Nilishasema tangu mwanzo hakuna jibu litakaloridhisha na hakuna swali litakaloachwa kuulizwa! Mmemuuliza Zitto kawajibu. Haitoshi. Mmeyaleta ya mama yake haitoshi. Hamuwezi kukubali jibu lolote isipokuwa "ndiyo mimi na Amina tulikuwa na uhusiano wa kimapenzi na ulikuwa mzuri kweli". Akijibu hivyo haina maana itakuwa mwisho maswali yatakuja "kwanini uvunje ndoa ya watu, wewe kama kiongozi.. tukuamini vipi na wake zetu? vipi mabinti zetu na dada zetu, unawezaje kukaa Bungeni ilhali hivi na vile".
Kila mtu ana haki ya kuuliza lolote lile kwa mtu yeyote yule, lakini huwezi kumlazimisha mtu kujibu kama hataki. Haki ya uhuru wa kusema, inahusisha na uhuru wa kutotaka kusema! Ndio maana wenzetu wamarekani wanayo mabadiliko ya tano ya katiba!
Inapohusu mambo ya umma na yanayohusu maslahi ya TAifa kila kiongozi analazimika kutoa habari sahihi kwa wananchi. Hata hivyo hatuwezi kumlazimisha kiongozi kwa suala ambalo si la kisheria kutueleza habari za maisha yake binafsi? Hivi Malecela ana watoto wangapi? Je Kikwete amewahi kulala na wanawake wangapi? Mbona hatujawahi kumuona mke wa Lipumba? Vipi kuhusu Mrema na mke wake? Vipi kuhusu Freeman na mahusiano yake na kina dada? etc etc etc...
Mnaosema double standard, you have no idea what your setting up! Kama tunakubali (na ninaamini ndiyo hoja yenu) kuwa masuala ya chumbani na malezi ya familia za viongozi yanaweza kuchambuliwa hadharani. Basi tufungue mjadala huo na tusiishie kwa Zitto na viongozi wa Chadema tu, au viongozi wengine wa upinzani. Tuwazungumze wote kwa uhuru na uwazi.
Ninachosema na ninapenda kueleweka ni kuwa kama Zitto alikuwa anatuhumiwa kujihusisha na biashara fulani haramu, hilo linazungumzika; kama anatuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mfanyakazi wake hilo linajadilika; kama Zitto angekuwa anatuhumiwa kuingiza jimbo lake kwenye mkataba wa ajabu ajabu hilo linazungumzika. Ni kutokana na mawazo hayo ndio maana tunauwezo na kila sababu ya kuhoji utendaji kazi wa viongozi wa serikali yetu, nia na matumizi yao.
Kuamua kutong'ang'ani kutaka kujua mambo ya undani ya chumbani ya mheshimiwa Zitto kwa vile tu yeye ni Mwakilishi wetu siyo unafiki! Sijawahi mahala popote kutaka kujua mambo ya chumbani ya Malecela, Kikwete, Kawawa, Lowassa, Nchimbi n.k SIyo kwa sababu hakuna madai dhidi yao au kwamba watu hawajui, ni kwa sababu tu kwamba jambo hilo linafungua sanduku ambalo hatuko tayari kulifungua. Mnapotetea kulazimisha Zitto awape undani wa kile "kilichotokea" hata kama keshakanusha hamtaki ukweli, bali mnataka ukweli kama ulivyoandikwa na nyinyi! Nilionya huko nyuma kuwa wanaotaka Zitto aseme hawawezi kuridhika hadi akiri kuwa na mahusiano ya kimapenzi na ni hicho ambayo baadhi ya ndugu zetu hapa wanataka. Chochote chini ya hapo, hakitakubalika.
Ninawaomba na tena nina wasihi kutoka ndani ya moyo wangu, msifungue sanduku hili la kujadili mambo ya chumbani ya viongozi au madhaifu ya kibinadamu ya viongozi wetu endapo mambo hayo hayahusiani moja kwa moja na nafasi zao, pesa za walipa kodi au maslahi yoyote yale ya kitaifa. Na msilazimishe kuwa kiongozi akienda msalani basi hilo ni jambo la kitaifa na mnataka details zake, kisa tu alionekana akienda msalani kwa jirani yake! Kipimo ambacho mnataka kukitumia kwa Zitto kikikubalika siyo kwamba kitaonesha umakini wa forum hii bali kutaishusha hadhi yake kuliko tunavyofikiria. Nawahakikishia kama mnafikiri mambo yanayojulikana ni ya Zitto peke yake fikirini tena. Wenye data za viongozi au wanaotaka kujua mambo ya viongozi siyo nyinyi peke yenu! Kuna watu wanajua viongozi wanaposafiri huja na kina nani, wanakaa wapi, na kina nani wanakutana nao. Tukikubali kuwa Zitto LAZIMA azungumze hapa (licha ya kuwa tayari amezungumza) na akiri (licha ya kuwa ameshakanusha) kuwa amefanya kitendo fulani (ambacho tayari amesema hakufanya) basi siyo kwamba tunataka kutenda haki bali kufurahisha tu udadisi wetu wa kibinadamu. Nawasihi tena, kama kweli ninyi mnaitetea forum hii, basi heshimuni mambo ya binafsi ya viongozi na hilo litumiwe kwa viongozi wote.
Hata hivyo endapo mambo yale ya binafsi yanahusiana na nafasi, vyeo, au yanaweza kuwa ni matendo ya kihalifu (criminal acts) basi hilo halina mjadala kwani hakuna mtu yeyote aliyejuu ya bodi au juu ya wanachama. Wote wako chini ya ukweli, ukweli mtupu, na si kingine bali ukweli.
Hata hivyo, sitarajii kuwa mtakubali ushauri huu kwani tayari mmeshanipa chama kuwa miye Chadema na ninamtetea Zitto. Na hii ni mara ya mwisho kuweka jambo hili sawa, mimi SIYO mwanachama wa CHADEMA ila ni mfuasi madhubuti wa mafundisho ya Mwalimu na mpenzi wa classical ideas za CCM. Kwa vile ninaandikia Tanzania Daima basi baadhi ya watu wamedhani mimi ni Chadema. Sasa hivi ninaandikia Kulikoni pia na sijui hilo linaendana na chama gani, na muda si mrefu (inshallah) nitaanza kuandikia magazeti ya serikali.
Mapenzi yangu ya kwanza na ya pekee yako mahali pamoja tu na hapo pekee ndipo ninaposimamia hoja. Napo ni Tanzania na Tanzania peke yake. Hakuna Chama, kiongozi, au mtu yeyote ambaye ni juu ya nchi yetu.
Narudia tena, siyo kwa jazba ya ujana bali kwa hekima ya uzee; TUSIFUNGULIE na TUKATAE kuendeleza mjadala huu wa masuala ya chumbani ya Zitto na Amina. Amina hataki/kazuiwa kusema tusimlazimishe; akitaka kusema ni haki yake na asizuiwe. Zitto ameshasema, tusimlazimishe aseme kitu ambacho hayuko tayari au hana tutakuwa tunafanya cyber bulling ili kutishia watu. Nawasihii tena, chonde chonde. Zitto keshazungumza, tukubali amefanya haki yake, zaidi ya hapo ni kujitafutia umaarufu usio wa lazima kwa mgongo wa kiongozi wa kitaifa! Hakuna cha kumkoma nyani geledi wala nini, ni kukomoana kinyama kwa kupigana mijeledi!
Na hii ni post yangu ya mwisho kwenye suala hili.