Utajiri wenye uchungu

NYEMO CHILONGANI.
UTAJIRI WENYE UCHUNGU.

Sehemu ya Kumi na Tatu.

Maisha hayakuwa mazuri hata mara moja, kila siku bi Leticia alikuwa mtu fukara ambaye hakuwa na kiasi chochote cha fedha, hakuwa akifanya biashara yoyote, hakuwa na kazi ila kitu pekee alichokuwa akikifanya katika maisha yake ni kuamka asubuhi, siku ya Jumapili, anawahi kanisani na kusafisha kanisa.
Hiyo ndiyo ilikuwa kazi pekee aliyokuwa akiifanya. Mume wake alipofariki, kila kitu kikaenda vibaya, hakuwa na fedha za kutosha, fedha ambazo alikuwa akizitegemea ni zile walizokuwa wakilipwa wajane ambazo zilikuwa katika mpango wa serikali ya Marekani.
Hata alipompata Dylan, hakukuwa na kitu kilichobadilika, maisha ya ufukara yaliendelea na fedha alizokuwa akipewa na serikali ndizo zilizokuwa zikitumika katika mambo mengine.
Mtoto Dylan akakua na kukua, akaanza masomo yake katika shule ya kimasikini hapo Kenner ambapo huko walimu wakagundua kitu kwamba mbali na umasikini uliokuwa ukimtafuna yeye na bi Leticia ambaye kila siku alijua huyo ndiye mama yake, lakini kichwa chake kilikuwa tofauti na watoto wengine.
Alikuwa na akili mno, alikuwa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma na kuandika, hakuwa muongeaji sana wala msomaji sana lakini kila alipoingia darasani, walimu waliushangaa uwezo wake.
Mpaka anafikisha umri wa miaka kumi na nne, muda wa wavulana wengi kubalehe, kwa Dylan hakuwahi kuona mabadiliko yoyote yale, alikumbuka vilivyo kwamba mwalimu wake alimwambia mara atakapofikia umri huo ndipo hapo angeweza kuona akiingia katika balehe lakini mpaka kipindi hicho, kukawa kimya.
Alishangaa, alishtuka, alihuzunika mno lakini hayo yote hayakuweza kubadilisha kitu chochote kile. Hakutaka kukaa kimya, alichokifanya ni kumwambia bi Leticia kile kilichokuwa kikiendelea ambapo mwanamke huyo alishangaa sana, akamchukua na kumpeleka hospitali.
“First of all, he has impotence problem,” (Kwanza kabla ya yote, ana tatizo la kutokusimamisha uume) alisema daktari maneno yaliyomshtua bi Leticia.
“What did you just say?” (Umesemaje?)
“He has impotence problem,” (Ana tatizo la kutokusimamisha uume wake) alijibu tena daktari.
Bi Leticia akaonekana kushtuka, hakuamini kile alichokisikia, alichokifanya ni kuchukua karatasi iliyoandikwa ripoti ile ili ajionee kama kile alichoambiwa ndicho kilichoandikwa au la.
