Wadau washauri Vyombo vya habari viwe na Dawati la Jinsia kukabili rushwa ya ngono

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Ili kukabiliana na rushwa ya ngono na mfumo dume katika vyumba vya habari, wadau wa habari wameshauri kwamba kila chombo cha habari kinapaswa kuwa na dawati la jinsia.

Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari kwenye mkutano uliofanyika Desemba 16, 2022, jijini Dar es Salaam.

Akiendesha mada kuhusu wanawake kupewa nafasi walau asilimia 30 kwenye vyombo vya habari, wakili wa kujitegemea, James Marenga alianza kwa kuhoji sababu za wanawake kuwa wachache kwenye tasnia hiyo.

Wadau wameeleza kwamba miongoni mwa sababu kwa wanawake kupata nafasi chache katika vyombo vya habari ni kutojiamini, mfumo dume na rushwa ya ngono.

“Kuna tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari, na hii husababishwa na baadhi ya wanawake kwenye vyombo vya habari kutojiamini lakini pia mfumo dume,” alisema Lilian Timbuka, mhariri wa gazeti la Mwananchi.

Alisema kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vyumba vya habari kutatoa fursa kwa wale watakaofanyiwa matukio kinyume na maadili ya tasnia hiyo kuwa na mahali pa kupata msaada.

Akichangia mada hiyo, mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema miongoni mwa sababu kwa wanawake kuangukia kwenye rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari ni kutokana na ugeni.

“Wapo wanaoangukia kwenye rushwa ya ngono kwa sababu wanawahiwa kwa kuwa ni wageni, ugeni huo unaambatana na woga.

“Nashauri kuwe na utaratibu kwamba wakiwa mwaka wa pili, waweze kuingizwa katika vyombo vya habari mara kwa mara walau wapate uzoefu kabla ya kumaliza masomo yao,” alisema Balile na kuongeza:

“Kwa kufanya hivyo, wataweza kujenga mazingira ya kuzoea tabia za vyumba vya habari na hapo baadaye, hawatakuwa na ugeni ambapo na woga pia utapungua.”
Akizungumzia asilimia 30 wanawake kwenye vyumba vya habari, Balile alisema kuwepo kwa sheria hiyo ambayo imependekezwa katika vikao vya maoni ya wadau wa habari na serikali, kutasaidia kumlazimisha mwajiri kuajiri wanawake.

“Walau kukiwa na sheria hii, itamlazimisha mwajiri kuajiri wanawake kwenye vyombo vyetu vya habari hata kama hataki, na kama hatofikia asilimia 30 lakini walau atafika asilimia 25,” alisema Balile

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom