Utata Mradi wa Mwendokasi (Dart- Phase 4) unaohusisha kuchukuliwa eneo la Kunduchi- Mecco Mtongani

KUNDUCHI MECCO

New Member
May 3, 2023
1
0
Wananchi wa Kunduchi Mbuyuni wanatakiwa kuondoka kupisha mradi wa Serikali wa mwendokasi (DART -PHASE 4).

Mradi huu umezua sitofahamu kati ya wananchi na waliteuliwa ku simamia mradi husika. Mradi ulitakiwa kuanza 2020 na eneo husika lilishatengwa (kiambatanisho namba 1). Tatizo linakuja ni kubadilisha eneo husika lililoadhinishwa mwanzo.

Eneo lililosadifiwa mwanzo lilikuwa ni kuanzia kituo cha mafuta cha GBP, kwa Rupia na eneo upande wa Salasala (tazama kiambatanisho cha ramani ya mwanzo). Wananchi hatujapewa sababu kwanini wameachana na upande wa Salasala ambapo kwa sasa pana ujenzi unao uendelea na kuamua kuvamia maeneo ya wananchi ambayo mwanzoni hayakuwepo kwenye dokezo la mwanzo.

Kitendo cha kuachana na eneo la upande wa Salasala na kujengwa jengo jipya (mall) kunaleta sitofahamu nyingi, yaani kuogopa kumwondoa anayemiliki hilo eneo na kuvamia maeneo ya wananchi wa hali ya chini ni uvunjaji wa haki za binadamu. Ina maana sisi ndio hatuna haki ya kuishi ila huyu aliyeanza ujenzi siku za karibuni aendelee ila sisi ambao tuko miaka na miaka tuondoke, hali hii inatusononesha sana wananchi wako.

Pili, huu mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia, na tunafahamu Benki ya Dunia ina sera za kulinda haki za binadamu na inatambua kwamba mradi wowote unapaswa kuheshimu haki za watu wote walioathiriwa na mradi huo.

“Kama kuna malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi ambao wanaathiriwa na mradi wa Benki ya Dunia, ni muhimu kwamba jambo hilo litatuliwe kwa njia nzuri na haki kwa kushirikiana na pande zote zinazohusika” nanukuu.

Tunahofia kama haki zetu hazitazingatiwa, inaweza kusababisha kutokuaminika kwa serikali na wafadhili wa mradi huo, na hii inaweza kuathiri vibaya maendeleo ya mradi na uhusiano kati ya serikali na wafadhili wa maendeleo. Kwa hivyo, ni muhimu kwa pande zote kuhakikisha kwamba haki za wananchi zinaheshimiwa na kulindwa wakati wa kutekeleza mradi huu.

Tunafahamu maendeleo ya nchi, ni pamoja na kupisha miradi kama hii, hatupingani na serikali, na itambulike kuwa wananchi hawana uwezo wa kugomea serikali, wananchi wanachopigania ni haki yao ya msingi ya kulipwa fidia stahiki , hivyo basi tunaomba tusikilizwe.

Kunduchi kuna eneo kubwa la wazi ambalo kwa uwelewa wetu mdogo tunaona linatosha kabisa kwa maegesho ya magari wanayokusudia. Sasa kwanini serikali isijitike kulitumia hilo eneo kuliko kuwasumbia familia Zaidi ya 130 ambazo wanashindwa kuwalipa fidia stahiki?. Maana tumeambiwa serikali ndio itatulipa fidia.

Kuna vitu vingi haviko sawa kuhusu huu mradi, kwanini Mradi umekiuka makubaliano ya mwanzo wa eneo husika na kutufuata sisi wananchi wa hali ya chini? Pili kuamua kutuhamisha kwa fidia isiyostahili yenye tofauti kubwa ya viwango tsh 50,000 kwa 125,000, kwa m2.

Yaani inawezekana vipi watu wa eneo moja wengine walipe 50,000 na wengine 125,000, kwa m2 moja. Hiyo land value zoning model uliotumika kufanya ulinganifu wa ulipaji wa fidia mbona umepwaya sana. Kwanini kuwe na tofauti kubwa sana kwenye eneo moja (zone moja) hii ni kuhujumu nchi.

Mthaminishaji mkuu wa serikali tunaomba utoke uje huku usiwaamini NIMETA consultant wanakudanganya. Pili, mradi utachukuwa takribrani eneo la ukubwa wa mita za mraba 156,000. Tunaomba serikali ufuatilie hata ukubwa wa hili eneo ni kubwa sana, Je eneo ni kwa ajili ya DART tu, au kuna uwekezaji mwingine ndani yake? Hii taharuki ya ukubwa wa eneo ndio unaleta sitofahamu na kuzua mambo mengi.

Endapo itaonekana serikali ina nia haswa ya kuchukua eneo husika, tunaomba kiwango cha fidia ya ardhi kiwe kimoja yaani shs 125,000 m² kwa kila kiwanja kinachoguswa na mradi ili kuwatendea haki sawa waathirika wote wa zoezi la kupisha mradi. Ambalo ndio lalamiko kubwa limekuwepo tangu kikao cha kwanza cha Serikali na wakazi wa MECCO.

