Watoto wawili wenye uzito mkubwa wafikishwa Mloganzila

Wizara ya Afya Tanzania

Official Account
Oct 1, 2020
58
124
Watoto wawili wa miaka saba na mitano wakazi wa Makole mkoani Dodoma wenye uzito uliopitiliza wamefikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya maradhi yanayowakabili.

Akiongea baada ya kuwapokea Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dkt. Asha Iyulla amesema wameanza kwa kuwafanyia vipimo vya awali ikiwemo kuwapima uzito ambapo wamebaini mkubwa ana uzito wa kg 76 na mdogo ana uzito kg 62, vipimo vingine ni pamoja na vipimo vya damu.

“Vipimo hivi tulivyofanya leo ni vya awali, kesho watafanyiwa vipimo vya ziada ikiwemo kupimwa wingi wa mafuta kwenye damu katika kliniki yetu ya uchunguzi na matibabu ya wingi wa mafuta kwenye damu pamoja na kufanya vipimo vingine ili kubaini tatizo linalowakabili” ameongeza Dkt. Asha.

Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao Bi. Vumilia Elisha amesema amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila kwani yamempa faraja na matumaini ya watoto wake kupona maradhi yao.

Kuletwa kwa watoto hao kunafuatia kauli ya Mkurugenzi Mtendaji, Prof. Mohamed Janabi kuwa hospitali ipo tayari kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa watoto hao ambao mama yao alionekana akiomba msaada kupitia video na picha iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
 
Back
Top Bottom