Vita kali kati ya Wamasai na Wachaga, 1820,s

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
7,231
12,733
Kabla hawajafika Wamasai katika nchi yetu, walikuwa wakikaa upande wa Afrika ya Mashariki unaoitwa sasa Kenya kwa miaka mingi, wakahama taratibu wakiingia nchi hii kutafuta malisho kwa wanyama wao. Katika mwendo wao wa kuhama waliingia nchi za tambarare zilizo chini ya mlima Kilimanjaro kwa upande wa kaskazini, na wakati ule hawakuwa wengi, maana mtawala wa Wachaga jina lake Rongoma aliweza kuwazuia wasienee sana. Imesemwa ya kuwa wale waliowahi kuingia nchi yake iliyo kati kati ya Kilimanjaro na Upare, walijiweka chini yake na yeye akawa mtawala wao. Wakati huo tunaosimulia sasa labda ulikuwa mwaka 1820, maana tunazo habari za Wachaga za tangu vizazi vingi vinavyotangulia wakati huo, lakini Wamasai hawatajwi mpaka wakati huo aliotawala Rongoma.

Kama tulivyosema, Wamasai walitaka kuingia zile nchi za tambarare zilizo chini ya mlima Kilimanjaro, na kwa hivi walikuwa hawana budi wapite upande huu au upande huu, ndipo waweze kuziingilia. Lakini Wachaga walikuwa wamekwisha weka imara utawala wao, na Wamasai wangalitaka kushika nchi yao wangalikuwa na kazi ngumu sana kuwashinda. Lakini Wamasai walikuwa hawana nia ya kushika nchi za mlimani, walitaka malisho yaliyo chini ya mlima tu, na hayo ndiyo yaliyoleta ugomvi kati ya Wamasai na wenyeji.

Mtawala mmoja mwenye nguvu jina lake Horombo alikuwa amejiweka juu ya nchi za watawala wadogo wote wa Wachaga wa upande wa kaskazini na upande wa mashariki, naye alikuwa na makundi makubwa ya ng'ombe, kwa hivi alitaka malisho akadai kuwa nchi za tambarare zote ni zake. Basi kila walipokuja Wamasai aliwafukuza na kuwanyang'anya ng'ombe zao. Wamasai hawakuweza kuvumulia hivi, wakaenda kwao wakakusanya kabila lao lote, likafanyika jeshi moja kubwa mno, likaja likakusanyika karibu na Kibong'oto kwa upande wa magharibi mwa Kilimanjaro. Horombo alijifanya tayari kwa vita akafanya hila. Aligawanya jeshi lake, na nusu alipeleka upande wa kusini mwa mashariki ili kuwavuta Wamasai wapiganie huko, na huku nyuma yeye mwenyewe aliwashambulia pamoja na askari zake waliobaki akitokea upande mwingine wa mlima. Lakini hakuwa na bahati, maana mwanawe aliyekuwa akiongoza jeshi lile la kwanza alifanya ujinga, akajaribu kuwashambulia Wamasai kabla ya wakati uliowekwa, na kwa hivi yeye na watu wake wote waliangamizwa kabisa. Basi hapo Wamasai walikuwa hawana wa kuwazuia, wakamwendea Horombo katika nchi yake yeye, naye alikuwa hana budi apigane nao pamoja na jeshi lake lililopungua sana. Horombo na watu wake walikuwa hodari wakapigana vita kali sana kwa muda wa siku tatu. Watu wengi sana wakafa katika vita hii na imehadithiwa ya kuwa harufu za maiti zilikuwa mbaya mno hata hazikuvumilika, ikawa kila usiku majeshi yote mawili hayana budi kuondoka mahali walipopigania kwa sababu ya uvundo.

Horombo na watu wake waliwazuia Wamasai barabara wakawa karibu kuwashinda na kuwarudisha nyuma, lakini msiba uliwapata Wachaga. Yasemwa Horombo alikuwa mtu mkubwa sana na kwa hivi adui zake waliweza kumwona vizuri na kumpiga shabaha. Basi mara ilipoanza vita alipata kupigwa na rungu, na mkono wake uliumia sana na kwa hivi hakuweza kushika ngao yake. Jioni ya siku ya tatu alipigwa mshale wa mbavu akaanguka, na mara pale pale watu wake walishikwa na hofu wakatawanyika. Lakini usiku ulikuwa unaingia na vita ilitulia, na Wamasai ambao wamepigwa sana hawakuweza kustahimili zaidi wakarudi nyuma. Basi kwa vile ambavyo Wachaga wametawanyika, na Wamasai wamerudi nyuma, ikawa hapana aliyeshinda wala hapana aliyeshindwa. Lakini tangu siku hiyo mlima wa Kilimanjaro haukuweza tena kuwazuia Wamasai, wakapita mpaka sehemu za chini yake na kuingia nchi za tambarare kukaa. Yasemwa kuwa vita hii ilitokea kati ya miaka 1820 na 1825.
 
Najiuliza: nini hasa madhumuni ya uzi huu? Ni kuchochea uhasama kati ya Wamasai na Wachaga ili kila mmoja aseme yeye ndiye mwenye haki ya kuishi hapo? Nini hasa madhumuni ya kukumbushia historia ambayo imeisha tulizwa na haileti tatizo lo lote hivi sasa? kama lingekuwepo tatizo, ndipo tungesema turudi nyuma kwenye historia wakati tunatafuta ufumbuzi wa tatizo lililopo.
 
Najiuliza: nini hasa madhumuni ya uzi huu? Ni kuchochea uhasama kati ya Wamasai na Wachaga ili kila mmoja aseme yeye ndiye mwenye haki ya kuishi hapo? Nini hasa madhumuni ya kukumbushia historia ambayo imeisha tulizwa na haileti tatizo lo lote hivi sasa? kama lingekuwepo tatizo, ndipo tungesema turudi nyuma kwenye historia wakati tunatafuta ufumbuzi wa tatizo lililopo.
Tukisoma historia ya vita ya Mkwawa na Wajerumani lengo huwa ni kitu gani?
 
Back
Top Bottom