VIPEPEO WEUSI: MKAKATI NAMBA 0034
EPISODE 9
Baada ya RCO Sweya kuingia na yule mama wa kiarabu na kuwaamuru maaskari waliomo mule ndani kwamba "anataka zoezi lifanyike haraka apeleke taarifa kwa RPC", nikaona wale maaskari wamesogea mbele kidogo kuelekea mahali sisi mahabusu tulipokuwa tunesimama.
Tulikuwa tumepangwa mistari miwili.. Kila mstari ulikuwa na mahabusu kumi. Mimi nilipangwa mstari wa nyuma na mbele yetu kama hatua mbili kwenda mbele walipangwa mahabusu wengine kumi tuliokuja nao.
Kilichokuwa kinanikera zaidi rohoni ni kwamba kila nikiwatazama wenzangu, nao walikuwa wanahofu kama mimi lakini nyuso zao zilikuwa zinaonyesha kuwa wanafahamu nini kinachoendelea. Nilitamani nimnong'oneze mahabusu wa pembeni yangu nimuulize lakini nikakumbuka onyo la Godi, "Usiongee"..
Nikajikaza kiume na kushusha presha yangu, walau kwa nje nionekane niko kawaida ingawa ndani nilikuwa na hofu karibu nipoteze fahamu.
Mara yule mama wa kiarabu akiwa ameongozana na RCO wakaanza kutembea kuanzia mstari wa mbele. Alipokuwa anapita alikuwa anamuangalia kila mahabusu kuanzia juu usoni mpaka chini miguuni.
Akafanya hivyo kwa mstari wote wa mbele yetu na kisha akaanza kukagua kwa namna ile ile kwa mahabusu wa mstari wetu.
Akakagua kila mahabusu lakini alipofika mbele yangu akatumia muda mwingi zaidi. Sikujua kama alikuwa ananiangalia mimi au mahabusu wa pembeni yangu, nahisi ni kutokana na hofu niliyokuwa nayo ilinifanya nisifikiri sawa sawa.
Yule mama wa kiarabu akatumia muda mrefu zaidi mpaka RCO nikaona naye anakuwa makini zaidi kwa kusogea karibu na sisi na kutuangalia kwa makini zaidi. Nikabaki nimemtumbulia macho yule mama huku nimejikaza kweli kweli nionekane niko kawaida.
"Huyu hapa!"
Akaongea yule mama wa kiarabu na kugeuka kumuangalia RCO. Kwa mbali nikaanza kusikia mkojo unanibana. Nikaanza kutamani niropoke kwa nguvu kuwa niko hapa katika mission yenye maslahi kwa usalama wa taifa. Ingawa ukweli ni kwa maslahi yangu, na cheupe na baba yake.
"Una hakika ni yeye?" RCO akamuuliza.
"Yes ni yeye" yule mama wa kiarabu akamuhakikishia RCO Sweya huku ananyoosha mkono kumgusa huyo anayemsema. Akamgusa lakini nikashtuka hakunigusa mimi kama nilivyokuwa nahisi. Nikageuza shingo kuangalia ni nani aliyekaa pembeni yangu.
Ni majuto!
Nikamuona Majuto anatoa tabasamu la hasira anashindwa aseme nini?
Mara maaskari wawili wakasogea alipo majuto na wakamshika msobe msobe na kumuondoa ndani ya kile chumba.
Kimya kimya RCO Sweya na yule mama wa kiarabu nao wakatoka kwenye chumba. Tukabaki sisi mahabusu, yule askari mbavu aliyevaa kiraia na maaskari wengine watatu.
"Haya twendeni" akaongea kitemi yule askari Mbavu aliyevaa kiraia.
Wakatuongoza moja kwa moja kuturudisha mahabusu. Lakini kitu cha ajabu tulipofika kwenye korido ya kuingilia kwenye selo zetu mahabusu wengine wakawa wanashangilia au sijui niseme wanapiga kelele..
"Manchester, manchesteeeerrr, manchesterrrr"
Wanapiga kelele huku wanacheka kweli kweli mpaka wakawa wanaudhi. Nikaanza kumuona yule askari anaanza kuchukia. Akageuka kwenye selo inayotazamana na selo yetu namba mbili. Hii ilikuwa ni selo namba moja. Akageuka kwa hasira kweli kweli.
