Uzinduzi wa Bwawa la Maji la Muko (Bilioni 1.9) Kijiji cha Mengo Kata ya Ndalambo Jimbo la Momba

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,902
944
Waziri wa Maji Jumaa Aweso tarehe 01 Agosti, 2023 amezindua mradi wa Maji wa Bwawa la Muko wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.9 lililopo katika Kijiji cha Mengo Kata ya Ndalambo ndani ya Jimbo la Momba.

Bwawa la Maji la Muko lina uwezo wa kuchukua Maji Lita Milioni 166,386,474 na kuhudumia idadi ya watu 11,671 kwenye Vijiji 4 (Mengo, Ndalambo, Ikana na Kawale) na Mifugo 3420 ambapo Bwawa litadumu kwa miaka 50 kwa Matumizi ya binadamu, Mifugo na kilimo cha Mbogamboga kwa ukanda wa chini.

Mbunge wa Jimbo la Momba, Mhe. Condester Mundy Michael Sichalwe akizungumza katika Uzinduzi wa Bwawa la Muko amemuomba Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso kuendelea kusaidia upatikanaji wa Maji kwa wingi katika Vijiji kwani bado uhitaji wa Maji ni mkubwa sana kwaajili ya Wananchi, Mifugo na Kilimo cha Umwagiliaji.

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema Momba inahitaji kusaidiwa kupata Maji na Wizara ya Maji ipo tayari kusaidia Momba kupata Maji na Wizara ya Maji wapo tayari kupanga fedha za kutosha kwaajili ya kuleta matumaini makubwa ya Jimbo la Momba kupata Maji ya kutosha.

Waziri wa Maji, Aweso amesema ameambatana na Wataalam wa Maji ili wakae chini Wizara, Wilaya ya Momba na Mbunge na kuainisha maeneo yanye uhitaji ndani ya Jimbo la Momba ili maji yapatikane na yatumike kwaajili ya Matumizi ya Binadamu, Mifugo na Umwagiliaji

Aidha, Waziri wa Maji, Aweso amempongeza Mbunge Condester Sichalwe kwa kuwasemea wananchi na kufanya kazi kwa bidii na kumuahidi kuwa atampa ushirikiano wa kutosha kuleta Maji katika Jimbo la Momba

Vilevile, Aweso amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi katika sekta ya Maji na kusema hatamuangusha Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha adhma ya Rais ya kumtua Mama Ndoo kichwani inatimia.

Aweso, amesema Jimbo la Momba limepata bahati nzuri ya kupata Mbunge mzuri anayefanya kazi kwa bidii na kuwasisitiza kumpa ushirikiano wa kutosha ili kila mmoja awe sehemu ya kuleta maendeleo katika Jimbo la Momba.

Wakiwa kwenye Mkutano wa ndani Kata ya Myunga (Chuo cha DIT), Mhe. Condester Sichalwe amemuomba Waziri wa Maji Aweso, kumpa miradi mingi ya Maji ili kuepuka adha ya uhaba wa Maji kwa wananchi kwani Kati ya Vijiji 72 ni Vijiji 23 tu vina maji ya bomba na ni miradi 20 tu ya Maji inayotekelezwa inayohudumia Vijiji 22.

Mbunge Condester Sichalwe amesema kuwa Kata ya Myunga ina Vijiji 7 ambapo Vijiji 6 havina Maji; Kata ya Chitete ina Vijiji 7 ambapo Vijiji 4 havina Maji; Kata ya Kamsamba ina Vijiji 6 ambapo Vijiji 4 havina Maji; Kata ya Ikana ina Vijiji 4 ambapo Vijiji 3 havina Maji; Kata ya Ndalambo ina Vijiji 4 ambapo Vijiji 2 havina Maji; Kata ya Ivuna ina Vijiji 5 ambapo Vijiji 4 havina Maji; Kata ya Mkomba ina Vijiji 5 ambapo Vijiji 4 havina Maji; Kata ya Nzoka ina Vijiji 6 ambapo Vijiji 5 havina Maji.

Waziri wa Maji, Aweso amesema Momba bado kazi haijafanyika vizuri na kusema kuwa nje ya bajeti ndani ya mwezi Agosti 2023 atatoa Shilingi Milioni 500 kwaajili ya kununua magari Matatu (03) ya RUWASA na gari Moja lipelekwe Jimbo la Momba kwaajili ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya Maji

Waziri Jumaa Aweso amesema bajeti ya fedha mwaka 2024-2025 wataongeza bajeti ya Maji kwa Jimbo la Momba na kusisitiza usimamizi mzuri wa fedha za miradi zilizopo na zitakazoletwa na kusisitiza kuwa bado nguvu kubwa inatakiwa ili kutatua changamoto ya Maji ndani ya Jimbo la Momba.

Waziri Jumaa Aweso ameambatana na Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe na viongozi mbalimbali kuzindua mradi wa Maji wenye Tanki la Lita za Ujazo Laki Moja (100,000) lililopo katika Kijiji cha Itelefya Kata ya Mkulwe.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Mbunge wa Jimbo la Momba, Mhe. Condester Sichalwe wamehitimisha ziara katika Kata ya Kamsamba kwa kufanya mkutano wa hadhara ambapo Aweso ameahidi kutoa Shilingi Milioni 500 kwaajili ya ujenzi wa visima vya Maji na kuahidi kuongeza bajeti kwa mwaka wa fedha ujao.




WhatsApp Image 2023-08-01 at 22.12.53(1).jpeg
WhatsApp Image 2023-08-01 at 15.51.44.jpeg
WhatsApp Image 2023-08-01 at 15.51.43(1).jpeg
WhatsApp Image 2023-08-01 at 22.12.52(1).jpeg
 
Back
Top Bottom