Viganja Mashavuni Mwangu

Viganja Mashavuni Mwangu

SEHEMU YA 53

Alisakamwa moyoni mwake mpaka akahisi maumivu mazito, akabaki akisikitika kwa kile alichotaka kukifanya.

Nguvu ya kutaka kufanya mauaji ikaanza kuondoka moyoni mwake na akajikuta akiingiwa na upendo wa hali ya juu kwa watoto wale.

“Siwezi kuwaua! Siwezi kuuawa watoto wasio na hatia,” alisema Sikujua.
Aliendelea kusubiri mpaka msafara uishe ndipo waliporuhusiwa akaliondoa gari lake mahali hapo na kuondoka.

Aliambiwa kwamba ni lazima aende akawaue watoto hao, hakutaka kufanya hivyo hata kidogo hivyo alichokifanya ni kuondoka mpaka katika soko la Mwananyamala ambapo akanunua kuku wawili na kisu kisha kuingia ndani ya gari.

Kwanza hakutaka kuondoka kuelekea baharini, alichokitaka ni kwenda kwa rafiki yake aliyekuwa akiishi Magomeni, alipofika, akamuachia watoto hao kwa lengo la kuwafuata baadaye.

“Wewe! Ndiyo watoto gani hawa?” aliuliza rafiki yake huyo huku akishangaa.
Sikujua hakuwa na jinsi, akamwambia rafiki yake huyo kila kitu kilichotokea kwamba hakutaka kuwamaliza watoto hao, alikuwa kwenye harakati kubwa ya kuokoa maisha yao hivyo ilikuwa ni lazima amsaidie kwa ajili ya kuwa nayo kwa muda wakati yeye akielekea Coco Beach kufanya kile alichotaka kufanya.

“Usichelewe,” alisema rafiki yake huyo na kuondoka.
Kidogo moyo wake ukajisikia amani, akafurahi, akawaangalia kuku wale, walikuwa wakilia, aliondoka nao mpaka alipofika Coco Beach ambapo kwa muda huo hakukuwa na watu wengi, akawachukua wale kuku, akawachinja kisha kunyunyizia damu zile ndani ya gari lile, hakuishia hapo, akawaweka katika mfuko mweupe wa nailoni ambao ulionyesha jinsi ulivyolowa damu huku ndani kukiwa na kitu, akaupiga picha, akaliacha na yeye kuondoka zake kutoa taarifa kwamba mauaji aliyokuwa ameambiwa, yalikuwa yamefanyika.
 
SEHEMU YA 54

Kila mmoja alikata tamaa, wakajua kwamba watoto wao walikuwa wameuawa kwani damu zilionekana ndani ya gari na kila mmoja aliamini kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuwaona mapacha hao.

Walikuwa na pesa, kuwapoteza watoto wao kuliwafanya kutokuwa na furaha ya utajiri ule, kuliwafanya kuona kwamba kila kitu walichokuwanazo mikononi mwao kupotea, utajiri huku watoto wako wakiwa wameuawa hakika yalikuwa ni zaidi ya maumivu.

Siku ziliendelea kukatika, Cassian alimuonea zaidi huruma mke wake, alionekana kuwa mwanamke mnyonge ambaye kila siku alikuwa akilia tu, moyo wake ulikuwa na maumivu makali mno na aliamini kwamba kama asingemfariji basi mwanamke huyo angeugua ugonjwa wa moyo na mwisho wa siku kufariki dunia.

Ilipofika siku ya nne huku kila mmoja akiwa na huzuni tele Cassian akaletewa taarifa na daktari ambaye aliichukua damu ile na kwenda kuipima, taarifa ilionyesha kwamba damu ile haikuwa ya binadamu bali ilikuwa damu ya kuku.

Alishindwa kuamini, hapohapo akamfuata mke wake na kuanza kuzungumza naye, akamwambia kuhusu ripoti hiyo aliyopewa na daktari kwamba damu waliyoikuta ndani ya gari haikuwa damu ya watoto wao bali ilikuwa damu ya kuku.

“Unasemaje?” aliuliza Naseku huku akiyafuta machozi yako.
“Ni ripoti ya daktari!”
“Sasa watoto wetu wapo wapi?”

Hilo lilikuwa swali ambalo kila mmoja hakuwa na majibu nalo.

Walishindwa kujua mahali walipokuwa watoto wao, mpaka kufikia hatua hiyo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumshukuru Mungu kwa kuwa watoto wao hawakuwa wameuawa kama walivyokuwa wakihisi kabla.

