Viganja Mashavuni Mwangu

Viganja Mashavuni Mwangu

SEHEMU YA 76

Kila mtu aliyekuwa mahali hapo alishangaa, wazazi wao wakasogea kuangalia kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kimewapata lakini nao waliposogea, wakaanza kusikia kivunguzungu, nao hapohapo wakaanguka kitu kilichomshtua kila mtu aliyekuwa mahali hapo, hakukuwa na mwingine aliyelisogelea gari lile kwani tayari kukaanza kusikika harufu fulani ambayo haikuwa ya kawaida.
*** Edmund alidhamiria kufanya mauaji, hakutaka kufikiria utu, aliamini kwamba kama Walter angekufa basi ingekuwa rahisi kwake kuendelea kuishi na Catherine ambaye alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Sumu yake aina ya Nitrosyl chloride alikuwa nayo chumbani kwake, ilikuwa ni lazima kwenda kwenye gari la mapacha hao walioungana kwa ajili ya kuiweka na kisha kuondoka zake.
Hakutaka kuchelewa, kwa kuwa siku hiyo Walter, Walker na wazazi wao walikuwa wakienda hospitalini katika Hospitali ya Queen Elizabeth kwa ajili ya kumuona Catherine, naye akapanga kwenda huko kwa muda wake.
Aliamini kwamba huko kungekuwa na watu wengi, hakutaka kwenda kikawaida, alifahamu jinsi polisi walivyokuwa wakivaa, suala la kutafuta sare wala halikuwa gumu kwani aliwasiliana na rafiki yake ambaye alikuwa akishona sare hizo kwa ajili ya kuigiza filamu mbalimbali nchini Uingereza, yeye akampelekea mavazi ya polisi ambayo kwa kuyaangalia kwa mbali, hayakutofautiana mpaka pale utakapoyachunguza zaidi.
Akaingia ndani ya gari lake na kuondoka huku akiwa na mtungi huo mdogo. Hakuchukua muda mwingi akafika katika hospitali hiyo, ni kama watu walijua kwamba mapacha hao walioungana wangefika hapo, wengi walikusanyika kwa ajili ya kuwashuhudia tena.
Edmund hakuteremka katika gari lake, alitulia huko huku moyo wake ukichoma kupita kawaida, baada ya kukaa kwa saa moja, akayaona magari yakianza kuingia hapo, akabaini kwamba gari moja lilikuwa limewabeba mapacha wale, hivyo akaanza kufuatilia.
Watu wakaanza kusogea kule kulipokuwa na magari yale huku wakiwa na simu zao mikononi na wengine wakiwa na kamera, walitaka kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
 
SEHEMU YA 77

Baada ya dakika kadhaa, mapacha hao wakateremka huku wakiwa na ulinzi mkubwa, kama kawaida yao wakaanza kuwapungia watu mikono huku wakipiga hatua kuelekea ndani.
“Can you sign an autograph on my book, pleaseee?” (unaweza kusaini kwenye kitabu changu?) aliuliza msichana mmoja kwa sauti ya upole kabisa, japokuwa kulikuwa na ulinzi mkubwa, yeye alifanikiwa kupenya, na walinzi walipotaka kumtoa, Walke akawazuia.
“Mine or his?” (yangu au yake?) aliuliza Walker.
“Both of you,” (nyie wote)
“Okay.” (sawa)
Hilo halikuwa tatizo, wakafanya kama msichana huyo alivyotaka na kisha kupiga naye picha na kuanza kuelekea ndani ya hospitali hiyo. Bwana Cassian na mkewe, Naseku walikuwa na furaha kupita ajabu, hawakuamini kama watoto wao walikuwa wakikubalika kiasi hicho japokuwa walionekana kuwa na matatizo.
Wakati watu wakiwa bize, haraka sana Edmund akateremka kutoka kwenye gari lake na moja kwa moja kuanza kusogea kule gari lililokuwa limewabeba mapacha wale lilipokuwa huku mkononi akiwa na mtungi wa gesi.
Alipofika, akaangalia ndani, akamuona dereva akiwa anavuta sigara, akaanza kulisogelea gari zaidi, alipolifikia, akakigonga kioo, dereva akafungua.
“Unajua kwamba unavunja sheria?” aliuliza Edmund huku akimwangalia dereva.
“Sheria gani?”
Akamuonyeshea bango dogo lililoandikwa kwamba hakukuwa na mtu aliyekuwa akiruhusiwa kuvuta sigara katika eneo la watu wengi likiwemo hospitali kama hiyo.
Haraka sana dereva akaizima sigara yake kwani kwa jinsi Edmund alivyoonekana, jinsi alivyokuwa amevaa sare za bandia za kipolisi, aliamini kwamba mwanaume huyo alikuwa polisi.
“Samahani sana.”
“Hebu teremka, nenda nyumba ya gari nikukute huko. Nataka nipekue, unaweza kuwa na bangi au madawa ya kulevya humu,” alisema Edmund, kwa kuwa alikuwa amefanya kosa, haraka sana dereva akafungua mlango na kwenda nyuma, Edmund akaingia ndani, akachukua sumu ile na kuanza kuipulizia katika sehemu ya kiyoyozi, aliipulizia kwa wingi huku kiyoyozi hicho kikiwa kimezimwa, alipomaliza, akafunga mlango.
 
