RAFIKI yangu, sitamtaja jina ambaye wote tunasoma chuo kimoja hapa Shanghai anapenda sana wasichana wa kichina. Rafiki yangu huyu Mmalawi, anasomea shahada ya kwanza ya lugha ya kichina na hivyo bado ni kijana. Katika harakati zake za ‘kutongoza' wasichana wa kichina, anakiri kuwa siku zote hudanganya kuhusu utaifa wake.
Rafiki yangu ananiambia: "Nikisema ninatoka Afrika siwezi kukubaliwa. Kwa Wachina wengi, Afrika ni msamiati mwingine unaomaanisha ‘umasikini', na hapa China, fedha ni kigezo muhimu katika uhusiano wa kimapenzi baina watu. Kama ni lazima useme unatoka Afrika, basi walau taja Afrika Kusini na hapo kidogo utaonekana wa maana".
Ukiwa mgeni unayeishi China, utaifa na rangi ya ngozi yako vinaweza kuwa faida au hasara katika kurahisisha au kufanya maisha yako yawe magumu. Kwa ujumla Wachina, wanathamini watu wanaotoka katika nchi tajiri, maana wao wanaleta fedha, na wanachukia wanaotoka nchi masikini kwa sababu wanaamini wao wanakuja kuchuma.
Mmarekani ni kama ‘mungu' wao hapa. Wazungu wa Ulaya kadhalika wanapendwa. Waarabu nao wanakubalika kiasi kwa sababu ya fedha. Kama unatoka nchi masikini ikiwemo za Kiasia kama Tajikistan, Uzbekhstan na nchi nyingine zinazoishia na …'stan', una matatizo. Mtu mweusi ndio kabisa. Mtu mweusi anayetoka nchi zilizoendelea atapendwa baada ya kufafanua kuwa yeye sio mweusi wa Afrika.
Katika hali hii ya unyanyapaa, mtu mweusi anaathirika mara mbili. Kwanza, kutokana na ukweli kwamba anatoka nchi masikini na pili ni kuwa na ngozi nyeusi. Kwa Wachina wengi, kuwa tu ‘mweusi' – hata bila kujali kipato, ni tatizo. Mambo kadhaa yanathibitisha ukweli huo.
Kule Beijing, Waafrika wamekuwa wakilalamika kuwa madereva wa teksi wengi hawasimami kama wakimwona abiria mweusi. Baadhi ya abiria weusi wamekuwa wakiwatumia Wachina kuwasimamishia teksi! Hayo ni ya kuambiwa. Yapo niliyoyashuhudia mwenyewe.
Jumamosi iliyopita nikiwa na rafiki Mtanzania mwenzangu (jina namhifadhi) tulipanda treni na kushuhudia ‘kinyaa' cha wazi cha baadhi ya Wachina wanapokutana na Waafrika. Tulipoingia ndani ya treni, hakukuwa na viti (siti) zilizo wazi na hivyo kutulazimu kusimama. Nilikuwa wa kwanza kupata siti. Kisha baadaye mwenzangu naye akapata, lakini, mara tu baada ya yeye kukaa majirani zake waliokaa upande wa kulia na kushoto, mwanamke na mwanamme, na ambao hawakuwa katika msafara mmoja, wakanyanyuka na kutafuta siti nyingine. Hawakutaka kukaa na mtu mweusi.
Katika tukio jingine lilitokea tukiwa ndani ya duka moja kubwa, siku hiyo hiyo, tulipofika kwenye deski la kulipia, mhudumu alizikagua fedha tulizotoa, akizigeuza juu chini, na kuzikodolea macho kwa umakini, kuthibitisha kuwa ni halisi. Wateja waliotangulia mbele yetu fedha zao hazikukaguliwa namna ile.
Kama haitoshi, baada ya kutuhudumia, wakati tumekwishatoka katika meza ya malipo, wateja walio nyuma yetu wakamwambia mhudumu kuwa hatujalipia chupa ya maji, ambayo wao hawakujua kuwa tuliingia nayo. Mhudumu akatufuata, na bila kuzungumza nasi akachukua ile chupa ya maji ambayo mwenzangu alikuwa ameishikilia mkononi na kuangalia lebo. Akagundua kuwa sio ya duka lao, lakini hata hivyo alikwishatufedhehesha.
Huu ndio ubaguzi wa kimyakimya wa China. Hawakupigi au kushambulia mwili wako. Wanakuua kihisia.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba unyanyapaa wa rangi hauathiri mwafrika mweusi tu, hata mchina mweusi, (labda awe na fedha). Hapa China, rangi nyeusi inanasibishwa na ukulima na umaskini. Nimeambiwa na mwenyeji mmoja kuwa kuna mji fulani huitwa ‘waafrika wa China' – wengi ni wahamiaji mijini, wanafanya kazi duni, ni maskini na tabia zao ni mbaya!