Mbali na swali kuhusu mahali walipokuwa watoto wao lakini pia kulikuwa na swali jingine kwamba kama Sikujua aliwateka watoto wao na kuondoka nao, kwa nini hakuwamaliza?

Je, hakuwamaliza kwa kuwa aliuawa yeye au ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
Wakawasiliana na polisi na kuwapa taarifa hizo.

Wao wenyewe hawakuamini, walijaribu kutafuta kila sehemu, tena wakati mwingine wakiwatumia hata wapelelezi wa
 
SEHEMU YA 55

Kazi ikaanza upya, haikuwa kuzitafuta maiti bali kilichokuwa kimetokea ni kutafuta mahali watoto walipokuwa. Walimwambia kwamba wangempa taarifa kwamba watoto wake walikuwa mahali fulani hivyo kumtaka kuwa na matumaini juu ya hilo.
“Kweli watapatikana?” aliuliza Naseku, muda wote alionekana kuwa na hofu tele.
“Wala usijali! Tumuombe Mungu, naamini watapatikana,” alisema Cassian huku akimkumbatia mke wake. **** Sikujua alikuwa na mawazo tele, aliwachukua watoto wale na kuishi nao huku kila mmoja akijua kwamba walikuwa wameuawa ufukweni. Hawakuwa watoto wasumbufu, hawakuwa watoto wa kulia na kwa sababu walikuwa wamemzoea sana, muda wote walionekana kuwa na furaha mno.
Moyo wake ulimuuma mno, alijua ni kwa jinsi gani CAssian na mkewe, Naseku walikuwa wakiumia, walilia na hivyo alichokifanya ni kutamani kuwasiliana nao kwa lengo la kuwakabidhi watoto wao.
Hakutaka kuchelewa, haraka sana akachukua simu na kumpigia Cassian, simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya mwanaume huyo kuanza kusikika upande wa pili. “Sikujua!” aliita Cassian, kwa jinsi alivyosikika, msichana huyo akajua kwamba aliwekwa loud speaker, ila hakutaka kujali.
Hakutaka kupindisha maneno, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuomba msamaha kwa kila kitu alichokuwa amekifanya, alijua kwamba aliwaumiza na kuwafanya kulia lakini aliyafanya yote hayo kwa kuwa nyuma kulikuwa na mtu aliyemlazimisha kufanya hivyo.
Hakutaka kuficha, alimwambia Cassian kwamba mtu aliyekuwa amemtuma alikuwa Evelyne ambaye alilipa kiasi kikubwa cha pesa kuhakikisha watoto hao wanauawa haraka iwezekanavyo kwa kuwa tu siku za nyuma aliumizwa hivyo na yeye alitaka kuwaumiza.
Cassian aliposikia maneno hayo, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa kasi, hakuamini alichokisikia, ilikuwa msichana huyo aendelee kuwafuatilia na wakati walikuwa wamekwishamalizana tangu kitambo? Moyo wake ukawaka kwa hasira, hakutaka kuona akibabaishwa na msichana huyo hivyo ilikuwa ni lazima kupambana naye.
“Watoto wangu wapo wapi?” aliuliza Cassian huku akitetemeka, pembeni alikuwepo mke wake aliyekuwa akisikia kila kitu, machozi yalikuwa yakimtoka kwa furaha kwani aliamini kwamba angewapata watoto wake.
 
