Rushwa ya ngono ilivyotamalaki Stendi ya Magufuli

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Dar es Salaam. Imeelezwa rushwa ya ngono katika mchakato wa upatikanaji kazi kwa wafanyakazi wa usafirishaji (mabasi) na kwa abiria waliokosa fedha za kujikimu katika kituo cha mabasi cha Magufuli ni miongoni mwa jinamizi linalotafuna katika stendi hiyo iliyopo Mbezi, jijini Dar es Salaam.

Kilichoonekana, wanaume wenye mamlaka katika vyombo vya usafirishaji abiria ambao ni mawakala, makondakta na mameneja wanatumia nafasi yao kupata rushwa hiyo kutoka kwa waombaji pamoja na abiria waliotelekezwa au kukosa nauli katika kituo hicho.

Hali hiyo inatokea ikiwa ni kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, inayoeleza kuwa ni kosa kwa mtu mwenye mamlaka kudai au kuomba rushwa ya ngono kwa mtu yeyote kama sharti la kutoa ajira, upendeleo, kumpandisha cheo, kumpatia haki au huduma maalumu.

Kupitia utafiti wa awali uliofanywa na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Mikoani (UWAM), uliohusu haki za wanawake na watoto, umebaini mbali ya rushwa ya ngono pia lipo suala la utelekezwaji wa watoto kituoni hapo pamoja na namna haki za kundi hilo zinavyotekelezwa.

Utafiti huo ambao ni mradi uliotekelezwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Women Fund Tanzania Trust unaoitwa Haki za Wanawake na Watoto katika Sekta ya Usafirishaji Abiria, uligusia maeneo muhimu kwa kuwahoji wadau wa usafirishaji wa abiria mikoani pamoja na wafanyakazi katika kituo hicho kikuu.

Uongozi wa UWAM ukiongozwa na Mwenyekiti Peter Ndengerio ambaye pia ni Mratibu wa Mradi huo, ulisema walifanya utafiti kwa wanawake 376 kituoni hapo kwa kukusanya takwimu kupitia uchunguzi wa moja kwa moja, mahojiano ya ana kwa ana katika makundi pamoja na dodoso.

“Asilimia 100 ya waliohojiwa walieleza kuwa mchakato wa utafutaji na upatikanaji wa kazi katika vyombo vya usafirishaji unagusa rushwa ya ngono. Walienda mbali na kueleza kuwa rushwa ya ngono ni kama usaili wa kupata kazi.

“Pia walieleza kuwa ni vigumu aliyekataa kutoa rushwa ya ngono kupata kazi katika vyombo hivyo vya usafirishaji. Aidha, tatizo la ngono linaendelea kukikumba kituo hiki, hasa kwa abiria wasio na fedha za kujimudu kimaisha,” ulieleza uongozi wa chama hicho.

Mbali na rushwa ya ngono, pia mradi uliangazia haki za wanawake na watoto katika vyombo vya usafiri na uligundua kuwepo kwa miziki na filamu zinazoonyeshwa kupitia runinga za mabasi zisizo na maadili.

“Watu wengine wanasafiri na watoto na wakwe zao, unakuta filamu na miziki inayopigwa hapo hadi unaona aibu. Washiriki wa utafiti huu walieleza miongoni mwa haki za wanawake na watoto wakiwa safarini ni pamoja na miziki na filamu iwe inalinda utu na heshima kwa wanawake na watoto wakiwa safarini,” ulieleza uongozi wa chama hicho.

Vilevile utafiti unaonyesha kuwa kuna kukosekana kwa huduma ya kwanza kwa ajili ya wanawake (wakati wa hedhi) katika mabasi, kusikika sauti za wanaume pekee wakati wa ufanyaji maamuzi safarini.

Vilevile ubaguzi wa ugawaji vinywaji pamoja na vitafunwa kwa watoto, uwepo wa lugha zisizofaa zinazotolewa na makondakta wa mabasi kwa wanawake na watoto.

