi uliokua unatoa nuru,giza totoro likaanza kuingia na kuwapa wakati mgumu wakina mzee Rama kwa kutoona walipokua wanaelekea! Sadiki aliekua ameshikwa na uoga maradufu alivunja ukimya
"..sasa mzee tutaendaje na hili giza??...si bora turudi tu!"
mzee Rama alitulia kwa muda bila kujibu,kisha kwa sauti ya msisitizo akasema...
"hatuwezi kurudi hilo sahau kabisa,tumeamua kujitolea na hii ndio maana ya kujitolea,wingu lipitalo lisikufanye ukageuza wako moyo,baada ya muda hali itarudi mahali pake"
baada ya mzee Rama kutoa hilo jibu ukimya ukarudi tena,hakuna alieongea zaidi,miguu yao ilizidi kusogea mbele taratibu kwa kukisia njia huku wakiyatoa macho yao ili yapambane na hali ile ya kiza iliyotawala,bado sadiki alikua na kinyongo moyoni lakini lile jibu alilopewa lilimfunga mdomo wake,hakua na jinsi,ilimbidi afuate kile atakachoelekezwa na ilikua ni robo saa sasa tangu waanze safari,walishakiacha kijiji chao kwa umbali wa kutosha japokua umbali wa maana bado ulikua mbele yao,walipiga konde.
Wingu jeusi taratibu lilianza kuacha mwezi uchomoze hivyo kuruhusu mwanga urejee na kuamsha matumamini ya wakina mzee Rama,waliongeza kasi sasa baada ya uhakika wa njia huku bado vinywa vyao vikiwa vimefungwa na macho yakitizama wanapoelekea,ghafla walisikia sauti za watu tokea nyuma zikiwaita!!! Mioyo yao ililipuka kwa uoga puh!! Kusikia majina katika hali kama ile ni kitu kilichowashangaza mno!! Mzunguko wa damu ukaanza kwenda kama mbio za marathoni! Shingo zao zilizowageuza nyuma hazikuwashuhudisha chochote,hawakuona kitu ila walisikia sauti!!..Miili ilitetemeka!!
"kimbiaaa Sadiikii!!" kauli hiyo ya mzee Rama ilikua kama kipenga kilichoruhusu mbio zianze,kila mmoja alikimbia kadiri ya uwezo wake huku akitizamatizama nyuma kuangalia kama wanafuatwa,umri wa mzee Rama ulikua ni kikwazo kikubwa kwani ulimfanya asiweze kukimbia kwa kasi kama Sadiki aliekua mbele yake,kila alipojitahidi kuvuta makasia ya mbio alihisi miguu inauma japokua alijitahidi kujizuia asisimame,mioyo yao ilikua inagonga kwa nguvu mno na jasho lilianza kutotesha nguo zao huku wakihema kama mbwa!! Fikra za kujutia uamuzi alioufanya zilianza kumtawala Sadiki mloe,atafanya nini sasa katikati ya ile safari?? Hakua na jinsi zaidi ya kuifungua miguu yake iokoe maisha yake.
Upepo mkali wa baridi ulimpita ghafla mzee Rama na kumfanya mwili mzima uite kwa msisimko wa ajabu!! Cha kustaajabisha ule upepo ulipomfikia Sadiki ulimbeba na kutokomea nae maporini!! Sauti yake nzito ya kuomba msaada ilifika vema kwenye masikio ya mzee Rama aliekua hana cha kufanya zaidi ya kutoa macho kwa kutoamini anachokiona,kama mchezo wa kuigiza Sadiki alipotelea kabisa..sauti yake nayo pia ikatokomea huko!!!
Mzigo wa hofu lawama na majuto ukatuama ndani ya moyo wa mzee Rama,alisimama huku mikono ikiwa kichwani,macho yakimtoka na jasho likimchuruza,alijiuliza mara mbilimbili kwanini ule upepo haukumbeba yeye akakosa jibu kabisa,hakujua ya kwamba ile fimbo iliyomkononi ndio iliyomuokoa,mkojo taratibu ulianza kutiririka katikati ya mapaja yake na kufanya nguo aliyoivaa iloe chepechepe,haraka wazo la kutaka kurudi kijijini likamjia kichwani,kwa macho ya uoga alitizama alipotokea na kuona kiza kimetawala,alipotizama na anapoelekea aliona hali ileile!! Harufu ya kifo ikaanza kugonga puani kwake,makelele ya umauti yakaanza kuita masikioni mwake!!
Je atapona na kufanikisha lengo lake???
USIKOSE SEHEMU 32 IJAYO.