SoC02 Wizara ya Afya chukueni hili kwani afya zetu, anguko letu ama maendeleo yetu

Stories of Change - 2022 Competition

MAKALANDEI

New Member
Jul 26, 2022
4
2
Sekta ya afya ina mchango mkubwa sana katika maisha ya kila siku kwa kila mmoja katika taifa,hii inapelekea akili yangu kuwaza sekta hii ina uelekeo gani.Je,inaleta anguko ama inaleta maendeleo katika jamii?.Tazama jinsi mnyororo wa afya ulivyo na athari katika jamii,iwapo mtu mmoja ambae ni tegemeo katika familia akipata shida ya kiafya; familia inayumba kiuchumi,kama kaajiriwa taasisi inakosa huduma yake,na pia anaweza kukosa ajira iwapo magojwa yatamzidia,mwisho nchi inakosa nguvu kazi na kukwamisha jitihada za kupunguza na kuondoa kabisa umaskini.

Andiko hili linalenga kubainisha mambo makuu matatu ambayo ni madhaifu katika sekta ya afya,athari zake na nini kifanyike.

Kama nilivyoainisha mchango wa sekta ya afya kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla kuna mengi yamekuwa kero kwa muda mrefu ambayo kama taifa tunapaswa kuyatafakari ama tuendelee nayo au tukubali kufanya marekebisho kwa mstakabali wa taifa.

Kwanza,Ongezeko la watumishi wa afya wasiokuwa ujuzi na weledi katika kazi;Hii imekuwa ni aibu kubwa kwa kada ya afya kwa sasa.Jamii inakosa imani na huduma ya afya tena na hii ni kwa sababu watumishi wengi wa afya kwa sasa wanabahatisha katika kazi zao inafikia wakati jamii inahoji kuhusu ubora wa mitaala na mafunzo ya afya kwa ujumla.Imekuwa ni kawaida kwa watumishi kusubirisha mgojwa huku akitafuta kwenye mtandao aina ya ugojwa ama dawa au ampe dawa/huduma ambayo kimsingi haiendani na ugonjwa.Kwa sekta muhimu kama ya afya hili si sawa hata kidogo kama jamii tunapaswa kutazama upya tumekosea wapi na tufanye nini.

Pili,Vitendo vya rushwa na kukosa ukarimu kwa wagonjwa katika huduma;Si mara ya kwanza sekta ya afya kukumbwa na kashfa hii lakini lazima kama jamii tujiulize kwa nini hili linatokea?kwanini kuhatarisha maisha ya binadamu mwenzio kwa sababu ya rushwa?baadhi ya watumishi wa afya si waaminifu tena lugha chafu na matusi vimekuwa sehemu ya kazi yao,jamii inavyokerwa sana na tabia hii haswa kwa wodi za akina mama haya yamekuwa sehemu ya maisha yao pia hata huduma nyingine hali si shwari.Lazima pia kwenye hili tujiulize tatizo ni kizazi hiki au kuna mahali hapako sawa?.

Tatu,Usumbufu wa bima kushindwa kugharamia baadhi ya huduma ndogo sana;Katika vitu vinavyo fikirisha sana ni bima kushindwa kulipia baadhi ya huduma ndogo sana mfano bima kushindwa kulipia huduma au kifaa cha Shilling 10,000 au hata chini ya hapo.Hili tatizo lipo na ni kubwa sana si mtu mmoja au wawili wanalalamika,maana ya kuwa na bima inapotea kabisa ukikutana na hali hii.

Kumekuwa na athari kubwa sana kwenye jamii kutokana na changamoto nilizoziainisha hapo juu kwa kuwa sekta hii inagusa maisha ya watu moja kwa moja.Hizi ni kati ya athari ambazo hupelekewa na huduma mbovu sekta ya afya;

Kwanza,Vifo visivyotarajiwa na ulemavu wa maisha;Kati ya athari nyingi hizi mbili huumiza zaidi,jamii inapoteza nguvu kazi kwa sababu ya uzembe ambao nimekwisha ueleza hapo juu kama kucheleweshwa kwa huduma pasipo sababu ya msingi,wakati mwingine ucheleweshwaji kutengeneza mazingira ya rushwa.Lakini pia kukosa weledi kwa kushindwa kutibu ugonjwa husika na kutibu ugonjwa usiokuwepo.Itoshe kusema hili haliwezi onekana kama tatizo kubwa mpaka itokee ukutwe na haya mambo mawili kwa kweli inaumiza sana.