"Weweeee Mbelwa acha useng*, kum* wewe! Usijifanye umezoea sana humu fala wewe, humu hakuzoeleki boya wewe" akamfokea mahabusu mmoja ambaye alikuwa anapayuka sana "manchester" kipindi tunaingia.
"Usimaindi sana Bitozi, usimandi mwanangu! Amani kaka" huyo mahabusu akamjibu yule askari ambaye nikafahamu kuwa wanamuita jina la utani Bitozi.. Alikuwa anamjibu huku anacheka! Nikaelewa huyu lazima amezoea sana humu mahabusu kumekuwa kama Nyumbani kwake.
Bitozi akafungua milango ya selo kwa hasira tukaingia kisha akaifunga tena kwa hasira na kuondoka.
Tukaingia ndani ya selo na kuketi. Godi nilimuona ule uchangamfu wake umepotea kabisa amejiinamia kuna kitu anawaza.
"Nani wamemsukumia fuko la mavi?" Mahabusu yule sharobaro anayeitwa Raphel akamuuliza.
"Majuto!" Godi akajibu kwa kifupi tu.
Nikaona wote wamekaa kimya.
"Godi, sijaelewa kilichotokea?" Nikamuuliza kwa shauku. Mahabusu wenzangu wote walionekana wanajua nini kimetokea na nini kinaendelea. Nachukia sana kuwa gizani wakati wenzangu wote wanafahamu nini kinaendelea.
"Oya kwani hujasikia watu wanavyopiga kelele 'manchester'".
Godi akanijibu kwa hasira.
"Nimesikia ila sijaelewa" nikamjibu na mimi huku nimekereka.
"Gwaride la utambuzi" akadakia yule mahabusu mtu mzima wa makamo anayeitwa Luambano.
"Nini?" Nikamuuliza huku nikigeuka kutoka kumuangalia Godi na kumuangalia yeye Luambano.
"Huko mlikopelekwa na kile kilichofanyika linaitwa gwaride la utambuzi.! Si unaona vile mlivyopangwa mstari? Kama vile wachezaji mpira wanapiga picha kabla ya mechi kuanza, ndio humu mahabusu tunaita jina la utani manchester" Luambano akanifafanulia na walau kuanza kunitoa gizani. Kwa mbali nilianza kuelewa nini kilichotokea ila nikahitaji uhakika zaidi.
"Ok, lengo lake ni nini hasa hilo gwaride la utambuzi" nikauliza huku kichwani nikiwa na nusu ya jibu la swali nililouliza.
"Chukulia kwa mfano kuna tukio la uhalifu limetokea mtaani na wahaisi labda moja wapo ya watekelezaji wa tukio hilo yuko humu mahabusu kwamba alikamatwa kutokana na kuhusika na tukio hilo au alikamatwa kwenye tukio lingine lakini ni baada ya tukio hilo wanalolilenga kufanyika. Kwahiyo wanachokifanya wanamleta moja ya watu ambaye alikuwepo wakati tukio linafanyika na akikutambua maana yake kwamba unaunganishwa kwenye kesi hiyo ya uhalifu na huo utambuzi wa huyo mtu aliyeletwa unatumika kama ushahidi mahakamani ukishtakiwa kwamba shahidi wa Jamuhuri alikutambua wewe ukiwa katika kundi la watu wengi hiyo maana yake ana uhakika wewe ulihusika kufanya tukio!! Hilo ndio gwaride la Utambuzi"
Luambano akanifafanulia.
"***! Sasa kama huyo shahidi waliyemleta akikosea, akakupointi mtu kumbe haukuwepo" nikaukiza kwa kukereka.
"Ndio inakuwa imekula kwako! Yani ndio usenge wa huku mahabusu, unaweza kuja na kesi ya kuiba simu ukajikuta unasukumiwa fuko la mavi la kesi ya mauaji!" Godi akadakia na kuongea kutoka kwenye mawazo aliyokuwa nayo.
"Yule uliyemuona pale ni mke wa Singa Singa wa masika pale si unamjua?" Godi akaniuliza..
"Yes! Namjua Singa Singa mwenyewe" nikamjibu.
"Sasa kama siku tatu zilizopita limefanyika tukio la ujamabazi nyumbani kwake pale pale masika na Singa singa mwenyewe ameuwawa kwa kupigwa risasi! Kwa hiyo leo mke wake amemtambua Majuto kuwa aliwepo kwenye tukio.. So ukiacha kesi yake Majuto inayomkabili iliyomleta huku tayari pale ameshasukumiwa fuko la mavi la kesi ya robbery na mauaji! Jambo la kujiuliza ni kwamba majuto yupo humu mahabusu karibu mwezi mzima, sasa anawezaje kufanya tukio uraiani siku tatu zilizopita?"
