Mpango huu wa maaskofu ni pedagogi ya ukombozi kwa wote
Deusdedit Jovin
Julai 8, 2009
NIMEFURAHISHWA na "Mpango wa Kichungaji Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010" kama ulivyoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kusaidiana na Chama cha Wanataaluma Katoliki Tanzania (CPT); kiasi kwamba nimeshawishika kuandika makala kuwahamasisha Watanzania wa dini zote kuunga mkono mpango huo kwani ndiyo ukombozi wa nchi yetu.
Wakiwa wanatimiza wajibu wao wa ‘kufundisha', ‘kuongoza' na ‘kutakatifuza' jamii kwa mawazo, kwa maneno na kwa vitendo, kama wanavyoagizwa na Katiba ya Kanisa Katoliki kuhusu majukumu ya ulei, upadre na uaskofu (Lumen Gentium 1965), wajumbe wa Mkutano wa Wakurugenzi wa Kichungaji na Wajumbe wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), waliamua kuchapisha na kusambaza, sio "Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2010" kama vyombo vya habari vilivyoripoti kimakosa, bali "Ilani (ya) Mapendekezo ya Vipaumbele vya Kitaifa" kwa ajili ya kufanikisha "Mpango wa kichungaji kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010".
Mpango huo unatekelezwa kwa kuzingatia mafundisho rasmi ya Kanisa Katoliki kuhusu haki za binadamu wote.
Hata hivyo, pamoja na ukweli huu ulio wazi, uamuzi wa maaskofu Katoliki umekumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya Watanzania. Upinzani huo, kwa sehemu kubwa, unatokana na baadhi ya wachambuzi ama kujikwaa kwenye kisiki kiitwacho argumenum adhomin au kuamua kukipiga teke kisiki hiki kwa makusudi.
Yote mawili yana matokeo yaleyale; yaani kumhakiki mtoa hoja badala ya kuihakiki hoja iliyowekwa ulingoni. Hivyo, kwa maoni yangu, ni muhimu kuweka bayana hoja ya Kanisa Katoliki na mazingira yanayoizunguka ili tuweze kuitendea haki.
"Ilani (ya) Mapendekezo ya Vipaumbele vya Kitaifa" ni waraka unaofafanua kwa lugha nyepesi jozi za maneno kama vile uhai na kifo, uhuru na utumwa, wema na ubaya, ukweli na uwongo, unafiki na uwazi, elimu na ujinga, afya na ugonjwa, uadilifu na uhalifu, haki na dhuluma, utajiri na umaskini.
Maneno kama vile ubinadamu na uhayawani, kichocheo na matokeo, umakini na usanii, utajiri na umaskini, maendeleo na utapia-maendeleo, kiumbe na muumba, kiwa na ombwe, na jozi za maneno mengine yanayopigana kisogo mithili ya usiku na mchana (conceptual dichotomies).
Umuhimu wa hizi jozi za mawazo yanayopigana kisogo ni kwamba huwawezesha wanadamu kutazama na kuona yanayowazunguka, kusaili waliyoyaona ili kubainisha tatizo lililopo, kusanifu haipotesia zinazoonyesha mapendekezo ya chimbuko la tatizo na dawa yake, kufanya utafiti ili kuthibitisha au kubatilisha haipotesia hizo, kutoa hukumu kwa msingi wa matokeo ya utafiti, kuchukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kutatua tatizo husika, na hatimaye kupima matokeo ya matendo yao mara kwa mara kwa ajili ya uboreshaji.
Kwa mfano, ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha baadhi ya viongozi wa taifa la Uingereza kuona kwamba utawala wa kifalme ulikuwa unakiuka utu wa binadamu, na hivyo kuhitimisha kwamba lilikuwa ni tatizo linalopaswa kutatuliwa ambapo walionyesha njia ya kulitatua kupitia matamko mbalimbali ya haki za binadamu ikiwa ni pamoja na "Magna Carta" (1215), "Habeas Corpus" (1679), na "Bill of Rights" (1689).
