Kwa mtazamo wangu, tunaodhani kuwa tunajua lugha ya Kiwahili ni wengi sana. Lakini, kinyume chake ni kuwa wengi wetu hatuijui lugha hii kwa ufasaha. Hata sisi tulioandika humu ukumbini hatuijui lugha hii kwa kiasi tunachokifiria. Mtu akikaa chini kutuchambua, hatachukua muda mrefu kuyaona makosa yetu.
Kitu kibaya zaidi ni kwamba ama hatujui kama hatujui au hatutaki kukubali kuwa hatujui. Kwa hiyo, ni lazima tujue na tukubali kuwa wanao kiharibu au wasiojua Kiswahili fasaha si Watangazaji na Waandishi peke yao bali ni sisi sote.
Tukifikia hatua hii, itakuwa ni mwanzo mzuri sana wa kuibadilisha lugha hii na kuiweka katika mizania ya kuheshimika, kupendwa, kuimarishwa na kuendelezwa katika misingi bora.
Katika kila lugha kuna ile lugha inayokubalika kama lugha ya mitaani. Lakini, tunapoichukua ile lugha ya mitaani na kuiingiza katika shule. redioni, magazetini, kwenye televisheni, mahakamani, bungeni na sehemu stahiki, huo ndio unakuwa mwanzo wa kuiporomosha lugha hiyo katika ujumla wake.
Kwa mfano: hatusemi "kitu hichi" bali tunasema "kitu hiki." Na katika wingi wake, tunasema "vitu hivi." Utagundua mara moja kuwa Ndugu Shy naye tayari kishafanya makosa katika makala yake hii inayokosoa Watangazaji wa Radio Clouds.
Badala ya kuwa walimu, tungekubali kuwa wanafunzi wazuri, tukajifunza kwa bidii lugha yetu hii adhimu. Huu ni urithi wetu wa kujivunia na ni urithi wa vizazi vyetu vinavyokuja.
Tuna mtindo pia ambao mimi binafsi nautumia kama wengi wengine. Mtindo ambao nauita "mtindo mbaya." Huu ni ule mtindo wa kuchanganya lugha, tunao uita Swanglish. Huu mtindo unaudhi sana. Hata pale ambapo lipo neno rahisi na la kawaida, mtu atapenyeza hapo neno la Kiingereza. Hata kama yule anayezungumza naye hatajua maana ya lile neno. Hali ambayo inaufanya ujumbe usifike unakokusudiwa.
Mara nyingi, dhamira hapo ni kuashiria usomi. Yaani, kwetu sisi usomi ni kujua Kiingereza. La haula, laiti tungejua, duniani kuna wasomi wengi mno ambao hawajui Kiingereza.
Imefika wakati, tuwajibike kuijivunia lugha yetu hii ya Kiswahili.