Makachero wamfuatilia Zitto hadi Kenya
Mwandishi Wetu
Agosti 6, 2008
WIKI moja kabla ya Mbunge wa Tarime (CHADEMA), Chacha Zakayo Wangwe kufariki, Mbunge kijana wa Kigoma Kaskazini kupitia chama hicho, Zitto Zuberi Kabwe, alizushiwa kifo huku akifwatiliwa na watu wasiojulikana hadi nchini Kenya alikokwenda kikazi, Raia Mwema imeambiwa.
Uchunguzi wa Raia Mwema umethibitisha kuwepo kwa taarifa kadhaa za uvumi wa kifo cha Zitto, sambamba na taarifa ya kufuatwa kwake na watu watatu kutokea Dar es Salaam, Nairobi na hatimaye Mombasa.
Wangwe alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea Julai 28, 2008 katika eneo la Pandambili, Kongwa mkoani Dodoma akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam, ajali ambayo hadi sasa imezidi kugubikwa na utata na malumbano ya kila aina kila kukicha ikiwa ni pamoja na mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa vyama vya upinzani.
Viongozi wa CHADEMA waliithibitisha Raia Mwema kupokea taarifa za uvumi wa kifo cha Zitto Kabwe, kabla ya kufanikiwa kumpata kwa simu akiwa Mombasa, alikoenda kwa shughuli za kibunge.
Zitto mwenyewe alilithibitishia Raia Mwema kuwapo kwa taarifa hizo ambazo alisema alishindwa kufahamu chanzo na sababu za kuwapo kwake, na alikataa kueleza kwa undani kuhusu suala la watu waliomfwatilia hadi nchini Kenya kwa maelezo kwamba suala hili nimeliacha mikononi mwa mamlaka zinazohusika.
Ni kweli nilifuatwa na watu watatu, wakati ambao naelezwa nilikuwa nimevumishiwa kuwa nimekufa na kwa kuwa sikuwa naelewa sababu ya uvumi huo, niliziarifu mamlaka zinazohusika za Tanzania na Kenya na nilitakiwa niendelee na shughuli zangu bila wasiwasi wowote, alisema Zitto.
Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja watu hao watatu walioonekana Dar es Salaam, Nairobi na Mombasa walikua raia wa nchi gani na walikuwa na malengo gani baada ya kutokuwapo taarifa zozote za walikopelekwa na vyombo vya Serikali nchini Kenya baada ya kukamatwa na kuhojiwa katika uwanja wa ndege wa Mombasa.
Barua ya CHADEMA kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini ilirejea, kwa ufupi, tishio hilo kwa viongozi wa CHADEMA na vyama vya siasa na kuomba ulinzi kwa viongozi wake ambao wamekua wakitishiwa maisha na hata kuzushiwa vifo bila kuingia undani wa suala hilo.
Hivi karibuni wabunge wa CHADEMA wamekuwa wakipata taarifa za vitisho pamoja na kuzushiwa vifo kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mikononi na ujumbe huo kusambazwa sana kama ilivyoripotiwa kwako na Mheshimiwa Zitto Kabwe. Tunaomba wabunge wetu wapatiwe ulinzi na pia taarifa hizo zifanyiwe kazi kwa kina, imeeleza sehemu ya barua hiyo ya CHADEMA.
Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa CHADEMA kutajwa kutishiwa maisha baada ya taarifa za awali za Dk. Slaa mwenyewe kutishiwa maisha mara kadhaa baada ya kutolewa kwa kile kilichofahamika kuwa orodha ya aibu ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi. Wengi wao katika orodha hiyo ni viongozi wenye madaraka ndani ya Serikali, baadhi yao wakiwa tayari wamekwisha kujiuzulu nafasi zao.
Baada ya kifo cha Wangwe, hali ya wasiwasi sasa imezidi kuingia miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa wakiwemo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao nao wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu kutokana na vitisho na hata kuvumishiwa vifo.
Miongoni mwa waliowahi kuvumishiwa kifo, yumo pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyopitia mkataba wa mradi tata wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kampuni ya Richmond Development LLC ya Marekani, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye wakati uvumi huo ukiendelea alikua mgonjwa.