SEHEMU YA 78 “Una bahati sikukuta kitu. Sijakukataza kuvuta, kama utaendelea, hakikisha unafunga vioo, washa kiyoyozi na ndipo uvute, vinginevyo sitokuelewa,” alisema Edmund huku akiwa anamwangalia dereva huyo.
“Haina shida.”
Dereva akaingia ndani, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kufunga mlango, kioo kikashushwa, akachukua sigara nyingine, akaiwasha na kuanza kuivuta.
“Alisema na kiyoyozi,” alisema na hapohapo kuwasha kiyoyozi.
Hilo likaonekana kuwa kosa kubwa kwani hapohapo sumu iliyokuwa imepuliziwa humo ikaanza kutoka mfululizo. Ilikuwa sumu mbaya ambayo ilikuwa ikiingia mwilini mwa binadamu kwa haraka na kuharibu ini huku ikianza kuusimamisha moyo na kuziba mishipa ya damu.
Dereva hakuchukua hata dakika moja, palepale alipokuwa, akatulia tuli, mwili ukaanza kukakamaa, mapovu yakaanza kumtoka mdomoni na hatimaye kutulia tuli.

Je, nini kitaendelea?
 
Samahani wapendwa ktk bwana sehemu ya 75 ilisahaulika bahati mbaya nawawekea hapa chini
 
SEHEMU YA 75

Kila Muingereza alijua kwamba Walter na Walker walikuwa nchini Uingereza. Watu wengi walijazana katika Hospitali ya Queen Elizabeth kwa ajili ya kuwaona mapacha hao waliokuwa gumzo kila kona duniani.
Wale waliokuwa katika miji mingine kama Liverpool, Newcastle, Manchester na sehemu nyingine wakaondoka kuelekea jijini London kwa ajili ya kuwaona mapacha hao waliokuwa na vipaji visivyo vya kawaida.
Walikuwa ndani ya hospitali hiyo huku watu wengi wakiwa nje. Kila mtu alitamani kwenda kuwaona lakini hakukuwa na mtu aliyepewa nafasi, wengi wakaambiwa kwamba walitakiwa kusubiri mpaka watu hao watakapoondoka, wawapige picha kwa mbali lakini si kuwasogelea.
Polisi walikuwa makini, kuwalina Walter na Walker haikuwa kazi ndogo hata kawaida. Watu walisumbua, walipata kazi kubwa ya kuwalinda kuhakikisha hakuna mtu mbaya yeyote ambaye anawasogelea na kuwafanya kitu chochote kile.
"Tunataka kuwaona! Mbona jana nasikia watu waliowaona hapa hospitali ila leo mnatukatalia?” alihoji jamaa mmoja, alionekana kuwa na hasira.
“Nyie subirini! Jana ni jana na leo ni leo!”
“Haiwezekani bwana. Yaani kuwaona mnataka mpaka tufanye fujo?” alihoji jamaa huyo.
Ilikuwa kazi ngumu kuwaona watu hao. Walter na Walker waliendelea kukaa hospitalini huku wakimfariji Catherine aliyekuwa ameanza kupata nafuu, ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni, kama kawaida wakatoka tayari kwa kuondoka mahali hapo.
Walipotoka nje, polisi wakafanya kazi ya ziada kwani kila mmoja alitaka kuzungumza nao huku wengine wakiwa na vitu vyao kwa ajili ya kusainiwa. Kwa mwendo wa taratibu, wakaanza kusogea kule watu walipokuwa na kuanza kusaini vitabu vyao huku wengine wakiwapiga picha.
Waliwafurahisha watu, walipomaliza, wakaanza kupiga hatua na wazazi wao kuelekea katika maegesho ya magari kwa ajili ya kuondoka mahali hapo. Dereva alikuwa ndani ya gari hilo, alikuwa amelala, wakaufungua, hawakujali sana, walichokifanya ni kuufungua mlango wa gari hilo lililokuwa limefungwa vioo, hata kabla ya kuingia ndani, hapohapo wakaanguka chini, wakaanza kutoka mapovu na miili kuwatetemeka.
 