Godi akaongea huku uso wake ukiwa serious tofauti na kawaida.
"Hii mingine inakuwaga ni michongo tu Shahidi wanamtonya mapema mtu atakaye kaa mstari gani na amevaaje ndio ampointi" akaongea luambano kwa sauti ya kulalamika.
"Ndio maana sipendagi kukaa mahabusu, bora ya gerezani aisee" akaongea Godi huku anainuka na kuanza kutembea kikomedi kama kawaida yake. Kwa mbali uchangamfu wake ulikuwa unarudi kadiri tulivyokuwa tunajadili hii mada.
"Ndio maana hupendagi?? Ina maana mwenzetu wewe Nyumbani hapa" nikamuuliza kwa uchokozi.
"Humu lockup nishakaa karibia mara kumi na gerezani nishakaa mara mbili! Mara ya zote mbili nilienda kwasababu ya kushindwa masharti ya dhamana sio kufungwa"
"Duuuh hongera! Vipi kukoje gerezani" nikamuuliza nikishindwa kuficha shauku yangu ya kutaka kujua. Kimoyo moyo nilikuwa natamani sana nipate details za kutosha kwasababu leo kama nitapelekwamahakamani kuna uwezekano mkubwa nitaenda gerezani kwa "kukosa dhamana" kama nilivyokuwa nimepanga na wenzangu cheupe na Issack.
"Mbona unauliza kwa hamu kubwa sana, vipi wanakupeleka ngomeni nini leo?" Godi akaniuliza, nahisi aliona shauku yangu kwenye swali langu.
"Yeah! Leo nitapelekwa mahakamani nadhani na sina wadhamini so naweza kupelekwa 'ngomeni'" nikamjibu na nikasikia mahabusu wengine kwenye selo yetu wakipiga miluzi ya taratibu.
"Duuuh! Wala usijali, nitakuwa mshenga wako.. Nitakutafutia bahasha mzuri mwenye hela tukikutana jela" akanijibu huku anaongea na kutembea kikomedi kama jana. Mahabusu wengine wakaanza kucheka.
Nikatambua kuwa hapa sitopata detail yoyote kuhusu jela! Jehanum inayonisubiri huko nitaikuta huko huko jinsi ilivyo.
Mara nikasikia geti kubwa kule nje kwenye korido linafunguliwa. Ilikuwa tayari karibia saa mbili asubuhi.
"Godfrey Nandonde, Godfrey Nandonde, Godfrey ……" Askari alikuwa ameingia huku anaita jina akipita kila sell kwa nje.
"Nipoooooo" Godi akaitikia kwa sauti huku anaelekea kwenye mlango wa selo.
"Umefika muda wangu wa kwenda kusulubiwa" Godi akaongea huku anageuka kutuangalia alipofika mlangoni.
Baada ya kugeka akainua mikono kufanana na jinsi Picha ya Yesu alivyosulubiwa msalabani. Kisha akalaza shingo yake begani. Watu wakaanza kucheka chini chini wakisubiri kituko anachotaka kukifanya.
"Naondoka naenda jela! Jela ni pazuri, naenda kuwaandalia makao ili nilipo mimi na nyinyi muwepo" akaongea kwa sauti kama ya kwenye filamu ya Yesu.
Watu wakaangua kicheko kikubwa kweli kweli. Aliongea kwa sauti kubwa hivyo mpaka selo nyingine tukawasikia nao wanacheka.
Mara mlango ukafunguliwa na Askari akamchukua na kuondoka naye Kwenda "kusulubiwa" mahakamani.
Kwa kiwango Fulani nilijisikia kumuhurumia kuwa hakuwa na wadhamini na atapelekwa jela kwa kushindwa masharti ya dhamana lakini nakiri kuwa kuna upande mwingine nilifurahi kuwa walau nikifika gerezani nitakuwa na "mwenyeji".
Tukaendelea tena na stori na wale mahabusu wengine. Lakini stori zilikuwa hazinogi kwa kuwa "ze komedi" hayupo.
Nikavumilia hivyo hivyo kumsikiliza Luambano akilalamika kuhusu wanawake mpaka ilipofika majira ya saa nne asubuhi alipofika Sajenti Bidebu yule askari anayesimamia kesi yangu ambaye alinichukua na kwenda ofisini kwake.