Majibu aliyopewa na kile kilichoandikwa kwenye ripoti hakikuwa na tofauti yoyote yale, ukweli ukawa kwamba Dylan alikuwa na tatizo la kutokusimamisha uume wake. Bi Leticia alihisi kuchanganyikiwa, moyo wake ukamuuma mno, duniani, yeye akajiona kuwa miongoni mwa watu wenye mikosi, alikuwa masikini, mjane na mwisho wa siku Mungu kumpa mtoto katika njia ya ajabu sana, ila pamoja na baraka hiyo, mtoto huyo alikuwa kwenye matatizo kiafya.
Daktari hakuishia hapo, alichokifanya ni kumuita bi Leticia ndani ya ofisi yake kisha kuanza kumpa elimu kamili kuhusu ugonjwa huo. Bi Leticia alibaki akimsikiliza lakini akili yake haikuwa hapo kabisa, alikuwa akimfikiria Dylan tu, jinsi atakavyoishi huko baadaye.
“Hili ni tatizo ambalo huwatokea watu wengi. Tatizo hili hutokea mara baada ya mtu kuumwa magonjwa hatari kama kisukari, kupooza ila na wengine huzaliwa nalo kama ilivyokuwa kwa Daylan...” alisema daktari yule na kumeza mate kisha akaendelea:
“Kuwa na tatizo hili haimaanishi kwamba utakufa, hauwezi kufa bali utaishi. Hii inamaanisha kwamba huyu Dylan hatokufa bali ataendelea kuishi,” alisema daktari maneno ambayo aliamini yangemtia moyo mwanamke huyo.
Bi Leticia alichanganyikiwa, hakutaka tena kubaki mahali hapo bali alichokifanya ni kumchukua Dylan na kuondoka naye. Majibu yale alipewa yeye kama yeye, kijana huyo hakujua ni kitu gani kilitokea lakini kitendo cha kumuona mama yake akiwa kwenye hali hiyo, akashangaa mno.
Alijaribu kumuuliza, alitaka kujua ni kitu gani kilindelea lakini bi Leticia hakutaka kujibu, alibaki kimya. Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza, kila alipomwangalia Dylan moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakutaka kuona jambo hilo likiendelea mwilini mwa Dylan lakini hakuwa na jinsi, wakati mwingine aliona kuwa na umuhimu wa kukubaliana na kila kitu.
Hata kabla Dylan hakufikisha miaka kumi na nane, akagundua kwamba alikuwa na tatizo hilo, hakuwa kama marafiki zake, jambo hilo lilimuuma mno, lilimliza kila siku, moyo wake uliumia kupita kawaida ila pamoja na kutokwa na machozi, moyo kuumia lakini hakukuwa na kilichobadilika.
Baada ya kugundua kwamba alikuwa na tatizo hilo, Dylan hakujishughulisha na wanawake, muda mwingi alikuwa akikaa na marafiki zake, wakizungumza, alicheka kwa furaha lakini kila alipokuwa peke yake, moyo wake ulikuwa kwenye uchungu mkubwa.
Hali hiyo iliendelea mpaka alipokutana na msichana Catherine. Ni kweli alimpenda msichana huyo ila kitu kilichosababisha kuwa naye ni hilo tatizo alilokuwa nalo. Lilimnyima raha, alikosa amani na hakukuwa na kitu alichokitamani kwa kipindi hicho kama kuwa na msichana huyo.
“Kwa hiyo hilo ndilo tatizo linalokukabili?” aliuliza Bwana James.