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha waasisi wa taifa la Marekani kuona kwamba ukoloni wa Kiingereza ulikuwa unakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalopaswa kutatuliwa na hatimaye wakaonyesha njia ya kulitatua kupitia Tangazo la Uhuru wa Marekani (The Declaration of Independence (1776), tamko ambalo lilisisitiza "uhai, uhuru na furaha" kama haki za msingi kwa kila binadamu.
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha waasisi wa Jamhuri ya Kikatiba ya Ufaransa kuona kwamba utawala wa kifalme ulikuwa unakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalopaswa kutatuliwa na hatimaye wakaonyesha njia ya kulitatua kupitia Matamko ya Haki za Raia wa Ufaransa na Binadamu Wote (Declaration of the Rights of Man and of the Citizen (1789/1793), matamko ambayo yanasisitiza "udugu, uhuru na mali" kama haki za msingi kwa kila binadamu.
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha Karl Marx wa Ujerumani na mwenzake Friedrich Angels wa Urusi kuona kuwa mahusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa wakati wa enzi za Mapinduzi ya Viwanda yalikuwa yanakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalohitaji kutatuliwa hatimaye walionyesha njia ya kulitatua tatizo hili kupitia kijitabu chao kiitwacho "Ilani ya Ukombozi kwa Mtazamo wa Kikomunisti" (The Communist Manifesto (1848)).
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha viongozi mbalimbali wa mataifa ya ulimwengu kuona kwamba vita kuu ya kwanza na vita kuu ya pili ya dunia ilikuwa ni mifano tosha kuonyesha kuwa utemi wa kijeshi unakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalopaswa kutatuliwa na hatimaye kuonyesha njia ya kulitatua kupitia kitabu chake kiitwacho "Sisi ni Watumwa Ndani ya Nchi Yetu" (The Universal Declaration of Human Rights (1948)).
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizomwezesha Frantz Fanon wa Algeria kuona kwamba ukoloni nchini mwake ulikuwa unakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalopaswa kutatuliwa na hatimaye kuonyesha njia ya kulitatua kupitia kitabu chake kiitwacho "Sisi ni Watumwa Ndani ya Nchi Yetu" (The Wretched of the Earth (1961)) ambapo anasisitiza haki ya taifa kujitawala katika nyanja zote za maisha.
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha wajumbe wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano kuona kwamba baadhi ya mapokeo ya Kikatoliki yalikuwa yanakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalopaswa kutatuliwa na hatimaye kuonyesha njia ya kulitatua kupitia "Katiba ya Kanisa Katoliki Kuhusu Jukumu la Kukuza na Kuhami Haki za Binadamu" (Gaudium et Spes 1965)).
Haki zote za Binadamu kama zinavyopatikana katika Tangazo la Dunia Kuhusu Haki za Binadamu zimeingizwa katika katiba hii.
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizomwezesha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuona kwamba kasumba za kikoloni nchini mwetu zilikuwa zinakiuka utu wa binadamu, na hivyo tatizo linalopaswa kutatuliwa na hatimaye kuonyesha njia ya kulitatua kupitia "Azimio la Arusha" (The Arusha Declaration 1967), azimio linalotaja vipaumbele vya kitaifa kuwa ni mapambano dhidi ya umaskini, ugonjwa, ujinga na maradhi.
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizomwezesha Paul Freire wa Brazil kuona kwamba mfumo wa elimu unaomfanya mwanafunzi aenende kama roboti (banking system of education) ni kiini cha udumavu wa kimawazo ulio na madhara makubwa sana kwa uhai wa taifa la kesho, na hatimaye akaonyesha njia ya kulitatua kupitia kitabu chake kiitwacho "Pedagogi ya Ukombozi" (Pedagogy of the Oppressed 1969)), uamuzi ambao ulimfanya aitwe, sio mkandamizaji, bali mkombozi.
