Shadrack Sagati
Daily News; Tuesday,December 02, 2008 @21:15
Mawaziri waandamizi wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona, jana walinusurika kupigwa na kikundi la vijana nje ya Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, waliodai kuchukizwa na washitakiwa hao kuachiwa kwa dhamana.
Tukio hilo lilitokea saa 4.55 asubuhi wakati mawaziri hao wanaoshitakiwa kwa kutumia madaraka vibaya na kusababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, walipotoka ndani ya mahakama hiyo kupanda magari warudi nyumbani.
Kundi la vijana, miongoni mwa umati uliofurika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo, lilijaribu kuvamia magari waliyopanda washitakiwa kwa nia ya kuwapiga, lakini ulinzi imara wa jeshi la Magereza uliwanusuru. Wakati vijana hao wakionyesha hasira, ndugu wa washitakiwa walikuwa na furaha ya kujumuika tena na wapendwa wao.
Mramba aliachiwa kwa dhamana na Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja baada ya kuwasilisha hati nne za mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh bilioni 3.1. Hati moja yenye thamani ya Sh milioni 397 ni ya Khatib Senkoro na ya pili ya Haruni Mohamed ina thamani ya Sh bilioni 1.2. Hati nyingine ni ya Kilimanjaro Mines yenye thamani ya Sh milioni 976.4 wakati ya nne ni mali ya Mramba mwenyewe yenye thamani ya Sh milioni 547.
Yona alitoa hati tatu zote zenye majina yake zenye thamani ya jumla ya Sh bilioni tatu. Hati moja ina thamani ya Sh milioni 443, nyingine Sh bilioni 2.2 na hati ya tatu thamani yake ni Sh milioni 420.3. Wiki iliyopita Mahakama Kuu iliwalegezea washitakiwa hao masharti ya dhamana na kuamuru wawasilishe hati za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.9 kila mmoja, badala ya kulipa fedha taslimu kama ilivyoamuliwa awali na Mahakama ya Kisutu.
Vijana waliojaribu kuleta fujo kupinga dhamana hiyo, walidai juma moja walilokaa rumande mawaziri hao wa zamani halitoshi, kwani hao ni wezi wa mali ya umma na wamechangia ugumu wa maisha kwa wananchi wengi. "Hawa ni wezi mtawaachiaje? Hawastahili hawa kuwa nje," alisikika akisema kijana mmoja ambaye alikuwa anazuiwa na askari magereza ili asiwafikie washitakiwa hao.
Jeshi la Magereza liliweka ulinzi mkali wa zaidi ya askari 10, wakiwamo wenye silaha, baada ya kuona ishara za vurugu. Magari yaliyowachukua washitakiwa hao yaliegeshwa karibu na mlango mkuu wa mahakama badala ya ule wa nyuma kuepuka vurugu. Kitendo hicho kiliwapa shida wapigapicha wa magazeti na televisheni, waliokimbia huku na kule kutafuta mahali watakapotokea mawaziri hao wa zamani.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Charles Kenyela, alithibitisha kuwa Mramba na Yona walitolewa mlango wa mbele kuwaepusha wasishambuliwe na wananchi. Washitakiwa hao walilazimika kuondoka haraka bila kusalimiana na ndugu zao waliojazana nje ya mahakama.
Mramba alipanda kwenye gari lenye namba za usajili T521 AFS LandCruiser VX huku Yona akipandishwa kwenye Suzuki Vitara ya kisasa yenye namba za usajili T822 ANR, magari ambayo yaliondoka kwa kasi mahakamani hapo. Vijana ambao walikwama kuwadhuru washitakiwa hao, waliishia kuwazomea, wezi hao... wezi hao
Katika kesi hiyo, Mramba anakabiliwa na mashitaka yote 13 wakati Yona anahusishwa na mashtaka sita ya kushiriki kuipendelea Kampuni ya Alex Stewart kwa kuipa nyongeza ya mkataba kinyume na taratibu. Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini, pia anashitakiwa kwa kutoa mkataba kwa kampuni hiyo bila kuishirikisha ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali. Mramba anashitakiwa pekee kwa kutoa misamaha mbalimbali ya kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart na kusababisha hasara hiyo ya Sh bilioni 11.7. Kesi hiyo itatajwa tena Januari 2 mwakani. Upande wa mashitaka umesema upelelezi bado unaendelea.
.............................................................................................
Swali langu:
Je hizi si dalili wazi za kuchokwa na jamii ya wala nyasi! Yona binafsi amepata wapi mali zote hizo za kujidhamini mwenyewe? Na Mramba je, hizo ni mali zake kwa majina tofauti? kama ni za washirika, wana uhusiano gani na Mramba? Wadau mwageni data.