Kiwango kidogo cha fidia ya ardhi iliyotangazwa hapo awali cha sh 40,000 kwa m² na hatimaye kupandishwa na kuwa shs 50,000. (hii ya wengine kulipwa 125,000 tsh, m2 ilikuwa imeficha toka mwanzoni, tumekuja kufahamu hivi majuzi tu kuwa kumbe kuna wananchi wenzetu wanalipwa/ watalipwa Kiwango cha shs 125,000 kwa m² na wengine (majority) cha 50,000 kwa m².

Hatujui ni kwanini kumetokeo tofauti ya ulipaji wa fidia kwa wakazi wa eneo hili hili moja la mradi na mwazoni wote tuliambia tutalipwa 40,000 tsh kwa m2 kwa wananchi wote. Sasa huu utofauti wa gafla umetokea wapi? Tofauti ya viwango vya fidia kimechochea hisia za kukosekana kwa haki sawia miongoni mwa wakazi wa eneo moja. Tofauti ni kubwa mno (75,000 tsh kwa m2).

Hii tofauti imezua malalamiko kwamba baadhi ya wakazi hasa wenye viwanja vidogo vidogo wananyimwa haki ya kulipwa fidia stahiki ya ardhi yao licha ya ukweli kwamba athari za kupisha mradi zinawagusa wakazi wote sawa sawa bila kubagua.

Tofauti kubwa kati ya viwango vya fidia vinavyolipwa kwa wakazi wa eneo hilo moja la mradi inaweza kuonekana kama ubaguzi na ukosefu wa haki sawa miongoni mwa wakazi.

Inapendekezwa kwamba viwango vya fidia vizingatie misingi ya usawa na haki ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayenyimwa fidia ya haki kutokana na ubaguzi wa kiuchumi, kijamii au kisiasa (divide and rules), wenye nacho wanaongezewa zaidi na wa hali ya chini wanapotezwa kabisa.

Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fidia ya haki kwa ajili ya ardhi yao na wanaondolewa kwa amani kutoka kwenye eneo la mradi. Ikiwa kuna tofauti katika viwango vya fidia vinavyolipwa, ni muhimu kwamba sababu zake zichunguzwe kwa uangalifu na hatua za kurekebisha zichukuliwe kuhakikisha kwamba wananchi wote wanalipwa fidia inayostahili.

Angalizo
Tunaomba serikali iingilie kati huu mradi kabla ujenzi haujaanza. Nahisi hapa ndio CAG, takukuru, Usalama wa Taifa, Vyombo vya Habari, na Taasisi za Haki ya Binadamu na kadhalika waingilie kati kuhusi huu mradi wawe wanafanya kazi sasa wasisubiri mradi uishe ndio waanze kuelezea ubadilifu uliojitokeza. tunaomba serikali ifanye uchunguzi wa kina kwa kutumia taasisi tajwa hapo juu kabla serikali haijapata hasara ya fedha na pia kukiuka haki za wananchi wanyonge.

Ni muhimu kwamba jamii ishirikishwe katika mchakato wa kupisha mradi na kulipwa fidia ya ardhi yao (maana mradi ndio umefuata wananchi hivyo wanahaki ya kusikilizwa, kulipwa fidia sawa kwa waathirika wote). Wakazi wote wanaohusika wanapaswa kupewa taarifa sahihi na wakati unaofaa juu ya viwango vya fidia vinavyotarajiwa kulipwa. Pia wanapaswa kushirikishwa katika majadiliano ya kuhusu masuala yanayohusiana na mradi na kuhakikisha kwamba maoni yao yanazingatiwa katika mchakato huo.

Pia kuna uvumi unasambaza kwamba mradi upo maeneo ya Mecco machimboni, kiuhalisia mradi haujaenda huko. Asilimia 95 ya eneo la mradi ni huku njia panda ya Kunduchi Mbuyuni kuelekea Mtongani, na kwa Rupia sasa hayo machimbo wanakosema sio kweli, inawezekena ndio mkakati wanaotumia hawa wathaminishaji ardhi (NIMETA Consultant) kuwadanganya viongozi wa serikali.

Tumegundua viongozi wengi wanadhani mradi upo kule Mecco machimboni wanapokuja ndio wanakutana na tofauti. Pia tunaomba Ikiwezekana zoezi la kuthaminisha maeneo wasitishe kwanza. Maana wananchi hawako tayari kwa kiwango hicho cha fidia.

Zoezi la kuthaminisha lilikuwa batili bila kufuata taratibu rasmi za uthaminishaji wa eneo, na tunaomba uwazi wa suala hili na kuwe na utaratibu mzuri wa kufanya hili zoezi ili haki itendeke kwa kila mwananchi. Tuna imani yetu muafaka ukipatikana kwenye suala hili la kiwango cha fidia ya ardhi, upinzani unaotokana na uelewa mdogo uliopo sasa miongoni mwa baadhi ya wakazi utakosa nguvu na kuisha.

Kwa mantiki hiyo tunaiomba serikali tukufu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu kutupa ufafanuzi kamili na kuingilia kati kuhusiana na mchakato huu.

Wako watiifu,
Wananchi wa Kunduchi Mecco mtongani.

Kiambatanisho no.1

1683187621126.png
 

Attachments

  • KUNDUCHI final.pdf
    217 KB · Views: 21
Back
Top Bottom