SEHEMU YA 79

Kila mtu aliyekuwa ameliona tukio lile aliogopa, wote wakasogea nyuma kwani hali ilionekana kutokuwa nzuri. Watu walibaki wakiwaangalia Walter na Walker walivyokuwa wakihangaika pale chini walipokuwa na wazazi wao.

Hakukuwa na mtu aliyetoa msaada zaidi ya watu hao kuanza kupiga picha kana kwamba walikuwa waandishi wa habari. Kwa kuwa ilionekana kama kulikuwa na gesi iliyokuwa imewadhuru, hapohapo wanaume wawili wakajifunga vitambaa puani na mdomoni, wakasogea kule walipokuwa watu wale na kuanza kuwasaidia, machela zikaletwa, wakapakizwa na kuanza kuingizwa ndani.
“Nini kimetokea?” lilikuwa swali la kwanza alilouliza nesi.

“Saidia kwanza. Tunahisi ni sumu!”
“Sumu?””Ndiyo! Husikii harufu ya Nitrosyl chloride? Ni sumu hatari sana hii,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa akitoa msaada.

Kila mtu akashtuka, dunia ikaingiwa na majonzi mazito, hakukuwa na aliyeamini kile kilichokuwa kimetokea. Kila mtu alikuwa na hofu, wengi wakaona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mapacha wale.

Lawama zote zilikwenda kwa Waingereza, ilikuwaje washindwe kuzuia jambo hilo na wakati walijua kabisa kwamba watu hao walikuwa maarufu hivyo kungekuwa na watu wengi waliotaka kuwaua kwa kuwa tu waliwaoneka wivu?

Kila mmoja akahisi kwamba kulikuwa na kiongozi mkubwa serikalini alikuwa amehusika katika tukio hilo la mauaji. Waziri mkuu nchini humo, Bwana Sinclaire hakutaka kuchelewa, haraka sana akawaita waandishi wa habari na kuwaomba msamaha kwa lililotokea lakini pia ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba mtu aliyefanya tukio hilo akipatikana haraka iwezekanavyo.

“Na hali zao?” aliuliza mwandishi mmoja.
“Bado sijajua chochote kile kwa kuwa baada ya kupewa taarifa nikawaita kwa ajili ya kuzungumza nanyi,” alisema Bwana Sinclaire huku akiwaangalia waandishi waliokuwa wamemzunguka.

Hospitalini hakukukalika, kila mtu alikuwa na hofu, sumu ambayo walikuwa wamepuliziwa ilikuwa ni sumu hatari ambayo ilikuwa ikitumika kuulia wanyama wakubwa msituni na samaki baharini.
 