Pili,Kuongezeka kwa watu wanaojitibia majumbani bila wataalamu wa afya;Hili ni tatizo jingine ambapo iwapo hatua zisipochukuliwa linaongezeka kwa kasi kubwa sana mtu anajiuliza kwanini niende hospital kumuona daktari ambaye anatumia mtandao kutafuta dawa na ugonjwa ninaoumwa?Mwisho wengi huamua kununua dawa na kujitibia kwa kutumia mtandao pia.Hii kupoteza imani kwa huduma za afya na inaenda mbali sasa na wengine kujiuliza kuna umuhimu gani kwenda kulipia kumuona daktari utadhani kumuona ndio tiba yenyewe?

Kwa kuwa andiko hili linalenga zaidi katika kutoa maoni nini kifanyike kupunguza au kuondoa adha mbalimbali katika sekta ya Afya,kwani jamii yetu inategemea sana sekta hii.Haya ni baadhi ya mapendekezo ya nini kifanyike.

Kwanza,Maboresho katika udahili na mafunzo kada za afya;Kwenye hili vyuo na vyuo vikuu vinavyotoa kozi za afya vinatakiwa kulichukua wadahiliwe wanafunzi wanaokidhi vigezo na kikubwa zaidi mafunzo yafanyike kwa umakini wa hali ya juu.Ni bora kuwa na wahitimu wachache wenye weledi na ujuzi kuliko kuwa nao wengi wasio na weledi wala ujuzi.Hivyo umuhimu uelekezwe zaidi katika ubora wa wataalamu kuliko Idadi ya wataalamu.

Pili, Weledi na ujuzi upewe kipaumbele na mchujo makini katika kuajira iwe kwa taasisi binafsi au serikalini ili kupata watu wenye vipaji,weledi,majitoleo na kupenda wanachokifanya.Imekuwa kawaida sana madaktari walio kwenye mafunzo na watumishi wengineo kuachiwa watoe huduma hii inakatisha tamaa sana kwenye sekta yetu ya afya ni vyema sasa kuhakikisha watumishi wazoefu hawawaachi waliokwenye mafunzo peke yao wakati wa kutoa huduma.

Tatu,Mifumo ya utawala ifanye kazi yake ipasavyo katika maeneo ya huduma za afya husika;Katika vitu muhimu sana ni utawala katika maeneo ya huduma za afya,pasipo utawala bora hata watumishi wema waweza kubadilika.Matatizo mengi katika huduma za afya huanza iwapo utawala haufanyi kazi yake inavyotakiwa vitendo vya rushwa,kucheleweshwa kwa huduma na lugha chafu kwa wagonjwa haya yote yanaweza kuepukika iwapo utawala wanawajibika ipasavyo.Nitoe rai kwa tawala za huduma za afya wakumbuke wasipowajibika kukemea vikali utovu wa nidhamu na kuhamasisha uwajibikaji wanaua taifa katika mnyororo mpana wa kiuchumi.

Nne,Maboresho ya mara kwa mara yafanyike katika malipo ya watumishi makini na wenye kupenda kazi zao;Maboresho ni muhimu sana kwa kadri ya bidii wanayoonyesha na kufanyika kwake kutapunguza tatizo la rushwa nje ya ukweli kwamba rushwa ni tabia inayojitengeneza siku kwa siku.Ikiwa ikazingatiwa katika mchakato mzima wa kuwapata hawa wataalamu hata kama ni wachache wakapatikana wenye ubora,kama taifa tutafaidika sana hata zaidi ya hilo ongezeko katika malipo yao,kwani watafanya kazi kwa moyo pasipo manung’uniko na kuchochea ubunifu mkubwa.

Mwisho,Umuhimu wa sekta hii hauelezeki ipasavyo,lakini naweza ifananisha na uhai kwa kuwa si kwa kuwa inahusika na kutunza uhai wa watu bali pia ni pumzi ya uhai wa sekta nyingine.Itoshe kwa watumishi wa kada hii kuelewa umuhimu wao na kuepuka aibu hii,ni ajabu Daktari kukesha klabu na kuamkia wodini,au ndugu wa mtumishi kusema wazi nikimkuta ndugu yangu ndie anahudumu siwezi tibiwa nae kwa kuwa nina mashaka na taaluma yake.
 
Back
Top Bottom