Kamati ya wataalamu wa masuala ya habari Zanzibar yaongeza kasi ufuatiliaji marekebisho sheria za habari

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
161
99
Kamati ya wataalamu wa masuala ya habari Zanzibar (ZAMECO) imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kufuatilia mchakato wa marekebisho ya sheria za habari ikiwemo sheria ya Utangazaji No. 7 ya 1997, ambayo ilifanyiwa marekebisho na sheria No. 1 ya 2010.

Katika vikao mbalimbali ZAMECO ilitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ya sheria hio kwa lengo la kupatikana sharia mpya na rafiki kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.

Aidha mnamo tarehe 9/4/2024 ZAMECO wamefika katika afisi za Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar iliyopo Vuga kwa ajili ya kufuatilia hatua iliyofikiwa baada ya kupokea mapendekezo hayo mwezi wa Octoba mwaka 2023.

Mratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa upande wa Zanzibar Shifaa Said ameeleza kuwa hatua hii ya ufuatiliaji imechukuliwa ili kuhakikisha kwamba mchakato wa kupata rasimu ya sharia ya Utangazaji unakwenda vizuri na hatimae sheria mpya itayokidhi vigezo vya kihabari ipatikane.

Kwa upande wake, Salim Said, mwandishi wa habari mkongwe amesisitiza kwamba vyombo vya habari havina nia mbaya na serikali, bali ni washirika muhimu katika kuleta maendeleo kwa jamii hivyo jitihada za ZAMECO na wengine katika kuendeleza maboresho ya sheria ya Utangazaji zinachukuliwa kama sehemu ya ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya habari na serikali.

“Vyombo vya habari havina uadui na Serikali, sisi ni washirika wazuri na wenye lengo jema kwa jamii na nchi kwa ujumla, kwa kuzingatia vyombo vya habari ni nguzo ya maendeleo ya uchumi” Alisema Salim Said

Katibu Tume ya Kurekebisha Sheria ndugu Mussa Kombo Bakari aliwapongeza ZAMECO kwa jitihada wanazozichukuwa kutafuta maendeleo ya tasnia ya habari na kubainisha kuwa mapendekezo waliyowasilisha yamepokelewa na kufanyiwa kazi.

“Tume imekwisha yapeleka mapendekezo hayo katika mamlaka husika na tunatumaini kwamba mapendekezo hayo yatachukuliwa kwa uzito unaostahili ili hatimaye rasimu ya mswaada wa sheria hio ipatikane , alieleza Katibu Mussa.

Mwisho, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) ametoa shukrani kwa katibu na wafanyakazi wote wa Tume kwa ushirikiano wao katika mchakato huu wa kupata sheria mpya huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano huu katika kuhakikisha upatikanaji wa sheria mpya kwa maslahi ya Zanzibar na wazanzibari wote.

Ni takribani miaka 20 sasa wadau wa maswala ya habari Zanzibar wamekua wakipambania marekebisho ya sheria mbalimbali za habari ikiwemo Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu No. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria No. 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Utangazaji No. 7 ya 1997 ambayo ilifanyiwa marekebisho na Sheria No. 1 ya 2010 , ambapo Oktoba mwaka jana Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar ilipokea mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya uatangazaji lengo ni kupata sheria huru iliyokua rafiki kwa tasnia ya habari na jamii kwa ujumla.​
 
Back
Top Bottom