BAADA ya bomoa bomoa, yameibuka madai kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wilayani Kinondoni, Anna Luvanda ‘Mama Makete' amekuwa akiwatumia wananchi wanyonge kwa maslahi yake binafsi kuvamia maeneo yaliyopo katika wilaya hiyo.
Agosti 22, mwaka huu Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na vyombo vya dola, ilibomoa nyumba zaidi ya 300 zilizojengwa katika Kata ya Mabwepande na Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa madai ya kuvamia eneo hilo. Pamoja na hilo, Mama Makete anadaiwa kuwapa pesa kinamama na watoto na kuwapakia katika magari binafsi na kisha kuwatelekeza karibu na ofisi ya Ikulu.
Akisoma taarifa ya umoja wa watu waliovamiwa maeneo yao jijini Dar es Salaam juzi, katika mkutano uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Kawe, Kaimu Mwenyekiti wa umoja huo, James Mramba, alidai Mama Makete amekuwa akitumia cheo chake kwa maslai binafsi. Mramba alidai kuwa Mama Makete aliwakodisha kinamama na watoto wao na kuwalipa ujira mdogo ili wafike katika ofisi za Ikulu waonane na Rais Jakaya Kikwete.
"Huyu kigogo ndiye chanzo cha vurugu zote za uvamizi wa maeneo katika wilaya hii, amekuwa akiwatumia wanyonge na mbaya zaidi wakati wa bomoa bomoa aliwachukua wanawake na kuwapeleka karibu na Ikulu.
"Aliwafikisha hapo ili waende wakaeleze kuwa wameonewa na manispaa na waweze kupatiwa maeneo hayo," alidai Kaimu Mwenyekiti huyo.
Aidha, alidai Mama Makete amekuwa akifadhili wananchi waliovunjiwa maeneo hayo kwa sasa kwa kuwapatia hifadhi katika eneo la machimbo ya kokoto ambako wameweka kambi.
Alibainisha kuwa, anashindwa kujitokeza hadharani kwa kuwa anajua eneo analomiliki hakulipata kihalali.
Akichangia katika mkutano huo,
Mbunge wa Viti Maalumu, Rita Mlaki (CCM), alisema serikali imeshafanya utafiti wa kina juu ya kuwepo kwa kigogo huyo na ripoti yake imeshafika mezani kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick.
"Hatuna haja ya kulalamika juu ya jambo hilo… ninajua Serikali ya CCM haiwezi kumkubatia mtu kama huyo," alisema.
Mlaki alidai kwa sasa kuna uhuni unafanywa na wavamizi hao ambapo wanajipanga na kuandaa nyaraka, ili ionekane wazi kuwa maeneo hayo ni mali yao kihalali.
Huku akikitetea chama chake, Mlaki alidai kuwa CCM haiwezi kukubali kigogo huyo aendelee kukichafua chama hicho, hivyo anaamini hatua zaidi zitachukuliwa kukomesha vitendo hivyo vya kifisadi. Hata hivyo, alisema ingawa wavamizi walikimbilia Tume ya Haki za Binadamu, bado wanayo nafasi ya kukutana na kiongozi wa tume hiyo ili kujua undani wa maeneo hayo.
"Nasi tusimame imara, Tume ya Haki za Binadamu ninawafahamu viongozi wake na tunaweza kwenda kule na tumevumilia vya kutosha kwa kuwa tunaiheshimu serikali maana nasi tulikuwa na uwezo wa kuwa Mungiki," alisema.
Naye Seif Magugu, alidai kigogo huyo anamiliki machimbo ya kokoto na ndiye mfadhili mkuu wa vijana wanaoendesha vitendo vya kibabe katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mama Makete aliziita ni za kisiasa na zina lengo la kumchafua.
Alifananisha tuhuma hizo na methali ya ‘akutukanaye hakuchagulii tusi' na akasema hawezi kuitumia Ikulu kuendesha vitendo viovu.
"Mimi nina malori matano na hayo sikai nayo, sasa ni muda upi niliwabeba hao watu na kwenda kuwashusha Ikulu?" alihoji.
Alisema eneo analodaiwa kuvamia aliuziwa miaka nane iliyopita, hivyo kama kuna mtu ana umiliki halali wa eneo hilo, hana budi kujitokeza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema, Jeshi la Polisi litafuatilia juu ya kuwepo kwa kikundi cha wavamizi kuweka kambi katika eneo la mchimbo ya kokoto.
Imeandikwa na Betty Kangonga
Source: Tanzania Daima
http://www.dullonet.com/?p=24350