Ofisini kwake akachukua makaratasi kadhaa akayashika mkononi tukatoka nje ya Jengo la Polisi makao makuu ya Mkoa wa Morogoro.
Siku hii kwa mara ya kwanza nikajua ni kiasi gani hewa ya uraiani ni tamu. Nilijikuta nafumba macho na kuvuta hewa nyingi ndani na kuitoa. Hakika huwa vitu vingi tunavichukua "for granted" kwa kuwa tu tumevizoea. Nimekaa lockup kama masaa ishirini na nne pekee lakini nilijikuta nimepamiss uraiani kuliko nilivyokuwa nafikiri nilivyokuwa ndani mahabusu.
Tukiwa hapa nje ya geti la Jengo la Polisi tukasimama kidogo mwanzoni sikujua anasubiri nini lakini kama dakika mbili baadae nikaelewa.
Kuna askari mwenzake alimuomba akamchukulie pingu.
Alipokuja nazo akanivesha "bangili" na tukanza kuondoka tukitembea kwa mguu.
Uzuri au ubaya ni kwamba, Jengo la Polisi na Mahakama ya Mkoa haviko mbalimbali sana. Ni kama kutoka kituo cha 'Fire' Morogoro Road mpaka Sekondari ya Azania.
Lakini hapo kati kati kulikuwa na maduka na migahawa, kwahiyo kila mtu alikuwa anatukodolea macho jinsi ninavyopelekwa na askari huku nimeveshwa pingu.
Nikajikuta namlaani kimoyo moyo Sajenti Bidebu kwa "kunidhalilisha" namna hii. Lakini mwenyewe alionekana wala hajali wala hana habari. Nikahisi hii itakuwa ni kawaida tu kuwapeleka washatakiwa namna hii. Lakini haijunipunguzia kukereka kwangu na jinsi raia walivyokuwa wananiangalia kwa macho ya tahadhali na kuniogopa. Mpaka mimi mwenyewe nikaanza kujihisi "muhalifu"
Kama dakika saba, tukawa tumefika mahakama ya Mkoa. Nikajishangaa kwa jinsi nilivyo shukuru kimoyo moyo kwa kufika mahakamani. Walau sasa naweza kuepuka kuangaliwa kwa macho ya kuogopwa na "raia wema".
Mahakama ilikuwa imejengwa katika mtindo ambao, ukiingia tu getini mkono wa kushoto kuna Jengo lenye ofisi za mahakimu. Kisha mbele yake kidogo mkono wa kushoto kuna 'Open court' na mkono wa kulia kuna 'open court' nyingine. Na mbele yake kidogo katikati kuna kichumba kidogo cha mraba kama cha mita 2 x 2 chenye madirisha makubwa ila yako juu juu, hiki kilikuwa chumba cha kuwahifadhi washtakiwa kabla ya kupandishwa kizimbani.
Tukaenda moja kwa moja kwenye hicho kichumba nje ambapo kulikuwa na askari watatu wamekaa na mmoja ana bunduki.
"Mshtakiwa mpya huyu muweke tunduni" Sajenti Bidebu akaongea huku anamkabidhi askari mmoja karatasi Fulani na akimaanisha askari huyo aniweke kwenye kile kichumba cha washtakiwa.
"Mahabusu wa magereza naona hawajafika bado, wacha nimpeleke moja kwa moja kwa muheshimiwa nadhani ameshamaliz kusikiliza civil"
Akaongea askari mmoja huku akiinuka. Nikamuelewa kuwa muheshimiwa huyo anayetaka kunipeleka ameshamaliza kusikiliza kesi za madai kwahiyo anaweza kusikiliza yangu wakiwa wanawasubiri mahabusu kutoka magereza.
Sajenti Bidebu akaagana nao na kuondoka. Kisha yule askari akaanza kuniongoza kuelekea kwenye Jengo la ofisi za mahakimu. Kimoyo moyo nikakariri alichokisema Godi, "mda wangu wa 'kusulubiwa' umefika"
Tulipokaribia kuingia kwenye ofisi za mahakimu, nikatupa jicho kwenye geti la kuingilia, nikamuona cheupe na Issack wanaingia. Hii mahakama imezungushiwa ukuta mfupi, kwa hiyo unaweza kabisa kuona nje. Na kule nje nikamuona Baba Bite akiwa na dada mwingine ambaye simfahamu.
