Siku moja baada ya Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda kudaiwa kuongoza genge la wahuni kuvuruga mdahalo wa katiba mpya ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, chama chake na Jeshi la Polisi wamekwepa kuzungumzia tukio hilo, huku Rais Jakaya Kikwete akipiga kijembe kiana.
Inadaiwa Makonda na vijana wenzake takribani 15, walizusha vurugu hizo juzi wakati mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, akihitimisha hotuba yake na hivyo mdahalo huo kusitishwa, ingawa hadi sasa jeshi la polisi halijachukua hatua yoyote kwa watuhumiwa.
Jana, Makonda aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo na kukana kumpiga Jaji Warioba huku akijitetea kwamba alikuwa akijaribu kumkinga asidhuriwe na wafanya fujo hao.
Wakati Makonda akijaribu kutoa utetezi usiokuwa na mashiko, Chama Cha Mapinuzi (CCM) Taifa, kimeshikwa na kigugumizi kulizungumzia tukio hilo, ambapo Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alidai yupo nje ya nchi na hivyo hana taarifa za kuwepo kwa vurugu hizo.
Makonda alivyojitetea
Akizungumza na waandishi wa habari, Makonda alijichanganya juu ya utetezi wake akisema kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu waliompa ulinzi Jaji Warioba ili asidhuriwe na vijana waliotambuliwa kuwa wanatoka katika jumuiya ya chama hicho.
Makonda alijichanganya wakati akijibu swali la kwanini atajwe katika vurugu hizo, ambapo alisema kuwa wakati vurugu zilipoanza alimkimbilia Amon Mpanju ambaye ni mlemavu wa macho na kwenda kumhifadhi kabla ya kumfuata mwandishi wa habari wa BBC, Arnold Kayanda aliyekuwa amejeruhiwa kwa kiti kichwani.
Alisema alitoa msaada huo baada ya kuombwa na Jaji Warioba na Joseph Butiku, ahakikishe vurugu hazitokei na Mpanju hadhuriwi katika mazingira aliyokuwa.
Niliongea na Jaji Warioba kisha Butiku wakanieleza nihakikishe vurugu hazitokei na hali ilipokuwa ngumu nikamueleza Mzee Warioba aondoke kwa kuwa hali imekuwa mbaya na nikamshika mkono kumuondoa na huu ulikuwa msaada wangu kwa watu watatu tofauti katika muda ule wa vurugu,alisema Makonda ingawa maelezo yake yanatofautiana na picha zilizopigwa akidai zimefanyiwa ufundi.
Chanzo: Tanzania Daima.