Watalii wenye Figo 1 waanza kupanda mlima Kilimanjaro

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
1677991980651.png
Watu 31 ambao wanaishi na figo moja, wameanza safari ya kuupanda mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuihamasisha jamii kujitolea kuchangia kiungo hicho kwa ndugu jamaa na marafiki wenye uhitaji.

Maadhimisho ya siku ya figo duniani, huadhimishwa Machi 9 ya kila mwaka, kwa lengo la kuhamasisha jamii kutunza viungo hivyo na watalii hao wataadhimisha siku hiyo wakiwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro.

Watalii hao ambao ni Raia kutoka nchini Marekani, walitoa figo zao kuwachangia watu wenye matatizo ya figo duniani na wanalenga kuamsha ari kwa watu kujitokeza kuchangia figo kwa wahitaji na kuonyesha dunia kuwa hata wenye figo moja wanaweza kuupanda Mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.

Kiongozi wa msafara huo wakati wakiwa katika lango la Lemosho, Bobby McLaughlin alisema kampeni hiyo ya kuupanda mlima Kilimanjaro, inafanyika kwa mara ya pili mwaka huu na kwamba mtu anapochangia figo hapati madhara yoyote.

"Tunaanza safari ya kuupanda mlima Kilimanjaro kuihamasisha jamii kujitokeza kuchangia figo kusaidia wenye matatizo ya figo katika maeneo mbalimbali duniani na hii ni kuionyesha jamii unaweza kuchangia figo na ukaendelea kuishi bila tatizo lolote kiafya," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Real Life Adventure Travel inayoongoza watalii hao kupanda mlima Kilimanjaro, Fredrick Chikima amesema watu hao watapanda mlima huo kwa kutumia njia ya Lemosho, ambapo ikifika Machi 9, ambayo ni siku ya figo duniani, watakuwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro.

"Watu hawa wamesaidia kuokoa maisha ya watu kwa kuchangia figo na wengine wametoa kwa watu hata wasiowajua na leo wanapanda mlima huu wakiwa na ujumbe mzito wa kuhamasisha jamii kuchangia figo kwani hata ukibaki na figo moja hupati madhara na unabaki na nguvu ile ile," amesema.

"Kwa njia hii watapanda kwa siku nane na Machi 9, ambayo ndiyo siku ya figo duniani watakuwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, hii ni hamasa kubwa kwetu watanzania tuamke kuupanda mlima huu kwani inawezekana kuupanda hata kwa wenye figo moja," amesema.

Naye ofisa uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Daudi Gordon amesema watu hao kupanda mlima ni hamasa kwa Watanzania na watu wengine duniani kote kutambua kuwa nao wanaweza kupanda mlima Kilimanjaro.

"Kuna watu wengi wamekuwa na hofu ya kupanda mlima huu wakihisi watapata changamoto mbalimbali za kiafya, sasa watu hawa wenye figo moja, wanahamasisha jamii kuwa kila mmoja anaweza kuupanda mlima huu.

“Sasa niwakaribishe Watanzania wote kujitokeza kwa wingi ili kuchochea ongezeko la utalii wa ndani," amesema.

MWANANCHI
 
 
Back
Top Bottom