Moyo wangu ukapasuka, paaaaaahh!
Nikatupa tena jicho kwa Cheupe na Issack, kisha nikatupa jicho kwa Baba Bite na yule dada ambao tayari nao walikuwa getini wanaingia. Nikajiuliza hawa wamekuja wote au vipi??
Cheupe na Isaack nikagundua kuwa walikuwa wanakwepesha macho na mimi. Hawataki macho yetu yakutane kwahiyo wakawa wanajifanya kama hawajaniona. Baba Bite yeye aliingia getini huku ananiangalia na tukakutanisha macho, kama kawaida yake akatabasamu.
Nikaanza kuchanganua akili nini kitakuwa kinaendelea kwa hawa watu?
Nikakariri tena sentesi ya Godi, "siku yangu ya kusulubiwa imefika"!
Tulipifika nje ya mlango wa Ofisi ya hakimu, yule askari nikamuona amechungulia ndani ya ofisi kidogo na kutoka nje. Dakika moja baadae kuna mama wa makamo akatoka nje mpaka pale mlangoni tulipokuwa tumesimama.
"Nimeleta fresh" yule askari akaongea huku anamkabidhi makaratasi aliyopewa na Sajenti Bidebu yule mama ambaye baadae nilikuja kumfahamu kuwa ni Karani wa hakimu.
Mama akayachukua Yale makaratasi na kurudi tena ndani ya Ofisi.
Tukabaki tumesimama pale koridoni nje ya mlango wa ofisi ya hakimu na askari.
Kama dakika tano baadae yule karani akarudi na kutuita tuingie ndani.
Tukaingia huku askari amenitanguliza na yeye ananifuatia kwa nyuma.
Ndani ya ofisi kulikuwa na meza kubwa kiasi ya kiofisi mbele kabisa na nyuma ya meza hiyo alikuwa ameketi Muheshimiwa Hakimu Gertrude Mwasota. Alikuwa ni "binti" mdogo kuliko ambavyo nilitegemea nilipokuwa naingia humo. Kichwani nilikuwa nimejenga picha nyingine kabisa.
Kwa kumtazama kwa haraka nilimkadiria kuwa alikuwa na umri kati ya miaka 34 hadi 36 na alikuwa ni mrembo haswa.
Alikuwa amevalia miwani ya macho ya fashion ya kisasa.
Juu alikuwa amevaa kikoti maridadi cha suti cheusi ambacho alikivaa juu ya blauzi ya rangi nyeupe.
Nilitamani asimame kidogo nione amevaa sketi ya rangi gani, na nione 'vitu vingine'! Daammnn.. Nikajikuta jicho langu moja kwa moja limetua katika kiganja chake cha mkono wa kushoto! Nikaona pete ya ndoa! "Shiiiiitt"… Nikajisemea kimoyo moyo.!!
'Male instinct' ilikuwa inachukua nafasi yake, kwa kiasi fulani kiduchu nikajikuta nakuwa disappointed. Akili zetu wanaume ni sisi wanaume pekee labda ndio tunazielewa. Haijalishi una mwanamke mzuri kiasi gani na unampenda kiasi gani, lakini bado sehemu fulani ya nafsi yako inatamani kummiliki kila mwanamke mwingine mzuri unayemuona mbele yako. Au hata kama sio kummiliki walau unajisikia faraja ukimuona yuko 'available', lakini sio kuona 'pete ya ndoa'. Haijalishi mme wako au boyfriend wako anakupenda kiasi gani, lakini hata siku moja asikudanganye, hakuna mwanaume anayemuona mwanamke mrembo akiwa na pete ya ndoa na kufurahi.
Muheshimiwa Getrude Mwasota, alikuwa ananiangalia toka naingia mpaka nasimama mbele yao wote waliokuwa ndani ya ile ofisi.
Mbele ya meza ya hakimu kulikuwa na meza nyingine ndefu kiasi ambayo upande wa kushoto alikaa yule mama karani na mkono wa kulia walikaa watu wawili ambao nilikuja kuelewa kuwa ni waendesha mashitaka wa serikali.
Mmoja alikuwa ni mwanaume na mwingine mwanamke. Wote walikuwa vijana, ingawa yule mwanaume alikuwa anaweza kukaribia labda miaka 38 hivi tofauti na yule mwenzake wa kike ambaye nilikadiria hawezi kuwa zaidi ya miaka 34.
