Wanawake wapiga hatua muhimu kubadilisha jamii licha ya vikwazo

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
VCG41N960665896.jpg

Na Serah Nyakaru


Juhudi za wanawake kuleta mabadiliko duniani sasa zinaonekana katika kila pembe ya dunia. Nchi zilizostawi na zinazostawi kote duniani zina miradi ambayo inaendeshwa ama ilianzishwa na wanawake tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mfumo dume uliwatenga wanawake.

Hivi sasa wanawake ni wanaharakati wakubwa wa kutetea mazingira, wengine ni viongozi tajika na wengine ni mabalozi wakuu wa upatanishi na amani. Hii ni habari njema, ulimwengu wa kina mama unapiga hatua. Licha ya vikwazo vya kimazingira, kijinsia na hata mifumo kandamizi, wanawake wa bara Afrika wameinuka na kutia fora katika fani mbalimbali. Wapo wale ambao majina yao yameandikwa katika kumbukumbu za ulimwengu kutokana na mchango wao adimu na wakutambulika.

Nchini Kenya kwa mfano kuna marehemu profesa Wangari Maathai ambaye mchango wake katika kupigania mazingira utakumbukwa milele. Ni vita ambayo alipigana na hii leo Afrika nzima inaona matunda yake. Bingwa wa dunia wa mbio za masafa marefu Bi Tegla Lorupe ni mwanamke ambaye mchango wake utaishi kukumbukwa milele sio tu kwa kuishindia Kenya mataji kwenye majukwaa ya kimataifa, bali pia katika kuhakikisha kina mama na watoto wanaishi kwa amani.

Bi Lorupe ambaye anatoka katika jamii za wafugaji ambao hugombea mara kwa mara maji na malisho ameunganisha jamii yake. Kupitia juhudi zake kama mama amewaleta wadogo kwa wakubwa, akawafunza umuhimu wa amani na hata kuanzisha miradi ya kunufaisha jamii yake kama vile miradi ya kilimo. Ulimwenguni kote ameongoza mikutano ya amani baina ya pande hasimu kwenye vita ambavyo wanawake na watoto huathirika zaidi. Kupitia kwa wakfu wake wa Amani wa Tegla Lorupe, kina mama ambao hawakuwa na kisomo sasa wanapata masomo, wanazuru mataifa tofauti ya dunia na kujifunza mengi.

‘’Mimi nilizaliwa sehemu ambayo ilikuwa na vita. Eneo la Pokot ninakotoka vita ilikuwa ikitokea kila siku, na wanawake na kina mama ndio huathirika pakubwa lakini kupitia mikono ya mwanamke-mama yangu mzazi, nilipata nafasi ya kukuza kipaji changu. Leo hii kupitia kipaji changu naongoza amani, kule kwetu kuna amani.’’ alisema balozi Tegla Lorupe.

Kulingana na Lorupe, ukosefu wa elimu ya kutosha na unyanyapaa ni baadhi ya vizingiti vinavyowazuia kina mama kung’aa zaidi. ‘’Tumepiga hatua katika elimu ya mtoto wa kike kama nchi, lakini kuna mengi ambayo bado hatujaafikia. Bado kuna visa vya wanawake kudhulumiwa, wanawake katika baadhi ya jamii hawana sauti. Haya yameturudisha nyuma lakini naamini mambo yatakuwa sawa.’’ Aliongezea Bi. Lorupe

Kilomita 790 kutoka kwa wakfu wa Amani wa Telga Lorupe eneo la West Pokot kwenye Bonde la Ufa nchini Kenya kuna mama anayeendeleza mikakati ya ‘ukombozi wa kisasa.’ Mary Naliaka Wafula mwakilishi wa wadi ya Airport kwenye kaunti ya Mombasa nchini anaendeleza juhudi za kuwarai na kuwashirikisha wanawake katika uongozi. Bi Naliaka anaamini kuwa mwanamke ana nafasi sawa na wenaume, lakini jamii imemdunisha na kumuweka pembeni katika masuala ya utawala.

Kupitia wakfu wa wanawake wa Pwani- Pwani Women Caucus, Bi Naliaka hutoa ushauri na mafunzo kwa wanawake namna ya kugombea nafasi za uongozi akiwa na falsafa kuwa mwanamke ni kiongozi bora zaidi.

Ulimwengu unapoadhimisha Siku ya wanawake duniani, Umoja wa Mataifa unasema kuwa hatua muhimu zimeafikiwa katika kuhusisha wanawake kwenye miradi muhimu ya kijamii ila mifumo ya jadi bado inawazuia baadhi yao kushiriki kikamilifu katika kuboresha jamii hasa kwenye nchi zinazostawi.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake duniani ni Usawa wa kijinsia leo, kwa Kesho endelevu.
 
Back
Top Bottom