Dk. Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela kupitia CCM alivumishiwa kifo siku chache baada ya kuugua ghalfa akiwa ndani ya Bunge na kutakiwa kupumzika akiendelea na matibabu, ugonjwa uliotaka kuhusishwa na kitu kilichodaiwa kumwagwa ndani ya ukumbi wa Bunge. Uchunguzi wa kitaalamu, hata hivyo, ulibaini kutokuwapo kwa aina yoyote ya sumu au kemikali yenye madhara yoyote.
Pamoja na kuwapo vitisho na hofu kubwa miongoni mwa wabunge na wanasiasa machachari, kifo cha Wangwe kimezidisha hofu miongoni mwa wanasiasa, hususan baada ya kuendeelea kuwapo kwa utata kuhusiana na kifo cha mbunge huyo machachari ambaye hata ndani ya chama chake cha CHADEMA alikuwa akiwachachafya mno.
Wakati huo huo, kifo cha Wangwe kimezidi kugubikwa na utata, na sasa inaelezwa kwamba kampeni za kisiasa kutafuta mrithi wake, zilianza kabla hata ya mwili wa mbunge huyo kuzikwa wilayani Tarime. Kampeni hizo zimeelezwa kuendelea hadi sasa kwa makundi mbalimbali ya kijamii kujaribu kutafuta mtu wa kugombea kiti hicho.
Habari kutoka Tarime zinaeleza kwamba, viongozi wa CUF, NCCR-Mageuzi na TLP waliokuwapo Tarime, walifanya mazungumzo na mwanasiasa mmoja wa Tarime wanayemgombea awanie ubunge kupitia vyama vyao, mazungumzo yaliyofanyika ndani ya chumba alipokua amelazwa marehemu Wangwe kabla ya mazishi.
Kwa mujibu wa habari hizo, hata malumbano yasiyo rasmi yaliyoibuka sasa miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo na wale wa CHADEMA, yanaelezwa ya kuwa ni sehemu ya kampeni hizo za kuelekea uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, ambao kila chama kinatajwa kutaka kusimamisha mgombea kwa imani ya kulitwaa jimbo hilo.
Viongozi wa CUF, Ibrahim Lipumba, Augustine Mrema wa TLP na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi walikutana na waandishi wa habari siku moja tu baada ya Zitto kukutana na Jukwaa la Wahariri, akilalamikia taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na matukio ya vurugu wakati wa msiba wa Wangwe, wilayani Tarime.
Lipumba alikwenda mbali zaidi na kusema kwamba kichwa cha Wangwe kilipondeka na kwamba kijana Deus Francis Mallya aliyekuwapo katika ajali hiyo na Wangwe ni jasusi ambaye alichukua mafunzo nchini Libya, tuhuma ambazo zimeelezwa kuwa nzito zikihusisha nchi nyingine yenye uhusiano na Tanzania.
Lipumba ni kiongozi hatari. Kusema Mallya ni jasusi ni kumhukumu na je, ikigundulika sio? Kusema Wangwe kichwa kimepondeka pia ni hatari kwa kuwa familia na waliokuwamo katika uchunguzi wa daktari wametoa taarifa tofauti. Siasa za Tanzania sasa zimekua chafu sana, anasema mwanasiasa mmoja ndani ya upinzani.
Tayari imeripotiwa kwamba Mallya alikwenda Libya katika mkutano, akiongozana na vijana wengine wa vyama vya upinzani na CCM pamoja na viongozi wa dini, safari ambayo Serikali ya Tanzania na Libya zilikuwa na taarifa nayo tofauti na taarifa za kuwa kijana huyo alikwenda kuchukua mafunzo ya kijasusi ama ya kijeshi.
Baba wa Mallya, Mzee Francis amenukuliwa na gazeti moja la kila siku akilalamikia kauli ya Lipumba akisema ni kumhukumu kabla ya uchunguzi wa vyombo vya dola kukamilika na kuthibitisha tuhuma hizo.
Katika safari ya Libya, Mallya anaelezwa kuwa pamoja na watu mbalimbali akiwamo Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Juma Hassan Kilimbah, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mamuya na Makongoro Nyerere ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara.