Zipo sababu zinazochangia mtazamo hasi wa baadhi ya Wachina dhidi ya Waafrika. Kwanza, jamii ya China kwa muda mrefu imejifungia, ikiishi katika dunia yao. Njia zao kuu za kupata taarifa ni kupitia vituo vya televisheni vyao wenyewe, redio zao, magazeti yao na mitandao yao ya kijamii iliyochukua nafasi ya Facebook, Twitter, Blogu, Youtube. Watapata wapi muda wa kujifunza kuhusu mataifa mengine? Hapa China ni wageni wanaoruhusiwa kuona televisheni za nje. Katika vyombo vya China, hakuna habari nyingi za Afrika na zilizopo nyingi ni kuhusu vita, ukimwi, umasikini na kadhalika.
Nakumbuka katika siku ya mwisho ya masomo ya lugha ya Mandarin kwa muhula ulioisha, somo lilihusu majina ya wanyama, mwalimu wangu alionyesha kwa kutumia projekta picha ya mbuga mojawapo ya wanyama iliyoko Afrika na kisha akaniuliza kwa mshangao nyumba mbona hazionekani. Eti, yeye alijua kuwa Afrika yote ni mbuga tu na kwamba tunaishi porini na wanyama. Mwalimu wangu mwingine nilipomfuata wiki chache baada ya kuanza masomo ili kutaka kujua Bara la Afrika linaitwaje kwa lugha ya kichina, alikuwa hana uhakika kama Afrika ni bara au nchi!
Ujinga huu ndiyo kwa kiasi fulani unachangia dharau na ubaguzi wa chini chini dhidi ya watu weusi hapa Shanghai. Unatembea mtaani, Wachina wengi wanakuangalia utadhani wameona kiumbe cha ajabu kilichodondoka kutoka mbinguni. Kwa rafiki zangu ambao rangi yao nyeusi iliyokolea, dharau ya Wachina wanapowaona ni mara mbili zaidi. Wengine wanakuuliza eti ni kweli kuwa Waafrika ni weusi kwa sababu ya jua kali. Na hii ni Shanghai, jiji la kubwa zaidi la China.
Ipo dhana pia kuwa Waafrika tuliopo hapa China tumekimbia nchi zetu zenye dhiki za kutisha na kuja ‘kuhemea' kwenye nchi yao. Hawa hawajui kuwa kuna Wachina wengi waliopo Afrika ambao nao wamekimbia shida za kwao, wakifanya biashara za kimachinga ambazo huenda sisi hatufanyi kwao.
Kadhalika, wapo wachina wanaofikiria pia kuwa wanafunzi tunaofadhiliwa kwa udhamini wa serikali tunafaidika kwa gharama yao, wakati wao wenyewe wanahitaji msaada wa serikali, wakisahau kwamba kampuni za nchi zao zipo kila nchi ‘zikipurura' maliasili zetu, na pia tumekuwa soko la bidhaa duni la China. Wanavuna mabilioni ya faida kwa kila senti moja wanayotusomeshea.
Zipo fikra kuwa Waafrika wenyewe waliopo China ni sababu ya huu‘unyanyapaa' kwani baadhi yao wanajihusisha na vitendo viovu na kupelekea Wachina wengi kuamini kuwa sisi ni wezi, majambazi na wauza madawa ya kulevya. Unaweza kudhani kuwa ni hoja yenye mashiko ukizingatia taarifa za Waafrika tunazozisikia huko nyumbani za kukamatwa kwa Waafrika wanaojihusisha na dawa za kulevya. Hata hivyo, vyombo vya habari vya China vinaarifu matokeo ya uhalifu mengi zaidi kuliko hayo ya waafrika. Halafu kama tatizo ni uhalifu mbona kuna wachina wahalifu wanaomaliza tembo wetu lakini hatuwabagui.
Kuna mambo mengi ya ubaguzi dhidi ya weusi yanayotokea hapa China hususan katika ajira na kwenye taasisi za elimu. Kwa ujumla kwa baadhi ya wachina (sio nwachache, ingawa sitaki kusema wengi), kila mwafrika ni mhalifu, masikini na dhaifu kitaaluma mpaka atakapothibitisha vinginevyo.
Huwa nacheka na kusikitika pale ambapo mara nyingi ninapotembea hujitokeza mchina kutaka kuniuzia bangi. "Mtu mweusi!? lazima anavuta tu!", ndivyo inavyoonekana wanavyofikiria.
Hata hivyo, si Wachina wote ambao wana mitazamo ya dharau na ubaguzi. Ni yule yule rafiki Mmalawi ambaye hudanganya utaifa wake anapotongoza wasichana wa kichina ambaye amepata hadi familia ya kichina, ambayo imempokea kama mwana familia. Kila wakati wa likizo huenda kupumzika na kujumuika nao wakimfurahia kama sehemu ya familia, ingawa hata hivyo siku zote hulalamika kuhusu bibi wa familia ambaye alikuwa hajapata kuona mtu mweusi maishani mwake na ambaye humsogelea na kumchunguza kwa ukaribu, (huyu ni binadamu kweli?) kila anapaopata muda.
Njonjo Mfaune - RaiaMwema