“Ndiyo! Najiona kuwa si kitu, ni mwanaume jina ila sijakamilika,” alisema Dylan huku akionekana kuwa na majonzi.
“Hapana! Nahisi hili tatizo linaweza kutibika, ni lazima nifanye kila liwezekanalo mpaka kuhakikisha unapona,” alisema Bwana James.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Unaamini nitapona?”
“Asilimia mia moja, nina madaktari waliobobea nchini China ambao wanafanya tiba kwa dawa za mitishamba, huko utafanikiwa tu, ni lazima twende,” alisema Bwana James.
Alivyoambiwa hivyo, kidogo Dylan akaonekana kuwa na tumaini, mzee huyo akaonekana kuwa msaada wake mkubwa. Hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alikuwa na uhitaji mkubwa, akaomba ruhusa katika klabu yake na kisha kuanza safari ya kuelekea huko huku akiongozana na Bwana James, tena kwenye ndege yake binafsi ya kitajiri.
“Ila naomba nikuulize swali...”
“Uliza tu!”
“Una uhakika utamuoa binti yangu ukitibiwa kwa gharama zangu?” aliuliza mzee huyo.
“Ndiyo! Nitamuoa, nakuhakikisha hilo,” alisema Dylan.
“Ni lazima tuweke mkataba, haiwezekani nikafanikisha utibiwe halafu mwisho wa siku unigeuke, ninampenda sana binti yangu na ndiyo maana najitolea kukusaidia kwa ajili yake,” alisema mzee huyo.
Alikuwa mfanyabiashara anayejua sana kuhusu mikataba, hakutaka kukubaliana na mtu mdomo kwa mdomo bali ilikuwa ni lazima makubaliano yaandikwe kwamba mara baada ya kumtibia basi amuoe binti yake, kweli mkataba ukaandikwa.
Walichukua zaidi ya saa ishirini na moja ndipo wakaingia jijini Beijing ambapo wakashuka na kuanza kuelekea hotelini. Alichokifanya Bwana James ni kuwasiliana na daktari wake wa tiba za asili ambapo akamwambia kwamba alikuwa nchini humo na mgonjwa wake hivyo alihitaji matibabu hayo.
“Hakuna tatizo...mlete...”
Dylan alikuwa mwenye furaha tele, moyoni mwake hakuamini kama kweli huo ndiyo ulikuwa mwisho wa matatizo yake. Aliamini dawa za mitishamba za Kichina, alijua namna zilivyokuwa zikifanya kazi kwa uwezo mkubwa sana, hivyo tumaini lake lote lilikuwa katika dawa hizo.
Baada ya kukaa hotelini kwa usiku mmoja, kesho yake wakaondoka na kuelekea katika kijiji cha Nanjing ambacho kilikuwa Kaskazini mwa nchi hiyo. Kutoka hapo Beijing, walichukua saa nne njiani na ndipo wakafika katika kijiji hicho ambapo wakapokelewa na kwenda kwa mzee maarufu wa kutibu watu kwa kutumia mitishamba.
“Karibuni sana...” alisema mzee huyo ambapo kila neno alilolizungumza, kulikuwa na mkalimani kutoka lugha ya Kichina kwenda Kingereza.
Mpaka kufikia hapo, Dylan alikuwa na uhakika wa kupona tatizo lake na hatimaye kumuoa msichana Catherine.