Wengine katika safari hiyo anatajwa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Simba, Shehe Seleman Kilemile na Hebron Mwakagenda, ambaye ni kutoka Leadership Forum.
Tayari Mallya amefikishwa mahakani akifunguliwa kesi ya usalama barabarani namba TR 103/08 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, akidaiwa kuendesha gari kwa mwendo kasi na kusababisha kifo cha Wangwe na kuendesha gari bila leseni.
Wakati Chama cha Mapinduzi nacho kikituhumiwa kuchochea mtafaruku ndani ya vyama vya upinzani kwa kuhofia wabunge wake kuhamia vyama hivyo kutokana na kuyumba kwa chama hicho, Wangwe anatajwa kuwa mmoja wa wanasiasa ambaye angetumika kwa kazi hiyo.
Mbali ya ushahidi wa nyaraka ulionukuliwa katika gazeti la Mwananchi la jana, maelezo ya watu mbalimbali yanaeleza wazi kuwapo kwa taarifa za mbunge huyo kuweza kukivuruga chama chake na kukihama kujiunga na CCM.
Kwa nyakati tofauti, maofisa kadhaa wa CCM, ngazi za mikoa na Makao Makuu, wameiambia Raia Mwema wiki hii kwamba maandalizi ya Wangwe kuhamia CCM yalikwisha kukamilika kutokana na yeye kudai alikuwa hatendewi haki ndani ya CHADEMA.
Maandalizi ya kuja CCM yalikwisha kukamilika. Sisi uongozi wa CCM wa Mkoa wa Mara ambako ndiko anakatoka Chacha Wangwe tulikuwa kama waratibu wa suala hilo, anasema kiongozi mwandamizi mmoja wa CCM Mkoa wa Mara, aliyezungumza na Raia Mwema, wiki hii mjini Dodoma.
Anaongeza kiongozi huyo: Alikuwa (Wangwe) akienda Dar es Salaam ambako baada ya kushiriki mazishi ya Mzee Bhoke Munanka, na kusikiliza maendeleo ya kesi yake dhidi ya uongozi wa CHADEMA, angekutana na waandishi wa habari kusema kile alichokuwa akiamini kuwa hakiendi sawa ndani ya chama chake na baada ya hapo angekuja CCM.
Alipanga kuanika hadharani kile alichokiita yeye uozo ndani ya CHADEMA wa ufujaji wa fedha za ruzuku na upendeleo katika kuteua wabunge wa viti maalumu ambao amekuwa akidai ulifuata zaidi ukabila badala ya sifa.
Madai mengine ya Wangwe ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara ni pamoja na kwamba majimbo, kama la kwake hayakuwa yakifaidika na fedha za ruzuku ambazo kimsingi zinatolewa kutokana na idadi ya viti vya ubunge ambavyo chama kinavyo na kwamba badala ya kwenda majimboni fedha hizo zilikuwa zikineemesha walioko Makao Makuu.
Raia Mwema haikufanikiwa kuzungumza na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba wiki hii, lakini habari za walio karibu naye zimekuwa zikisema kwamba alikuwa na mawasiliano ya karibu na Wangwe kwa ajili ya yeye kuhamia CCM.
Yamekuwapo mawasilino na Ofisi ya Katibu Mkuu na nadhani mambo yalikuwa yakienda sawa, kilichokuwa kinasubiriwa tu ni kwa Wangwe mwenyewe kukamilisha mambo yake CHADEMA ili isionekane kwamba CCM ilikuwa imemrubuni.
Wachunguzi wanasema hata hivyo kwamba suala hilo la kurubuniwa kwa Wangwe, kama hatimaye angehamia CCM, lazima lingeibuka kwa kuwa tayari kuna madai kutoka CHADEMA ya kwamba yeye alikuwa akitoa siri za chama hicho kwa CCM, madai ambayo yanaelezwa kuwa yalikuwa yakimkera sana mbunge huyo na ambayo yalichangia yeye kusimamishwa asiendelee na nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA.
Wachunguzi wanasema kifo cha Wangwe kitaendelea kwa muda kuibua mambo mengi kutokana na kuwa katika kipindi cha karibu mwaka mzima uliopita Wangwe mwenyewe alikuwa katika simulizi za mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini.