Majira ya saa moja jioni ya leo, nilikuwa na rafiki yangu maeneo ya Mlimani City, Dar er Salaam tukijadili masuala ya kimaisha na kisiasa sawia. Katikati ya mazungumzo yetu, rafiki yangu huyo aliibua hoja ambayo ilituingiza katika tafakuri nzito. Alinieleza kuwa jirani tu na eneo tulilokuwepo kulikuwa na pilika pilika na hamasa zisizo kifani za watu wakijiandaa kuingia Mlimani City Conference Hall kushuhudia utoaji tuzo za Kilimanjaro Music.
Akikubaliana na kauli iliyopata kutolewa na Ernesto Che Guavara, mara baada kutoka kusaidia harakati za ukombozi nchini Congo, kuwa Waafrika kwa hulka zao, wanapenda sana starehe,waoga na wasio tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya kujikomboa wao wenyewe, rafiki yangu huyo,alitanabaisha kuwa tabia na matendo ya wanasiasa wetu,kama zao la jamii yetu, yanaweza kuthibitisha dai hili:
Wakati Mhadhiri mwandamizi wa UDSM, Prof. Chachage S. Chachage, anafariki dunia, wakati huo yeye akiwa mwaka wa mwisho Mlimani, hakuona viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa na kiserikali wakati wa kuaga mwili wa marehemu Chachage katika ukumbi wa Nkurumah. Aidha, kila mwaka UDSM hufanya kongamano la kumkumbuka Chachage, lakini viongozi wetu wa kisiasa na kiserikali,kama kawaida yao, hawahudhurii kabisa.
Nikakumbuka matukio kadhaa ya miaka ya karibuni:
Prof. Haroub Othumani aliaga dunia, wanasiasa na viongozi wachache wa serikali walihudhuria mazishi. Hali ilikuwa hivyo pia siku chache baada ya kifo chake, Jumuiya ya Wanataaluma wa UDSM, UDASA ilipoandaa mhadhara wa kumbukumbu ya marehemu.
Mwaka mmoja, baada ya kifo chake, UDASA waliandaa tena mhadhara wa wazi kumkumbuka marehemu na kama ilivyo ada yao, wanasisa na viongozi wetu wa serikali hawakujitokeza.
Mwaka 2010, Prof. Jwani Mwakyusa wa UDSM alifariki dunia, na mwili wake uliagwa katika ukumbi wa Nkurumah. Mbali na Dkt. Harison Mwakyembe na Prof. Mark Mwandosya na wanasheria wengine waandamizi, viongozi wetu wengine wa kitaifa, kwa mara nyingine tena, hawakuonekana. Hali ilikuwa hivyo pia katika misiba ya Prof. Christant Kamuzora, Prof. Sam Mushi, Dkt. Ndibalema Alphonce na wengine wengi.
Hivi karibuni, taifa limempoteza ndugu yetu mpendwa, Steven Kanumba ,ambaye kwa kweli ana mchango mkubwa katika kukuza sanaa yetu kimataifa. Sote tumeshuhudia jinsi viongozi wetu wa kisiasa na kiserikali walivyojitokeza kwa wingi kabisa na kikamilifu kabisa nyumbani kwa Marehemu, katika kumuaga na hatimaye katika mazishi yake.Sitaki nieleweke kuwa ninapinga viongozi wetu kuhudhuria mazishi ya wasanii wetu.
Hoja yangu ni kuwa kwanini sasa inaonekana ni kawaida, wanasiasa na viongozi wetu na Watanzania kwa ujumla wetu tunakuwa wazito kuhudhuria katika misiba ya Wanataaluma wetu ambao wamepata kutoa mchango mkubwa katika maeneo yao ya kitaaluma ikiwemo kuandaa wataalamu mbalimbali na michango yao katika kuleta maarifa mapya kupitia tafiti, machapisho na vitabu vyao?
Kwanini tunaenenda hivi? Na kwanini tusibadilike?
Karibu tujadili.