Watoto wenye jinsia tata wafanyiwa upasuaji Muhimbili

Wizara ya Afya Tanzania

Official Account
Oct 1, 2020
58
124
Hospitali ya Taifa Muhimbili imewafanyia upasuaji wa mfumo wa mkojo na haja kubwa kwa watoto 31 na kati ya hao sita walizaliwa na jinsia tata, ambapo upasuji huo umefanywa na Madaktari Bingwa wa MNH kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Ireland na mwingine kutoka Bahrain.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema ni muhimu kwa wazazi kujifungulia kwenye vituo vya afya ili watoto wakizaliwa waweze kufanyiwa uchunguzi wa kina na kugundulika mapema ili waweze kuapta matibabu mapema.

“Mtoto akigundulika mapema atafanyiwa upasuaji na kurudi katika hali yake kama inavyotakiwa na mtoto huyo atakapokuwa ataweza kuchangamana na watoto wengine hata akienda shule atasoma kwa uhuru na kutimiza ndoto zake ”amesema Prof. Janabi.

Aidha ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwanyooshea watoto vidole pale wanapoona kuwa wanafanya tabia ambazo si za kawaida badala yake wawalete hospitali ili wafanyiwe uchunguzi na kupatiwa msaada.

Akizungumzia umuhimu wa kufanya uchunguzi mapema, Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Watoto MNH Dkt. Petronilla Ngiloi amesema mtoto anaweza kuzaliwa na muonekano wa jinsia ya kiume kumbe kwa ndani ni mtoto wa kike au mtoto anazaliwa na muonekano wa ya jinsia ya kike kumbe ndani ni mtoto wa kiume, tatizo linakuja wakati wa balehe yule ambaye ni wakike akalelewa kama mvulana wakati wa balehe anapata yale maunbile ya kike kama kutoa matiti kupata hedhi na kadhalika”amesema Dkt. Ngiloi

Akizungumzia ukubwa wa tatizo Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo na Upandikizaji wa Figo Dkt. Gabriel Mtaturu amefafanua kuwa kati ya watoto Elfu Tano wanaozaliwa mmoja ana jinsia tata na kati ya watoto 300 mmoja anazaliwa akiwa na jinsia zilizoungana.

Dkt. Mtaturu amesema watoto waliofanyiwa upasuaji walikuwa katika makundi manne ambapo baadhi walikuwa na jinsia tata,wengine walikuwa na maumbile ya kike ila ndani walikuwa na maumbile ya kiume, mmoja alikuwa na sehemu mbili za kutolea haja ndogo na mwingine alikuwa wakike ila hana sehemu za siri hivyo walimfanyia upasuaji rekebishi na kumtengenezea maumbile ya kike.
 
Back
Top Bottom