Wafanyabiashara Soko la Tegeta Nyuki walalamikia ubovu wa miundombinu na mazingira machafu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,814
11,991
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Soko la Tegeta Nyuki, Dar es Salaam wamelalamikia ubovu wa miundombinu ya soko hilo hilo kwa kusema asilimia kubwa inachangia huduma kuwa mbovu hasa wakati wa mvua.

Nurdin Abdul, Mfanyabiashara wa sokoni hapo amesema “Changamoto katika soko letu ni matope, mazingira si mazuri kutokana na mvua, wateja hawafiki kutokana na hali ilivyo.

“Tunahitaji viongozi watusaidie kwa kuwa hali hii inatuweka katika mazingira ya kupata maambukizi, kingine kibaya ni kuwa hatuna sehemu ya maegesho, wateja wanakuja lakini wanakosa sehemu za kuweka magari yao.”

Upande wa Abed Kibiriti ambaye naye ni mfanyabiashara sokoni hapo amesema “Hatuna eneo la dampo, lililopo lipo karibu na mtaro, gari ikikosea kidogo tu linaingia kwenye mtaro, hiyo inatishia usalama wa watu na vyombo.

“Kitu kingine ni kuwa mizigo inashuka kwa shida sana kutokana na kukosa sehemu za kuegesha magari.”

Aidha, Deogratius George ambaye ni mmoja wa Wakusanya Ushuru katika Soko la Tegete Nyuki anasema “Nina kama wiki mbili tangu nianze kazi hapa lakini ninachokiona ni kuwa miundombinu si rafiki.

“Barabara hazipitiki, sehemu ya mapaa yameezuliwa, mvua zikinyesha kunakuwa na changamoto kubwa zaidi.

“Tunaomba Serikali itusaidie kurekebisha miundombinu yetu bila hivyo itakuwa ngumu kupata ushirikiano kutoka kwa wafanyabiashara hasa kwa kazi zetu hizi za kukusanya ushuru

“Kuna sehemu hazifikiki kirahisi hata ukienda kumtoza ushuru unaona kabisa hajauza unashindwa jinsi ya kumtoza, hakuna maegesho maalum ya kushushia mizigo.”

Pia soma>> Soko la Tegeta nyuki, kukizuka kipindupindi serikali ipewe lawama zote na iwajibike!
 
Back
Top Bottom