Wananchi: Kuzimwa kwa intaneti kote nchini wakati wa uchaguzi mkuu kumeathiri vibaya uchumi na maisha

Wananchi: Kuzimwa kwa intaneti kote nchini wakati wa uchaguzi mkuu kumeathiri vibaya uchumi na maisha

Mwizukulu wa Buganda

JF-Expert Member
Joined
Nov 19, 2024
Posts
638
Reaction score
1,771
Kuzimwa kwa intaneti kote nchini Uganda wakati wa uchaguzi mkuu kumeathiri vibaya uchumi na maisha ya wananchi, hususan wafanyabiashara na vijana wanaotegemea huduma za mtandaoni. Biashara za fedha kwa njia ya simu zilisimama, waendeshaji bodaboda waliopata wateja kupitia programu walipoteza kipato, huku wanafunzi na waandishi wa habari wakishindwa kuwasiliana na kufanya kazi zao. Serikali ilisema hatua hiyo ililenga kulinda amani na utulivu wa taifa, lakini upinzani na waangalizi wa uchaguzi wamedai ilidhoofisha upatikanaji wa taarifa, shughuli za kiuchumi na imani ya umma katika mchakato wa uchaguzi.

--
Wakala wa miamala ya kifedha kupitia simu, Mirembe Tracy, anaeleza kuwa shughuli zake za kibiashara katika jiji lenye pilikapilika la Kampala zilisambaratika kabisa kufuatia uamuzi wa serikali kuzima intaneti wakati wa uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita uliokuwa na ushindani mkubwa.

Akizungumza na BBC, anasema huduma zote za kutoa fedha zilikwama, huku akisisitiza kuwa sehemu kubwa ya kipato chake hutokana na kamisheni ya miamala hiyo. Kutokuwepo kwa huduma hizo kulisababisha mapato yake kufikia sifuri.

“Kwa kawaida, ndani ya wiki moja naweza kupata hadi shilingi 450,000 za Uganda. Fedha hizo ndizo hunisaidia kulipia kodi ya nyumba. Kuzikosa kulikuwa hasara kubwa sana,” anasema.

Katika siku mbili kabla na baada ya uchaguzi, hakuwa na shughuli nyingine zaidi ya kukaa nyumbani, akiuza tu vocha za muda wa maongezi, ambazo kwa mujibu wake hazina faida ya kamisheni.

Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda iliamuru kusitishwa kwa intaneti nchi nzima kwa madai ya kulinda amani, usalama wa taifa na kuzuia matumizi mabaya ya majukwaa ya mawasiliano wakati wa zoezi muhimu la kitaifa. Hata hivyo, upinzani ulipinga hatua hiyo, ukidai ililenga kuficha dosari za uchaguzi na kuzuia mawakala wao kutuma matokeo kutoka vituo vya kupigia kura.

Kwa vyovyote vile, kusitishwa kwa intaneti kuliathiri pakubwa mwenendo wa maisha ya kisasa, hasa shughuli za kiuchumi. Biashara nyingi za mtandaoni zilizotegemea miamala ya fedha kwa simu zilisimama, huku zingine zikilazimika kurejea matumizi ya fedha taslimu.

Jiji la Kampala linajulikana kwa usafiri wa bodaboda, ambapo waendesha wengi hupata kipato kupitia programu za kidijitali. Mwanzilishi mwenza wa SafeBoda aliwaeleza waandishi wa habari wa ndani kuwa mifumo ya jukwaa hilo ilizimika kabisa wakati wa kusitishwa kwa intaneti, hali iliyowalazimu waendesha pikipiki wengi kusitisha shughuli zao na kuathiri mapato ya biashara nyingine zinazotegemea huduma hiyo.

Kwa upande wake, Namukwaya Olivia, muuzaji wa mavazi ya asili ya kitamaduni anayetegea sana mitandao ya kijamii kama Instagram, TikTok na WhatsApp, anasema kipindi hicho hakufanikiwa kusafirisha bidhaa zozote. Anaeleza kuwa wateja wake hutegemea picha kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi.

“Hatukuweza kutuma picha wala kupokea oda, na usafirishaji ulisimama kabisa,” anasema, akiongeza kuwa madhara yalionekana mara moja na kufanya iwe vigumu kugharamia mahitaji ya msingi kama kodi ya nyumba. Hata baada ya kurejeshwa kwa intaneti, anasema hali haijaimarika kikamilifu kwani wateja bado wanapata changamoto kuwasiliana nao mtandaoni.

Mwandishi wa habari Ngabo Amon anasema simu yake ya kisasa, ambayo ni nyenzo muhimu ya kazi, ilipoteza maana yake wakati wa kuzimwa kwa intaneti. Hakuweza kufanya utafiti, kufuatilia matukio ya uchaguzi wala kuwasilisha taarifa kwa chumba cha habari.

Kwa mujibu wake, maisha ya kila siku yaligeuka kuwa ya kusubiri kwa wasiwasi kurejeshwa kwa huduma hiyo. Baadhi ya familia zilijikuta zikirejea kutazama televisheni au kununua filamu za zamani ili kujipa shughuli.

Vijana pia walikumbwa na changamoto. Ronnie Mwesigwa, mwenye miaka 20, anasema alikatika kabisa mawasiliano na marafiki na kukosa burudani za mtandaoni, ikiwemo michezo ya kidijitali. Ili kupitisha muda, alilazimika kutazama picha na video zilizokuwa tayari zimehifadhiwa kwenye simu yake.

Ngabo anaeleza kuwa hali hiyo ilikuwa ngumu zaidi kwa waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti uchaguzi, kwani bila intaneti ilikuwa vigumu kuonesha picha kamili ya matukio ya ghasia na mvutano mitaani. Katika maeneo ya vijijini, baadhi ya waandishi walilazimika kusafirisha video na picha kwa usafiri wa kawaida hadi vyumba vya habari, mara nyingi zikiwasili kuchelewa kiasi cha kupoteza umuhimu wake.

Ripoti ya waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika ilibainisha kuwa kuzimwa kwa intaneti kulipunguza upatikanaji wa taarifa, kuathiri uhuru wa kujumuika na kudhoofisha shughuli za kiuchumi, sambamba na kuibua mashaka na kutoaminiana katika mchakato wa uchaguzi.

Mwandishi wa habari kutoka Kenya, Caroline Mutai, aliyekuwepo Uganda kufuatilia uchaguzi, anasema hali hiyo ilimletea msongo mkubwa wa mawazo, akipata ugumu mkubwa kutuma taarifa na kukatika mawasiliano na familia yake wakati wa hali ya wasiwasi wa kiusalama.

Kwa wanafunzi, kusitishwa kwa intaneti kuliathiri masomo na mawasiliano. Aaron Benitez, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho, anasema hakuweza kuwasiliana na familia yake wala kushiriki masomo ya mtandaoni, huku walimu wakishindwa kutuma noti na kazi. Hata baada ya uchaguzi, anasema huduma bado ni ya polepole na isiyotabirika.

Serikali ilirejesha kwa sehemu intaneti baada ya Museveni kutangazwa mshindi, ingawa baadhi ya mitandao ya kijamii iliendelea kuwa na vikwazo, hali iliyowafanya vijana wengi kutumia VPN kuunganishwa. Kwa wengi, tukio hilo halikuwa kero ya muda mfupi tu, bali lilidhihirisha kwa uwazi namna upatikanaji wa teknolojia ya kidijitali ulivyo muhimu katika maisha ya kila siku.

Source: Uganda's internet shutdown: Slashed incomes and gamers go cold turkey
 
Back
Top Bottom