SEHEMU YA 56 “Ninao!”
“Unao hapo? Niambie upo wapi nikufuate,” alisema Cassian.
“Naogopa!”
“Unaogopa nini?”
“Utanikamata!”
“Sikujua! Umenisaidia, uliagizwa kuwaua watoto wangu, hukufanya hivyo, kwa maana hiyo umenisaidia, siwezi kukumata. Nakuahidi hata kuja huko nakuja na mke wangu tu. Usiogope, niambie upo wapi,” alisema CAssian.
Alimaanisha, alichokuwa akikihitaji kilikuwa ni watoto wake tu, japokuwa Sikujua alikuwa akiogopa lakini hakuwa na jinsi, akawaambia mahali alipokuwa na mwanaume huyo kwenda huko kuwachukua watoto wake.
Njiani, hakukuwa na aliyeamini, hawakujua ni kwa namna gani walitakiwa kumshukuru Sikujua ambaye alitumwa kuwaua lakini hakutaka kufanya hivyo kwa kuwa tu moyo wake ulijikuta ukishikwa na upendo wa ajabu, huruma ambayo haikuwahi kumpata kabla.
“Mke wangu! Usilie, ngoja tukawachukue watoto wetu,” alisema Cassian huku akiendesha gari kuelekea Magomeni.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika huko, kwa maelekezo ya msichana huyo, wakatokea nyumbani kwake alipokuwa akiishi na kuingia ndani. Hawakuamini, waliwakuta watoto wao wakiwa kwenye kochi sebuleni huku kukiwa na chupa ya maziwa pembeni.
Haraka sana Naseku akawasogelea, akawabeba kisha kuwakumbatia. Huzuni aliyokuwa nayo moyoni, kilio alichokuwa amelia kwa siku tatu mfululizo kikapotea, furaha ya ajabu ikamuingia moyoni mwake.
Cassian akamsogelea mke wake na kumkumbatia. Wakati hayo yote yakiendelea, Sikujua alikuwa pembeni, alionekana kuwa na hofu nzito moyoni mwake, aliteteka, hakujiamini, aliona kama mwanaume huyo angemfanyia jambo lolote lile baya.
“Hutakiwi kuogopa Sikujua,” alisema Cassian huku akimwangalia msichana huyo.
Walimshukuru msichana huyo kwa wema wake, hawakuwa na cha kumlipa kwani kwa kuwaokoa watoto wao walimaanisha kwamba hiyo ilikuwa ni zaidi ya pesa, kilikuwa kitu kikubwa ambacho hata kama wangemlipa milioni mia moja bado isingelingana na kile alichowafanyia.
“Unataka tukufanyie nini?” aliuliza Cassian huku akimwangalia Sikujua.
Msichana huyo hakuhitaji kiasi chochote cha pesa, kitu pekee alichokihitaji ni kuwa huru tu.
 
SEHEMU YA 57

Hiyo haikutosha, Cassian akamuahidi kwamba angemlipa kiasi cha shilingi milioni hamsini, angemfungulia biashara kwanii kwa jinsi maisha aliyokuwa akiishi hapo nyumbani kwake, hayakuwa mazuri hata kidogo.
“Halafu mimi niache nidili na huyu msichana,” alisema Cassian kisha kuondoka nyumbani hapo huku Sikujua akiwa na amani tele moyoni mwake.
Huo ndiyo ukawa mwanzo, kupatikana kwa watoto hao ilikuwa siri kubwa, aliamini kwamba kama wasingewaficha basi hali ya Sikujua kule alipokuwa ingekuwa mbaya, inawezekana wenzake ambao walikubaliana wawamalize wakajua kwamba walidanganywa na hivyo kumuua yeye.
Akamuhakikishia ulinzi na hivyo kuendelea na maisha yao kama kawaida. CAssian alipanga kumtafuta Evelyne, alitaka kummaliza kwa kile alichokiona kwamba kingemfanya kuwa na amani moyoni mwake, akamwambia mke wake alichotaka kukifanya kwamba amtafute msichana huyo na kumuua lakini mkewe akamsihi kwamba hakutakiwa kufanya hivyo.
“Ila alitaka kuwaua watoto wetu!” alisema Cassian.
“Bado si sababu!”
“Kwa hiyo tumuache?”
“Ikiwezekana!”
“Ila atarudi tena na kuwaua endapo atajua kwamba wapo hai!” alisema Cassian.
“Tuongeze ulinzi, uwe mkubwa zaidi na tusimwamini mtu,” alisema Naseku.
Mkewe akaubadilisha moyo wake, maneno mazito yakamuingia na kumwambia kwamba hakutakiwa kulipa ubaya kwa ubaya bali alitakiwa kulipa ubaya kwa wema, akaamua kuachana na msichana huyo na kufanya mambo yake.
Familia ikawa ya furaha tena, siku zikakatika, kila mtu aliyafurahia maisha yake. Kuwa na watoto hao ndani ya nyumba ilikuwa siri kubwa, cha ajabu kabisa hata polisi hawakujua kama watoto hao walipatikana.
Ulinzi ukawa mkubwa, hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo kiholelaholela, Cassian na mkewe wakaishi kama jinsi ambavyo mabilionea walivyokuwa wakiishi. Siku zikakatika, miezi ikakatika mpaka watoto hao, Walter na Walker walipofikisha umri wa miaka miwili.
Walikuwa wameungana kama ilivyokuwa. Japokuwa walikuwa hivyo lakini hawakutaka kabisa kwenda kuwatenganisha, waliungana sehemu mbaya, walichangia sehemu ya ubongo, kwa kuwaangalia, walionekana kuwa na furaha tele, hawakuonekana kuumizwa na hali waliyokuwa nayo.
 