Wote walikuwa wamevalia suti nyeusi na shati nyeupe kwa ndani.
Kwa hiyo nilikuwa nimesimamishwa mbele yao wote. Kwa kiasi fulani nilishukuru kwa kuwa kesi yangu itakuwa inaendeshwa huku "chamber court" walau itaniondolea aibu ya kusimamishwa mbele ya kadamnasi ya kusimamishwa kizimbani kama kesi ingelisomwa "open court".
Lakini kilichokuwa kinakera huku chamber court ni jinsi unavyokuwa umekaribiana na hawa "waheshimiwa" kiasi mpaka unajisikia aibu.
Yule askari aliyenileta alikuwa amesimaa mlangoni na nilipoangalia nje ya mlango niliwaona Cheupe na Issack na pembeni yao kidogo wamesimama Baba Bite na yule Dada ambaye nilikuwa bado sijamfahamu mpaka sasa. Wote walikuwa wamesimama koridoni lakini wamekaribia kabisa mlango wakiwa wanafuatilia kinachoendelea huku ndani.
Baada ya kama dakika nne hivi wote mle ndani ya ofisi ya hakimu walikuwa wameacha kunitazama na wameinama wanaandika kwenye makaratasi juu ya meza zao, hakimu akaanza kuongea.
"Mwendesha mashtaka" Hakimu akaongea kwa kifupi huku ameinama anaandika katika makaratasi yake.
Mwendesha mashtaka yule wa kiume akasimama na kuanza kuongea "Muheshimiwa Hakimu shtaka lililoko mbele yako ni shtaka la jinai namba 264 la mwaka 2016 ambapo Jamuhuri inamshtaki Bwana Rweyemamu Charles Kajuna kwa makosa matatu" akanyamaza kidogo.
Nikamuona hakimu anaandika kwa haraka haraka kwenye makabrasha yake.
"Endelea" Hakimu akamueleza muendesha mashtaka bila kumtazama akiwa anaendelea kuandika kwenye makabrasha yake.
"Shtaka namba moja" muendesha mashtaka akaanza kusoma huku ananitazama na kuangalia kwenye makabrasha yake na kunitazama tena. "Siku ya tarehe 23 Novemba 2016, kinyume na sheria za adhabu ya makosa ya jinai namba 333 na 335 (a) ya mwaka 2002, akijua kabisa ni kinyume cha sheria Rweyemamu Charles Kajuna alitumia kadi za benki mali ya Bi. Hasnati Jaffar Kumbea kuiba fedha katika mashine za fedha za Benki ya Barclay's kiasi cha shilingi milioni moja na laki sita"
Mwendesha mashtaka alinisomea shtaka.
Hakimua aliandika andika kwa sekunde kadhaa baada ya muendesha mashata kunyamaza kisha akaniangalia na kuniuliza, "Mshtakiwa kweli ama si kweli?"
"Si kweli!" Nikamjibu
Akainama na kuandika tena kwenye karatasi zake.
"Mwendesha mashtaka?" Hakimu akaongea huku akimuangalia muendesha mashtaka.
Muendesha mashtaka akaendelea tena kunisomea mashtaka..
"Shtaka la pili, Kinyume na Kifungu cha sheria namba 271 ya adhabu ya makosa ya jinai ya mwaka 2002, Rweyemamu Chrles Kajuna akijua kabisa ni kinyume cha sheria alitumia nguvu kumuibia simu ya mkononi Bi. Hasnat Jaffar Kumbea katika mtaa wa mazimbu FK, wilayani Morogoro Mjini, Mkoa wa Morogoro"
Akanyamaza tena kidogo.
"Mshtakiwa kweli ama si kweli?" Hakimu akaniukiza safari hii bila kuniangalia alikuwa anaandika kwenye makaratasi yake.
"Si kweli" nikajibu
"Mwendesha mashtaka" hakimu akaongea akimuangalia muendesha mashtaka.
"Shtaka la tatu, kinyume na kifungu namba 337 cha adhabu ya makosa ya jinai, Rweyemamu Charles Kajuna katika eneo la Mazimbu FK, Wilani Morogoro Mjini, mkoa wa morogoro akijua kabisa ni kosa kisheria alimshambulia na kumpiga Bi. Hasnat Jaffar Kumbea na kumsababishia maumivu Makali"
Nikasomewa tena shtaka la tatu.
"Mshtakiwa kweli au si kweli?"
"Si kweli.!"