Aidha, ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizowawezesha Watanzania walioshiriki katika kuandaa Katiba yetu ya mwaka 1977 kuona kwamba kuna haja ya kuzitambua rasmi, kuliko ilivyokuwa hukonyuma, haki za binadamu, na hatimaye kuonyesha njia ya kulitatua kupitia marekebisho yaliyoziingiza haki za binadamu ndani ya katiba hiyo.
Katika katiba yetu kwenye Ibara ya 12 hadi ibara ya 24 zinaorodheshwa haki muhimu za kila Mtanzania kwa mujibu wa Tangazo la Dunia Kuhusu Haki za Binadamu. Tangazo hilo lilikubaliwa na kutiwa saini na Serikali ya Tanzania mara tu baada ya uhuru mwaka 1961.
Ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizomwezesha Enrique Dussel wa Argentina kuona kwamba baadhi ya mawazo yanayopenyezwa katika ulimwengu wa tatu kutoka katika ulimwengu wa kwanza ni kutu ya kimawazo (ideological contamination) inayopaswa kutatuliwa na hatimaye akaonyesha njia ya kulitatua tatizo hilo kupitia kitabu chake kiitwacho "Falsafa ya Ukombozi" (A Philosophy of Liberation 1985).
Na hatimaye ni jozi za mawazo yanayopigana kisogo zilizoliwezesha vilevile Kanisa Katoliki Tanzania kuona kwamba kuna ukosefu wa "vipaumbele vya kitaifa" nchini, na hatimaye wakaonyesha njia ya kulitatua kupitia vijitabu vitatu vinavyojulikana kama: "Mpango wa Kichungaji Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010", "Ilani (ya) Mapendekezo ya Vipaumbele vya Kitaifa", na "Mada za Kuongoza Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2010".
Kwa ufupi basi, niseme kwamba historia hii pana inaonyesha mambo mawili makubwa. Mosi, inaonyesha ukweli kwamba kukiuka utu wa binadamu (human dignity) ni jambo lisilokubalika sehemu yoyote duniani. Na pili inaonyesha ukweli kwamba njia bora zaidi ya kukuza na kuhami utu wa binadamu tajwa ni kukuza na kuhami haki za binadamu wote bila kujali upekee wao kwa misingi ya vigezo vya kinasibu kama vile dini, jinsia, umri, uzito, urefu, rangi, kabila, au itikadi za kisiasa.
Katika muktadha huu, nimevisoma vijitabu vyote vilivyotolewa na Kanisa Katoliki ili nijiridhishe kwamba wamezingatia mambo haya mawili. Na sasa naweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba haki zote za binadamu zimezingatiwa. Hakuna mahali popote ambapo Kanisa Katoliki limependekeza ama kudumaza au kutelekeza haki yoyote ya binadamu.
Kimsingi, bila kuathiri haki yoyote ya binadamu, Mpango wa Maaskofu Katoliki Tanzania unapendekeza orodha ya haki za binadamu ambazo, kwa maoni yao, zinapaswa kuchukuliwa kama "vipaumbele vya kitaifa".
Kwa hiyo, ninalazimika kuhitimisha makala yangu kwa kusema kwamba Maaskofu Katoliki Tanzania wamechagua fungu lililo bora kwa binadamu wote wa Tanzania.
Anayekataa ukweli huu ama atakuwa anashindwa kutofautisha kati ya hoja na mtoa hoja au atakuwa anakanusha upita-mipaka wa utu wa binadamu (universality of human dignity).
Katika hilo la kwanza, tutalazimika kumpuuza mtu huyo; maana atakuwa amechagua kufanya utovu wa nidhamu ya kitaaluma. Na katika lile la pili, mtu wa aina hiyo atakuwa anatukuza utabaka kwa msingi wa vigezo vya kinasibu (specificity of human persons). Watu wa aina hii watakuwa wanaipinga katiba ya Tanzania na hivyo watu wa kuogopwa kama ukoma!
Mpango huu wa maaskofu ni pedagogi ya ukombozi kwa wote
Simu:
0734 800808