Je, nini kitaendelea?
 
Madame santee
NYEMO CHILONGANI.
UTAJIRI WENYE UCHUNGU.

Sehemu ya Kumi na Nne.

Nyumbani hawakutulia, kila wakati Catherine alikuwa akipiga simu kwa baba yake kujua walifikia wapi, kama Dylan alikubali au alikataa. Moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, hakutulia, alijifikiria kuhusu mvulana huyo, alimpenda mpaka hatua ya mwisho kabisa ambapo akipenda zaidi ya hapo angechanganyikiwa na kuwa kichaa.
Saa zikaendelea kukatika, kila alipomuuliza baba yake waliishia wapi, alimwambia asubiri kwani bado kulikuwa na vitu vichache vya kufanya. Catherine akatulia, akajipa moyo kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima baba yake akamilishe kile kitu, hivyo akatulia.
Siku hiyo ilipokatika, Bwana James akawapigia simu na kuwaambia kwamba ni lazima waondoke waelekee nchini China kwani kulikuwa na kitu hakikukaa sawa. Hilo liliwachanganya Catherine na mama yake, hawakuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea kwani hata safari hiyo ilikuwa ya ghafla sana.
“Kuna nini?” aliuliza bi Claire.
“Kuna kitu mke wangu!”
“Ni salama lakini?”
“Ndiyo! Wala msijali...”
“Na huyo kijana amesemaje? Atamuoa?”
“Hilo ndilo tunalizungumzia, ila kama tukifanikisha kukifuata kile tunachokifuata nchini China, atamuoa tu,” alisikika Bwana James.
“Kitu gani hicho?”
“Usiwe na hofu mke wangu! Nitakujulisha tu,” alisema Bwana James na kukata simu.
Kitendo cha kuambiwa na mume wake kwamba kulikuwa na kitu ambacho hakutakiwa kukifahamu, kilimfanya kuwa na wasiwasi mkubwa, akakosa amani kwa kuona kwamba kulikuwa na kitu kibaya ambacho mumewe hakutaka akifahamu. Hilo hakujali, hakumwambia binti yake, akabaki nalo moyoni na siku kuendelea mbele.
Upande wa pili, tayari mzee huyo wa dawa za mitishamba akaanza kufanya mambo yake, alihakikisha anamchunguza kwa umakini kujua tatizo lilikuwa nini kwani hakutakiwa kufanya kazi hiyo pasipo kujua historia fupi ya mgonjwa.
“Mtoto wako alianza lini hili tatizo?” aliuliza mzee huyo kupitia mkalimani, tena mbele ya Dylan mwenyewe.
“Alizaliwa nalo.”
“Na ilikuwaje katika kipindi chake cha utotoni? Nataka nipate historia kidogo kutoka kwako mzazi,” alisema mzee yule.
“Huyu si mtoto wangu, ni rafiki yangu!”
“Siyo mtoto wako?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Mbona mmefanana hivyo?”
“Hutokea tu, ila ni rafiki yangu!”
Si mzee yule aliyeshangaa bali hata mkalimani naye akapigwa na mshangao. Kila alipowaangalia watu hao, walionekana kuwa kama mapacha, walifanana kwa asilimia kubwa sasa kitendo cha kuambiwa kwamba watu hao hawakuwa ndugu, kiliwashangaza wote.
“Basi ni lazima mama yake au baba aje hapa, ninataka kujua historia yake kwanza juu ya afya yake,” alisema mzee huyo.
“Hakuna tatizo! Atafika ndani ya siku mbili!”
Hilo wala halikuwa tatizo, walichokifanya ni kuwasiliana na bi Leticia na kumhitaji nchini China. Bwana James ndiye alisimamia kila kitu, akawasiliana na watu wake nchini Marekani na kuwaambia kile alichokitaka.
Kutafuta hati ya kusafiria wala halikuwa tatizo kwani kila mtu alimfahamu na aliheshimika sana. Baada ya siku mbili, Bi Leticia alikuwa ndani ya ndege akielekea nchini China.
Yeye mwenyewe hakuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, aliposikia kwamba anahitajika na mzee huyo bilionea, moyo wake ukawa na wasiwasi mno kwa kuhisi inawezekana kulikuwa na kitu kibaya kilichokuwa kimetokea ambacho kilimtia hatihani kijana wake.
Baada ya zaidi ya saa ishirini, alikuwa akiingia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beijing ambapo akateremka na kupokelewa na watu ambao waliandaliwa na kumchukua na kumpeleka ndani ya gari moja na safari ya kuelekea kijijini kuanza.