Hakimu akaandika tena kwenye karatasi zake.
"Mwendesha mashtaka?" Akamuuliza na kumuangalia mwendesh mashtaka.
"Muheshimiwa hakimu upelelezi bado unaendelea na upande wa Jamuhuri hauna pingamizi juu ya dhamana" akaongea mwendesha mashtaka na kukaa chini.
Hakimu akatumia muda mrefu zaidi safari hii kuandika. Alitumia karibia dakika mbili nzima kisha akainua kichwa na kuniangalia.
"Mshtakiwa unatakiwa uwe na wadhamini wawili na wote watasaini karatasi ya dhamana ya shilingi milioni moja kila mmoja, je una wadhamini ndugu mshtakiwa?"
Hakimu akaniuliza na nilikuwa najiandaa kumwambia hapana lakini kabla sijasema chochote nikasikia mtu anaingia ndani ya ofisi ya hakimu na kuongea kwa kupayuka.
"Tupooo muheshimiwa.!"
Wote tukageuka kuangalia mlangoni. Alikuwa ni Baba bite ameongozana na yule dada nisiyemfahamu. Mikononi wameshika makaratasi. Wakaingia haraka haraka na kunyoosha mkono kumkabidhi karani makaratasi yao.
"Muheshimiwa hawa watu siwafahamu.!" Nikajikuta naropoka kwa nguvu..
"Relax Ray, wacha tukusaidie"
Baba bite akaongea kwa tabasamu na ikanikera zaidi..
"Nooooo siwajui…!"
"Order please!!" Hakimu akafoka na kutukatisha mabishano yetu..
"Mahakama iko inaendelea nawataka muheshimu" akaongea huku anatuangalia mimi na Baba Bite.
"Enhe mshtakiwa unasemaje?"
"Muheshimiwa hawa watu siwajui na wala siko tayari kudhaminiwa nao kulinda usalama wangu!" Nikaongea kwa jazba.
"Ray mimi na wewe tunakaa nyumba moja unawezaje kusema…."
Baba bite akaongea kwa sauti ya juu lakini Muhesgimiwa hakimu akamkatisha.
"Naomba uheshimu mahakama, sijakuruhusu uongee na wala sijakuruhusu kuingia humu ndani… Karani mpe karatasi zake na naomba uondoke kabisa eneo la mahakama"
Muheshimiwa hakimu akaongea kwa hasira na kwa mamlaka.
Baba bite akachukua makaratasi yake huku anatabasamu kwa kujiamini kisha akanigeukia na kutikisa kichwa kwa kunisikitikia.
"Nahahirisha mahakama kwa muda na mahakama itarejea baada ya dakika kumi." Hakimu akaongea baada ya Baba bite na mwenzake kutoka nje.
Kila mtu akasimama na kuanza kuchukua makaratasi yake kutoka nje.
Askari naye akaanza kuniongoza ili kutoka nje.
"Mshtakiwa naomba abaki" hakimu akamuamuru yule askari.
"Sawa muheshimiwa" askari akaitikia na kutoka nje.
Nikabaki nimesimama pale pale nilipokuwa. Ndani ya ofisi ya hakimu tulibaki mimi na yeye tu. Mwanzoni nilipokuwa naingia kwa kiasi Fulani nilivutiwa na Urembo wake lakini sasa baada ya kumshuhudia akidhihirisha mamlaka aliyokuwa nayo, nikawa nimebaki na mtazamo wa kumuheshimu kwa hali ya juu.
"Kaa kwenye kiti mahakama imehairishwa" Hakimu akaongea huku ananiangalia kana kwamba anamuangalia mtoto mdogo.
"Sawa muheshimiwa" nikaongea kwa heshima.
Akachukua mkoba wake wa kike ambao alikuwa ameuwek chini kwenye sakafu na kuuweka juu ya meza. Akaufungua ndani na kuanza kutafuta kitu. Akakipata na kukitoa.
Kilikuwa ni kikaratasi cheupe kimekunjwa. Akanyoosha mkono kunipa.
Nikamtumbulia macho tu nikijiuliza kama ni sahihi nilivyowaza kuwa alikuwa ananikabidhi kikaratasi au ni mawazo yangu. Akaendelea tu kuninyooshea mkono kunikabidhi kikaratasi.
Nikanyoosha mkono na kukipokea.
Baada ya kukipokea nikagundua kuwa kinafanana kabis na vile vikaratasi ninavyoletewaga kutoka kwa Dr. Shirima.