Sehemu ya 80

Kitendo cha kuwapata kidogo tayari ilionyesha nguvu zake kiasi kwamba walianguka na kupoteza fahamu huku hali ya miili yao ikianza kubadilika ghafla pamoja na wazazi wao.

Madaktari walikuwa na kazi kubwa kuokoa maisha ya mapacha hao na wazazi wao. Haraka sana wakawapeleka katika chumba cha upasuaji na kuanza kuwahudumia haraka sana.

Ilikuwa kazi kubwa kwani walitakiwa kwanza kuondoa sumu ile ambayo ilikuwa ikisambaa taratibu katika miili yao.

Wakawatundikia dripu zilizokuwa na maji yaliyotiwa dawa ambazo zilikuwa na uwezo wa kuruhusu matone kumi na tano kwa dakika moja tu.

“Hii itawasaidia!” alisema daktari mmoja.
“Kweli?” aliuliza nesi.
“Ndiyo! Ila hatutakiwi kuamini sana kwani kadiri dakika zinavyozidi kwenda mbele, mapigo yao yanazidi kushuka,” alisema daktari huyo.

“Kwa hiyo wanaweza kufa?”
“Uwezekano wa kupona ni asilimia thelathini na kufa ni asilimia sabini. Cha msingi ni kumuomba Mungu tu,” alisema daktari huyo, pamoja na utaalamu wake mkubwa lakini kwa sumu waliyokuwa wamepuliziwa watu wale, ilionekana kumshinda.

Serikali ikaamua kuongeza madaktari wengi kumi kutoka katika hospitali nyingine. Ilikuwa ni lazima wapambane usiku na mchana kuokoa maisha ya watu hao kwani kama wangekufa katika ardhi yao ingekuwa aibu sana dunia nzima hivyo iwe isiwe ilikuwa ni lazima kupambana kuokoa hali zao.

*** Polisi jijini London walichanganyikiwa, hawakuamini kile kilichotokea kama kweli kilitokea katika ardhi ya Uingereza.

Kila mtu alikuwa akizungumza lake, wengi waliona nchi hiyo ikiwa na uzembe mkubwa kiasi kwamba walishindwa kuweka ulinzi wa kutosha kuhakikisha vijana hao wanakuwa salama mpaka pale ambapo wangeondoka nchini humo.

Haraka sana, mkuu wa jeshi la polisi nchini humo, Bwana Simon Pegg akazungumza na kitendo cha Usalama wa Taifa, Military Intelligence Section 6 kwa lengo la kutaka kujua kila kitu kilichokuwa kimetokea.
 
SEHEMU YA 81

Haraka sana maofisa wa Usalama wa Taifa wakaanza kufanya kazi hiyo. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda mpaka katika hospitali hiyo kwa lengo la kuangalia kwenye kamera kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Walipofika huko, wakapelekwa katika chumba kilichokuwa na televisheni ambacho kiliunganishwa na kamera thelathini na sita zilizokuwa katika hospitali hiyo.

Walitaka kujua kila kitu kilichokuwa kimetokea tangu mapacha hao walipofika katika hospitali hiyo mpaka tukio la kuupatwa na sumu lilivyotokea.

Hilo halikuwa tatizo, kila kitu kilikuwa kimerekodiwa na kilichofanyika ni kuonyeshwa kila kitu kilichotokea.
Walianza kufuatilia.

Dakika kumi kabla ya mapacha hao kufika mahali hapo wakaanza kuangalia mazingira jinsi yalivyokuwa.

Hakukuwa na mtu yeyote ambaye walimtilia shaka, kila aliyekuwa mahali hapo alionekana kuwa na hamu kubwa ya kuwaona mapacha hao na ndiyo maana kila mmoja alishikilia simu yake tayari kwa kupiga picha.

Baada ya dakika kadhaa, wakayaona magari yaliyokuwa kwenye msafara mfupi wa mapacha hao ukianza kuingia ndani ya eneo la hospitali hiyo.

