Wanawake 21 hufa kila siku wakati wa kujifingua
Katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2012, takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji imeongezeka kutoka asilimia 19 hadi kufikia asilimia 50. Wakati idadi hiyo ikiongezeka, madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake wa Hospitali ya Muhimbili, wanasema kuwa vifo vya wajawazito bado msalaba mkubwa kwa Taifa.
Takwimu za hivi karibuni nchini zinaonyesha kuwa katika kila mwaka Tanzania inapoteza akina mama 7,900 kutokana na sababu zitokanazo na ujauzito. Idadi hiyo ikigawanywa kwa siku 7,900 kwa siku 365 unapata wastani wa vifo 21.64, sawa na vifo 22 kwa siku.
Ofisa Mawasiliano wa Muungano wa Utepe Mweupe kwa uzazi salama (WR), Lydia Kamwaga anasema wakati taarifa nyingi zimeonyesha bado vituo vingi vya afya havitoi huduma za dharura za uzazi kutokana na ukosefu wa vifaa na kutokuwapo chumba cha upasuaji (theatre).
"Serikali ni miongoni mwa zinazoguswa na vifo vya wajawazito na watoto wachanga, ndiyo maana katika mkakati wake wa kupunguza vifo hivyo, mwaka 2008/2015, iliahidi kuwa ifikapo mwaka 2015, asilimia 50 ya vituo vitatoa huduma za uzazi za dharura, hata hivyo utekelezaji wa ahadi hiyo haujafanyika kwa asilimia 100 kama ilivyotarajiwa," anasema Kamwaga na kuongeza:
"Hivyo, sisi kama wadau wakubwa wa afya ya wajawazito na watoto, yaani Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania, tunaikumbusha Serikali kutimiza ahadi hii kwani ina nafasi kubwa sana katika kuokoa maisha ya wajawazito na watoto wachanga."
Wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, wanazungumzia kukosekana huduma za dharura katika vituo vya afya mjini humo na kusema kuwa wanaamini changamoto hiyo pia ni moja ya sababu inayochangia vifo vya wajawazito mjini humo kutokana na kuitegemea pekee Hospitali Rufaa ya Tumbi kupata huduma hizo.
" Kweli vituo vya afya vingi bado havijaanza kutoka huduma za dharura za kujifungua. Desemba mwaka jana, nilifika Kituo cha Afya Kongowe, nikaambiwa niende Tumbi, huko wakaniambia wanapokea wa rufaa tu, nikatakiwa kwenda kituo cha afya mkoani," anasema na kuongeza: "Baada ya kupimwa kwenye kituo hicho cha afya, nilibainika kuwa na uchungu, nikalazimika kupelekwa Tumbi ambako hawafanyi upasuaji," anasema Mwanaidi Rashid.
Naye Mratibu wa afya ya mama na mtoto mjini Kibaha, Dk Allan Sayi anasema pamoja na changamoto ya kutokuwapo huduma za dharura katika vituo vingi vya afya mjini humo, bado jamii haitilii mkazo maelekezo wanayopewa kliniki na hasa suala la kuanza mapema kuhudhuria kliniki pindi mama anapohisi ujamzito au uchungu. Dk Sayi amebainisha kuwa wajawazito huanza kwenda kliniki wakati mimba ikiwa tayari ina miezi zaidi ya minne, na wengine wanashikwa na uchungu lakini hawaendi kliniki mapema, badala yake husubiri hadi hali imekuwa ya uchungu zaidi na kuamua kwenda hospotali. Katika mazingira kama haya, mama anaweza kupoteza maisha, mtoto au wote kwa pamoja.
"Lipo tatizo pia katika jamii yetu, mjamzito anakaa nyumbani mimba ina miezi mitano au sita ndiyo anaanza kliniki, wengine wana utamaduni uliopitwa na wakati, anahisi uchungu wa kujifungua kama sio yeye basi mzazi wake ndiyo amwambie, sasa hawa wote wapo katika kundi hatari.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Dk Isa Kaniki anasema kituo cha Afya Kongowe na mkoani vipo katika mpango wa kuanza kutoa huduma za dharura za uzazi baadaye mwaka huu mipango ipo katika bajeti ya mwaka huu.
Wanawake 21 hufa kila siku wakati wa kujifingua - Kitaifa - mwananchi.co.tz