Walichukua saa nne ndipo wakaingia ndani ya kijiji hicho. Wakapokelewa vizuri na kupelekwa ndani ambapo Bi Leticia akakutana na kijana wake, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumkumbatia.
“Umefanya nini Dylan mtoto wangu?” aliuliza Bi Leticia huku akimwangalia Dylan usoni, machozi yalikuwa yakimbubujika.
“Sijafanya kitu mama!”
“Sasa kwa nini upo huku?”
“Huyu mzee anataka kushughulikia tatizo langu,” alijibu Dylan.
Miongoni mwa watu walioshtuka, hata Bi Leticia naye alishtuka, alipomuona Bwana James, jinsi alivyofanana na kijana wake alibaki akishangaa. Kipindi cha nyuma aliwasikia baadhi ya vijana wakisema kwamba kijana wake alifanana sana na bilionea huyo, alibisha lakini siku hiyo ndipo akakutana naye, walifanana kwa kiasi kubwa sana na ilikuwa rahisi kusema kwamba ni mapacha.
Hapohapo mzee wa tiba akawaita, wote watatu wakaingia ndani ya chumba kimoja ambapo huko akamtaka Bi Leticia kusimulia historia fupi kuhusu Dylan na jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea katika ukuaji wake.
“Wewe kama mzazi utakuwa unafahamu vingi, tatizo lake uliligundua kipindi gani?” aliuliza mzee huyo.
“Kipindi fulani, alipokuwa na miaka kumi na nne...” alijibu.
“Ulimzaa huyu mtoto akiwa mzima wa afya?”
“Hapana!”
“Unamaanisha alikuwa akiumwa? Alikuwa akiumwa nini?” aliuliza mzee huyo, Dylan na Bwana James walikuwa kimya wakimsikiliza.
“Sikumzaa mimi!” alisema bi Leticia huku akiangalia chini, alijisikia uchungu sana kuzungumza maneno hayo kwani katika maisha yake yote mpaka kipindi hicho, Dylana aliamini kwamba huyo alikuwa mama yake wa kumzaa.
“Hukumzaa wewe?”
“Ndiyo!”
“Kwa hiyo wewe si mama yake?”
“Ndiyo!”
Mapigo ya moyo wa Dylan yalikuwa juu, hakuamini kile alichokisikia kutoka kwa mwanamke huyo kwamba hakuwa mama yake. Katika kipindi chote cha maisha yake alifahamu kwamba huyo alikuwa mama yake, sasa ilikuwaje tena aseme kwamba yeye hakuwa mama yake, na kama yeye si mama yake, mama yake alikuwa nani na kwa nini alimficha kwa kipindi chote hicho.
“Naomba unisamehe Dylan, sikutaka ulijue hili,” alisema bi Leticia huku akianza kububujikwa na machozi.
“Sijaelewa mama...”
“Sikukuzaa....”
“Hukunizaa?”
“Ndiyo! Mimi si mama yako!”
“Wewe si mama yangu?” aliuliza Dylan.
Bi Leticia hakujibu swali hilo, tayari machozi yaliongezeka na kuanza kulia kilio cha kwikwi, hakukuwa na mtu aliyechanganyikiwa kama Dylan, kila alipomwangalia mwanamke huyo na maneno aliyokuwa akiyasema, hakuamini, wakati mwingine aliona kama anadanganywa.
Huo ulikuwa ni wakati wa Dylan kufahamu ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea, Bi Leticia hakutaka kuficha, akaanza kuwahadithia kuanza siku ya kwanza walipokuwa kanisani, tsunami ilipopiga, ilipoliharibu Jiji la New Orleans kwa kujaa maji mpaka baadaye kumuokota mtoto Dylan akiwa kwenye friji.
Alipofikia hapo tu, Bwana James akapigwa na butwaa, akasimama kutoka alipokuwa, akamwangalia Dylan mara mbilimbili, hakuamini kabisa kile alichokisikia. Kila mtu aliyekuwa mahali hapo alibaki akimwangalia mzee huyo ambaye alionyesha wazi kwamba alichanganyikiwa kwa furaha.
“Dylan ni mtoto wangu!” alisema Bwana James huku akionekana kutokuamini.
Kila mtu akabaki akimwangalia mzee huyo, bado hawakufahamu ni kitu gani kilimtokea mpaka kupagawa kiasi hicho. Bwana James akainama na kumshika Dylan, hapohapo akamkumbatia, akamng’ang’ania kama mtu ambaye hakutaka kutoka mikononi mwake.
Si Bi Leticia aliyeshangaa, kila mtu aliyekuwa ndani ya chumba hicho alishangaa mpaka mkalimani mwenyewe. Bwana James alikuwa akibubujikwa na machozi, hakuamini kama kuna siku angekutana na mtu huyo, mtoto wake ambaye alimuhifadhi ndani ya friji na hatimaye mpenzi wake, Catherine kufariki miaka mingi iliyopita.

Je, nini kitaendelea?
 
15 Reactions
Reply
Back
Top Bottom