SEHEMU YA 58

Japokuwa walikuwa wameungana lakini watoto hao walikuwa wazuri wa sura, hata wazazi wao walipokuwa wakiwaangalia, walionekana kuwapenda, walivutia na walikuwa na uhakika kwamba wangemvutia msichana yeyote ambaye angewaangalia.
Walipofikisha umri wa miaka mitatu wakaanza kusoma katika shule ya chekechea ya Amazon Day Care iliyokuwa Mikocheni B, shule iliyokuwa ikisomwa na watoto wa mawaziri na matajiri mbalimbali Tanzania. Mbali na watoto wa matajiri, pia kulikuwa na watoto wa mabalozi wa nchi mbalimbali.
Siku ya kwanza kufika shuleni hapo kila mtu alikuwa akiwashangaa, walimu hawakuamini kama wangeweza kuwaona watoto walioungana kama hao, walizoea kuwaona katika televisheni na sehemu nyingine lakini hawakuamini kama ingetokea siku wangewaona kwa macho yao.
Waliwashangaa lakini wakati mwingine waliamini kwamba Mungu alikuwa wa ajabu sana kwani pamoja na kuungana huko watoto hao walikuwa wazuri mno, sura zao zilionyesha kabisa kwamba huko mbeleni wasichana wangechanganyikiwa nao sana.
“Jamani hawa watoto wazuri sijawahi kuona,” alisema mwalimu Getrude huku akiwaangalia watoto hao, alitamani hata wangekuwa watoto wao.
“Kweli kabisa. Ningepata watoto wenye sura nzuri kama hawa, nadhani ningewaambia wazazi wa watoto wa kike mtaani kwangu wawe makini na mageti yao,” alisema mwalimu Susan na wote kuanza kucheka.
Walimu walikuwa wakiuzungumzia uzuri wa watoto hao, walikuwa na uzuri wa ajabu mno. Shuleni hapo walikuwa wachangamfu mno, japokuwa kwa siku za kwanza watoto wengine walikuwa wakiwaogopa lakini mwisho wa siku wakawazoea na kucheza nao kiasi kwamba kila mmoja alifurahia uwepo wa watoto hao shuleni hapo.
“Jamani! Nina wasiwasi, wale Jackline na Rosemary, nahisi baadaye huko kutakuja kutokea jambo,” alisema mwalimu Susan ofisini.
“Wale watoto wa mabalozi?”
“Ndiyo! Yaani naona wamezidisha ukaribu na watoto hawa. Wakiendelea kuwa karibu hivi kila siku, miaka na miaka, kuna jambo linaweza kutokea,” alisema mwalimu huyo na wengine kuanza kucheka.
 
SEHEMU YA 59

Jackline alikuwa mtoto wa Balozi wa Marekani, Bwana Godluck Puff huku Rosemary akiwa mtoto wa Balozi wa Uingereza, Bwana Emmanuel Sinclair. Wawili hao walianza kusoma kutika shule hiyo, walikuwa watoto wa Kizungu waliokuwa wazuri mno.
Walikuwa watoto wakimya sana, hawakuwa wazungumzaji lakini tangu Walter na Walker wahamie shuleni hapo, watoto hao wakaanza kuonyesha uchangamfu wa ajabu kiasi kwamba hata walimu walikuwa wakiwashangaa.
Walikuwa wakicheza pamoja, kula pamoja na kufanya vitu vingine pamoja. Katika kipindi ambacho watoto hao walipokuwa wakifuatwa na wazazi wao kurudi nyumbani ilikuwa ni kilio, hawakutaka kuachana, hawakutaka kuona wakitenganishwa, kila siku walitamani kuwa pamoja.
Kutokana na ukaribu wa watoto wao, Cassian na mkewe wakajikuta wakiwa karibu na wazazi wa watoto hao wa kike, kwa kuwa walitambua kwamba walizoeana, wakaanza kuwapeleka nyumbani kwao na kuanza kucheza pamoja na wakati mwingine kutoka nao pamoja kitu kilichowafanya watoto hao kuwa na furaha tele.
Ilikuwa ni kama wamegawana, Jackline akawa karibu sana na Walter huku Rosemary akiwa karibu sana na Walker, kwa kifupi walikuwa na urafiki wa ajabu, urafiki uliomshangaza kila mtu aliyekuwa akiwaangalia. Walikuwa watoto hivyo kila mmoja kuhisi kwamba ni utoto tu lakini cha ajabu kila walivyozidi kukua, ukaribu ukaongezeka zaidi.

Je, nini kitaendelea?
 
Back
Top Bottom