SEHEMU YA 72
Kupatikana kwa Walter kulimaanisha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa uhusiano wake na msichana Catherine aliyekuwa kitandani. Moyo wa Edmund uliuma na kuchoma sana, kila alipokuwa akimwangalia mwanaume huyo ambaye aliungana na pacha mwenzake kulimaanisha kuwa huo ndiyo ungekuwa mwisho, yaani alitakiwa kusahau kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Hakutaka kukubali, kwa wakati huo alikuwa tayari kupoteza kila kitu isipokuwa kumpoteza Catherine ambaye kila alipokuwa akimwangalia, kila siku uzuri wake uliongezeka maradufu.
Japokuwa alikuwa kitandani lakini kitendo cha kumuona Walter akiwa amefika mahali hapo, Catherine akaonekana kuwa na furaha mno, furaha ambayo Edmund mwenyewe alikiri moyoni kwamba hakuwahi kumuona msichana huyo akiwa kwenye furaha kama siku hiyo.
“Nilikukumbuka sana,” alisema Catherine huku akimwangalia Walter machoni.
“Nilikukumbuka pia. Sikutaka nione ukiendelea kuwa kwenye matatizo halafu mimi nipo. Nitahakikisha nakulinda maisha yangu yote,” alisema Walter.
Wazazi wa pande zote tatu walibaki wakiwaangalia watu hao, kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo Edmund alivyozidi kuumia. Hakukuwa na mtu aliyefahamu kile walichokuwa wameongea zaidi ya wao wawili tu.
Alivumilia tu kukaa na hata alipokuwa akitambulishwa, alijibaraguza kwa kuonekana kuwa na tabasamu pana na wakati moyo wake ulikuwa ukiwaka moto kwa wivu.
Hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka na kurudi nyumbani. Ndani ya gari, alikuwa akilia kama mtoto, hakuamini kilichokuwa kikiendelea. Uwepo wa Walter ulimaanisha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yake.
Alipofika nyumbani, akajifungia chumbani na kuanza kulia. Alipenda mpaka kufikia hatua ya mwisho kabisa, hatua ambayo aliona ikivuka hapo angekuwa kichaa, mapenzi yaliuendesha moyo wake, yalimsumbua kupita kawaida na ndiyo maana alipogundua kwamba mwanaume aliyekuwa amemuona alikuwa Walter, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.
“I must kill him,” (ni lazima nimuue)
Huo ndiyo ulikuwa uamuzi alioufikia kipindi hicho, hakutaka kuona akimkosa Catherine kwa sababu ya Walter, alitamani kuendelea kulilinda penzi lake lakini si kuona likipotea na kuchukuliwa na mtu mwingine.