Nikainua kichwa na kumuangalia Hakimu, na yeye alikuwa ananiangalia huku amenikazia macho.
Nikakikunjua kikaratasi. Na ndani kilikuwa kimeandikwa.
"KESHO BISHOP RESIDENCE 4:00 PM
D.S. #14"
Nikakisoma kikaratasi kwa kukirudia rudia. Nikainua macho kumuangalia Hakimu. Bado alikuwa amenikazia macho.
Nilielewa kuwa hiki kikaratasi kimetoka kwa Dr. Shirima na anataka tufanye kikao chetu cha 14 na kikao changu mimi naye safari amepanga kitakuwa katika makazi ya Askofu!
Sikuweza kung'amua mara moja kama huyu Hakimu mrembo naye ni mmoja wa wanachama wa The Board, au ni kibaraka kama nilivyokuwa mimi au wamemtumia tu siku ya leo.
Nikakikunja kikaratasi na kukiweka mfukoni.
Waendesha mashitaka walikuwa mlangoni wanaingia, dakika kumi zilikuwa zimeisha. Wakaingia na kuketi.
Baada ya Hakimu kuandika andika katika makaratasi yake akaanza kuongea.
"Mahakama imerejea tena na kabla ya kuihairisha tulikuwa tunazungumza kuhusu dhamana ya mshtakiwa… Aaahh sasa ni kwamba… aahh baada ya mahakama hii kutafakari kwa kina imeafikia maamuzi kwamba, kwa kuwa mshtakiwa Rweyemamu Charles Kajuna ni mtu anayefahamika na mwenye heshima katika jamii hivyo basi kwa kutumja kifungu cha Sheria namba …..… (sikukishika kichwani kifungu alichotaja) hivyo basi mahakama hii inamruhusu mshtakiwa ajidhaimini yeye mwenyewe."
Nilishtuka na nikagundua sio mimi pekee niliyeshtuka. Hata waendesha mashataka walikuwa wameshtuka zaidi yangu. Wakawa wanaangaliana na kwa haraka yule mwendesha mashtaka wa kiume akainuka.
"Muheshimiwa hakimu…."
Kabla hajamaliza hakimu akamkatisha.
"Kaa chini mwendesha mashtaka sijakuruhusu uongee.. Mshtakiwa?"
Hakimu akaongea kwa mamlaka akinipa mimi nafasi niongee na kumuamuru mwendesha mashtaka akae chini.
Nikapatwa na kigugumizi kwa karibia dakika nzima. Sikujua nisemeje. Inapaswa niwe makini sana kukubali hii "ofa" ya mahakama kwamba nijidhamini mwenyewe. Nilihisi huu ni mtego.
Nikahisi huyu Hakimu anatumiwa na The Board, kwa hiyoThe Board wanataka niwe uraiani. Kwanini??
Nikafikiri haraka haraka. Nikaamua kwamba busara ni kufanya kinyume na The Board wanachokitaka.
"Muheshimiwa hakimu kwa kuzingatia tukio lilitokea na kwa kuzingatia usalama wangu mimi mwenyewe binafsi siko tayari kujidhamini"
"Unaweza kuieleza mahakama unahofia nini?"
"Muheshimiwa nashukuru mahakama yako kwa kuniamnini, lakini naomba mahakama yako ifahamu kuwa siko tayari kujidhamini"
Ule mshangao ambao waendesha mashtaka walikuwa nao mwanzoni uliongezeka mara kumi zaidi. Nahisi walikuwa wanahisi kama wako ndotoni kwa hiki kilichokuwa kinaendelea.
Muheshimiwa nikamuona ameshikwa na hasira. Akanikazia macho kwa takribani dakika mbili pasipo kusema chochote.
"OK.! Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo mshtakiwa utaenda mahabusu gerezani na kesi imehairishwa mpaka tarehe 8 mwezi wa 12"
Hakimu akaongea akiwa serious zaidi huku anaandika. Waendesha mashataka wao bado walikuwa wameduwaa tu hawaelewi wala kuamini nini kimetokea.
Yule askari akaja akanishika mkono na kuniongoza kutoka nje. Moyo wangu ukajaa giza nikifikiria kitakachofuata mbele yangu dakika chache zijazo..
Itaendelea Jumanne Ijayo.. Usikose..
Join my exclusive whatsapp group kusoma simulizi na makala kila siku – 0718 096 811 (kuna “subscription fee”)