Wiki ya Haki za Binadamu: TAMWA-ZNZ watoa Wito wa Upatikanaji wa Habari na taarifa

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
Ikiwa dunia inahitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kumalizia na maadhimisho ya haki za binadamu, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinaiomba Serikali, asasi za kiraia na wadau wote kuimarisha uhuru wa habari na kufikiwa kwa taarifa.

Siku ya haki za binadamu ambayo ujumbe wa mwaka huu ni "Uhuru, Usawa na Haki kwa Wote" ambao unatoa nafasi tena kwa mataifa kujipima kiwango chake cha kutekeleza uhuru huo na hivyo kuweka mikakati kwa mwakani ili kuimarisha zaidi.

Hivyo, pamoja na mambo mengine uhuru wa habari una umuhimu wa pekee ambao ndio utaifanya jamii kuelewa masuala mbali mbali yanayoikabili jamii na kushiriki kikamilifu katika kuleta suluhisho.

Kwa muda mrefu sasa, waandishi wa habari wamekuwa wakihimiza mabadiliko ya sheria za habari ambazo zimepitwa na wakati hasa Sheria ya Magazeti Na. 5, 1988 iliyofanyiwa marekebisho 1997 na sheria ya Utangazaji Na 7, 1997 iliyofanyiwa marekebisho 2010.

Sheria hizo zikifanyiwa marekebisho vizuri ikiwemo ya kuwalinda waandishi wa habari, kuheshimu uhuru wa uhariri, kurahisisha usajili, kuweka bodi inayojitegemea, kuondosha maneno ya ujumla kama “maslahi ya taifa” na kuruhusu Mahakama kuwa ndiyo muamuzi wa mwisho wa makosa, zitaweza kuwa ni kichocheo kikubwa cha mijadala na maendeleo makubwa ya nchi kiuchumi na kidemokrasia.

Hali hiyo itakwenda sambamba pia na ukuwaji wa elimu na teknolojia nchini ambapo sasa vijana wengi wanasomea masuala ya habari na pia kutumia teknolojia ya habari kupitia vyombo vya habari vya kawaida na mitandao ya kijamii.

Wajibu wa kulinda na kuheshimu haki za binadamu ni wa kila kundi ikiwemo jamii, serikali, vyombo vya habari na taasisi hivyo ni vyema kuweka sheria imara zitakazohakikisha kuwa haki hizo zinalindwa kila sehemu.

Haki za binadamu zinahusisha pamoja na haki ya kuishi, uhuru wa kujieleza, uhuru wa dini, haki ya kupata elimu, na haki ya kuwa na maisha bora na yenye hadhi na kinga dhidi ya ubaguzi na unyanyasaji.

Tamko la Haki za Binadamu lilitangazwa rasmi mwaka 1948 mjini Paris, Ufaransa kwa lengo la kulinda na kuheshimu haki za msingi za kila mtu ikiwemo haki ya kujieleza.

Tarehe 10 Disemba 1948, Umoja wa Mataifa (UN) ulitangaza Azimio la Haki za Binadamu ambalo nchi zote zinapaswa kuzifata ili kuharakisha haki za kila binadamu katika nchi.

Dkt. Mzuri Issa
Mkurugenzi
TAMWA ZNZ
IMG_20231217_145200_217.jpg
 
Back
Top Bottom