Kila mmoja alikuwa akiyaangalia kwa makini mpaka pale yalipokwenda kupaki.
Waliwaona walipokuwa wakiteremka, lengo lao halikuwa kuwaangalia mapacha hao bali lengo lao kubwa ni kuangalia ni nani alikuwa amekwenda katika gari lile baada ya mapacha hao kuteremka.

Wakati wameelekea ndani, wakamuona polisi mmoja akiteremka katika gari lake huku mkononi akiwa na kitu ambacho hawakuwa wakikifahamu kwa kuwa ilikuwa ni picha ya mbali kabisa.

Polisi yule akaanza kutembea mpaka lilipokuwa gari lile walilokuwa mapacha wale na kuanza kuzungumza na dereva. Hawakujua walizungumza kitu gani lakini baada ya dakika moja wakamuona dereva akiteremka na kuelekea nyuma ya gari na polisi yule kuingiza kichwa kwa ndani.

“Hebu vuta kwa karibu, vuta zaidi,” alisema Bwana Pegg ambaye naye alifika kwa ajili ya kuangalia.
 
SEHEMU YA 82

Picha ya karibu ikavutwa zaidi, halafu akamwambia arudishe nyuma na kisha kutakiwa kuvuta kile kitu kilichokuwa mkononi mwake, walitaka kujua kilikuwa kitu gani. Kilipovutwa, hakukuwa na mtu aliyeamini, ulikuwa mtungi mdogo wa gesi kali aina ya Nitrosyl Chloride iliyokuwa ikitumika kuulia samaki baharini na wanyama wakali.

“Huyu ndiye aliyeweka hiyo gesi ambayo imekuwa sumu. Hebu mvute karibu. Ni polisi kweli huyu?” aliuliza.
Jamaa aliyekuwa ameshikilia kipanya akaanza kuvuta picha kwa karibu zaidi. Walikuwa wakitaka kuona kama kweli huyo alikuwa polisi au la.

Alipovutwa, waliangalia sare zake, hazikuwa origino kama za polisi wengine kitu kilichomaanisha kwamba mwanaume huyo ndiye aliyefanya tukio hilo la kuwamaliza mapacha hao.

“Vuta sura yake, piga picha halafu anza kupeleka sehemu zote. Nahitaji ndani ya nusu saa mtu huyo awe amekamatwa,” alisema Bwana Pegg na hapohapo picha ya Edmund kuchapishwa na kuanza kupelekwa sehemu mbalimbali, hasa katika vituo vya polisi.

Na kwa sababu waliipata picha ya sura yake, walichokifanya ni kutaka kupata data zote kuhusu mwanaume huyo ambaye waliamini kwamba kama alikuwa ni rais wa Uingereza basi ilikuwa ni lazima kujiandikisha kama rais wa nchi hiyo na hivyo kuwa na data zake zote.

Wakaiingiza picha ile katika kompyuta ambayo ilikuwa na taarifa ya raia wote wa Uingereza na kuanza kumtafuta mwanaume huyo.

Zaidi ya picha elfu moja zilikuwa zikipita ndani ya sekunde sitini na baada ya dakika tano, picha yake ikasimama na neno kubwa lililosomeka Match 100% likionekana vizuri kwamba picha ile iliyokuwa imeingizwa ilifanana kwa asilimia mia moja na picha iliyokuwa ikionekana.

“Anaitwa Edmund Jefferson. Anaishi hapa London katika Mtaa wa Camberwell nyumba namba 297.

Kikosi cha askari ishirini wanatakiwa kwenda huko haraka sana,” alisema Pegg na hivyo kikosi cha kwenda huko kupigiwa simu na kutumiwa picha ya mtu aliyekuwa akitakiwa na maelezo yote kuhusu yeye.
 
SEHEMU YA 83

Kidogo moyo wa Edmund ukajisikia amani, akahisi kwamba alifanikiwa kwa asilimia mia moja kufanya jambo lile lililompa uhakika kwamba mbaya wake, Walter alikufa katika gesi ile kali.

Akaondoka hospitalini hapo, njiani, redioni ni taarifa za mapacha hao ndizo zilzokuwa zikisikika kila kona kwamba walikuwa wamekufa.