Wadau watema nyongo
Wakizungumza kwenye kikao cha uwasilishaji taarifa kilichofanyika mwishoni mwa wiki kituoni hapo, wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji pamoja na haki za wanawake waliweza kuzungumzia hali halisi sambamba na maoni yao juu ya nini kifanyike.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala na Makarani wa Mabasi Dar es Salaam (CMMD), Ephraim Mwambela, mbali ya kukiri uwepo wa rushwa ya ngono pia alisema ni wakati sahihi wa kuweka kanuni na taratibu kuweza kukomesha tabia hiyo.

“Kina dada wanadhalilika, hata mimi nakiri uwepo wa tatizo hili lakini cha kufanya iwekwe namna ya kuwafikia muombaji na mtoaji rushwa hiyo, tuweze kumaliza tatizo,” alisema Mwambela.

Pia, alisema Mamlaka zinazotoa leseni kwa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji zinapaswa kuweka kanuni za kutopiga miziki na filamu zisizo na maadili safarini.

Mwenyekiti wa wajasiriamali wa kwenye kituo hicho, Yusuph Rule alisema elimu lazima itolewe kwa wenye tabia hiyo.

“Kwa asili ya wanaume wa Kitanzania, mwanamke akimuendea ili amsaidie lazima na yeye atataka afaidike, kwa hiyo ili kuzuia hili lazima itolewe elimu kuanzia ya mtu binafsi kujielewa,” alisema Rule.

Akizungumzia namna ya kumaliza changamoto hiyo, alisema mfumo wa ulinzi kituoni hapo uanze kufuatilia wanaume wanaokaa na wanawake na wasichana kwa muda mrefu ambao wengi wao wanarubuniwa kwa kukosa pesa kwa ajili kulinda kundi hilo.

Salome Mande, ambaye ni Karani wa Kampuni ya Mabasi ya Al Saedy alisema rushwa ya ngono haijawaacha wanawake salama wanaoomba kazi katika kituo hicho kutokana na kuombwa rushwa na baadhi ya wamiliki wa mabasi, mameneja, mawakala na makarani wa kiume.

TGNP wajitosa
Mwenyekiti wa bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali, alisema kinachotakiwa kufanywa ni kutoa elimu ya uraia kwa wahusika.

Alisema hata miundombinu ya kituo hicho inapaswa kuwekewa ujumbe kila mahali unaoonyesha kupinga rushwa ya ngono pamoja na kuweka mazingira yatakayopunguza mwingiliano wa abiria na wafanyakazi wa hapo.

“Tuweke mkakati ambao utafanya kila basi linapaswa liwe na mkakati wa kutoa elimu ya uraia na si kuweka filamu na miziki isiyo na maadili,” alisema.

Uongozi wanena
Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Maendeleo ya Jamii kituoni hapo, Milika Ngoyi alisema changamoto za kutelekezwa kwa abiria zipo kituoni hapo, jambo ambalo ni chanzo cha kuombwa rushwa ya ngono. “Kazi yetu ni kuhakikisha watu waliotelekezwa stendi tunawaweka eneo salama kisha tunawasaidia kuwaunganisha na maofisa ustawi wa eneo wanaloenda,” alisema.

Meneja wa kituo hicho, Issihaka Waziri alisema kinamama wa kituo hicho ndio watu wa kwanza kuweza kutatua kadhia hiyo. Alisema wanawake waliopo Magufuli wanayo nafasi muhimu katika kushughulikia changamoto za kijinsia zinazoendelea.

Aliitaka jamii iliyopo Magufuli ijitambue na wanawake watekeleze wajibu wao katika kupinga ukatili wa kijinsia.
Waziri alikiri uwepo wa changamoto zilizowasilishwa na UWAM kwenye ofisi zake mkabala na Kituo cha Magufuli.

“Matukio yote ya ukiukwaji wa haki za kijinsia yaripotiwe katika mamlaka zinazohusika kituoni hapa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika,” alisema Waziri.

Pia, ametoa mwaliko kwa UWAM kuyafikia makundi yaliyopo Magufuli Bus Terminal ili kuyapa elimu ya haki za kijinsia itakayosaidia kukomeshwa kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kituoni.

Mwananchi
 
Back
Top Bottom