Wakati dunia ikihuzika na kulia, kwake hali ilikuwa ni tofauti kabisa kwani moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida.

Alipofika nyumbani, hakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kuondoka nchini humo kwa kuamini kwamba mara baada ya kugundulika ilikuwa ni lazima kutafutwa kila kona.

Akachukua baadhi ya vitu vyake na kuondoka zake huku lengo lake kubwa likiwa ni kuelekea nchini Ireland ambapo aliamini kwamba huko angeishi kwa amani kabisa.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumpigia simu rafiki yake, Thom na kumshukuru huku akimwambia kwamba alikuwa akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Ireland.

“Nimefanikisha. Nashukuru sana,” alisema Edmund, akachukua begi lake lililokuwa na baadhi ya vitu na kuondoka mahali hapo.

Akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha, hakutaka kuaga, alipoingia barabarani tu, akasikia ving’ora vya polisi kwa mbali, akapishana nao, yaani wakati yeye akiondoka nyumbani kwao, nao ndiyo walikuwa wakiingia.

“Hamuwezi kunipata!” alisema Edmund huku akitoa tabasamuu pana ambapo alipokuwa akiangalia nyuma kupitia kioo cha gari cha pembeni, akawaona polisi wakiingia katika eneo la nyumba yao. Akaongeza gia na kukanyaga moto. Akapotea eneo hilo.
 
SEHEMU YA 84

Ilikuwa ni lazima kuondoka kuelekea nchini Ireland, hakutaka kuonekana kwa kuhisi kwamba ilikuwa ni lazima kutafutwa na polisi kwa kile alichokuwa amekifanya.

Edmund hakuwa na uhakika kama angegundulika, hakuwa ameziona kamera ndogo za CCTV zilizokuwa zimefungwa kila kona hospitalini hapo.

Aliendesha gari lake kwa mwendo wa kawaida kabisa, hakutaka kushtukiwa na polisi ambao mara nyingi magari yao yalikuwa mitaani yakitembea huku na kule kuhakikisha usalama kila kona hapo London.

Wazo lake kwa wakati huo lilikuwa ni kwenda Olympia London ambapo huko angenyoosha moja kwa moja mpaka Twickenham, huko angepumzika kidogo kabla ya kuelekea katika Jiji la Reading, angeingia Swindon, Bristol ambapo hapo angechukua treni ya chini ya maji mpaka nchini Ireland.

Akaliingiza gari mpaka katika Barabara ya Brixton na kuanza kuelekea Upande wa Kusini huku lengo lake likiwa ni kufika West Noorwood ambapo hapo angechukua barabara nyingine ya Tooting Bec ambayo ingempelekea Upande wa Mashariki mpaka Battersea, huko angechukua Barabara ya S Circular ambayo ingempeleka mpaka Twickenham.
Kuanzia hapo Camberwell alichukua saa tatu mpaka kufika huko.

Kila alipopita, hakukuwa na tatizo lolote lile, alihisi kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akimfuatilia. Hapo Twickenham akaendelea mbele na baada ya saa moja akafika Felthman ambapo hapakuwa mbali kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow.

Hapo ndipo kulipokuwa na barabara mbili zilizoungana, moja ilikuwa ikienda upande wa Kaskazini ambayo ilikwenda mpaka Harmodsworth ambapo kama angekata kulia basi angekwenda mpaka Dorney na kushuka kwa kuelekea chini.

Ilikuwa ni njia ndefu ambayo aliamini angetumia zaidi na saa tano. Kwake, njia hiyo haikuwa salama hata kidogo, kwa kukubali kwenda huko kulimaanisha kwamba ilikuwa ni lazima angekamatwa na polisi kama tu wangekuwa wakimtafuta kwa kuwa barabara hiyo haikuwa mbali na uwanja wa ndege.

Akaamua kuichukua Barabara ya ya Engham ambayo ilimpeleka mpaka Thorpe alipokutana na barabara nyingine ambayo ndiyo ilikuwa ikimpeleka mpaka Bristol.
 
Back
Top Bottom