Hahaha umeona eh
Ahhahhahah nyemo ameshaanza
Madame asantee
NYEMO CHILONGANI.
UTAJIRI WENYE UCHUNGU.
Sehemu ya Kumi.
Wote walibaki wakimwangalia Dylan, alifana mno na Bwana James kiasi kwamba wakaamini maneno kuwa kweli duniani kulikuwa na watu wawili-wawili. Kwa Catherine, mbali na mfanano aliokuwa nao kijana huyo, akahisi moyo wake ukianza kumpenda, kila alipomwangalia alihisi kabisa kuwa na mapenzi mazito moyoni mwake.
Hakujua kama kweli yalikuwa mapenzi ya kweli au kwa sababu mvulana huyo alikuwa na akili nyingi zaidi yake. Kila alipomwangalia, aliachia tabasamu pana.
“Ninamshukuru Mungu kwa hatua hii niliyofikia, huwa niliamini kwamba mafanikio yangu yapo kwenye mchezo wa kikapu, nikaweka tegemeo langu huko kabla ya viongozi wa timu kukataa kuniuza bila kujali ni umasikini wa aina gani unaitafuna familia yangu. Mbali na mchezo wa kikapu, kumbe kuna sehemu nyingine naweza kufanikiwa, naahidi kupambana, nitakuwa mfanyabiashara mkubwa sana hapa,” alisema Dylan, japokuwa alitoa tabasamu pana, lakini wengi waligundua kwamba tabasamu hilo halikuwa kutoka moyoni.
Akakabidhiwa zawadi yake na kuteremka. Alishindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka machoni mwake, aliumia mno, kila alipofikiria maisha aliyokuwa akipitia na mama yake, alihisi kwamba dunia haikuwa na usawa kabisa.
Sherehe iliendelea, watu walikunywa, kila mmoja mahali hapo alionekana kuwa na furaha kubwa isipokuwa watu wawili tu, Dylan na mama yake. Watu hao wawili walionekana kuwa na majonzi, leo hii walikuwa katika jumba kubwa, lililokuwa likiheshimiwa duniani lakini kila walipofikiria kwamba mara watakapotoka ndani ya jumba hilo walitakiwa kwenda kwenye nyumba yao ya kawaida, hakika mioyo yao iliumia mno.
“Habari yako...” Dylan alisikia sauti kutoka nyuma yake, alipogeuka, macho yake yakatua kwa msichana mzuri wa sura, mwenye uso wa tabasamu pana, alikuwa Catherine.
“Safi mrembo, karibu...”
“Asante! Hongera sana, sikufikiria kama kungekuwa na mtu mwenye akili kama zako,” alisema Catherine huku akiliachia tabasamu pana usoni mwake, Dylan akazidi kuchanganyikiwa.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Asante sana...”
“Inaelekea unasoma sana?”
“Hapana! Sikumbuki mara ya mwisho kujisomea ilikuwa lini, labda nilipokuwa mdogo,” alisema Dylan.
“Mmh! Basi hongera zako!”
Catherine alijitahidi kuzungumza na kijana huyo, alitaka kumzoea kwa ukaribu, alizungumza naye huku muda wote akionekana kuwa mwenye furaha tele. Walipoona wamezoeana vya kutosha, Catherine akamchukua Dylan na kwenda kumtambulisha kwa mama yake kama rafiki yake mpya ambaye mwanamke huyo aliukubali urafiki huo kwa moyo mweupe.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, mara kwa mara walikuwa wakichati kupitia simu zao, kila mmoja alimpenda mwenzake lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kumwambia mwenzake kwamba alimpenda kwa moyo wa dhati.
Catherine alimuogopa Dylan, hakuamini kama mvulana huyo angekubali kuwa wake, hakujiamini kabisa, kila alipomfikiria, alihisi kabisa moyo wake ukiwa na hofu kubwa hivyo kupotezea ila kwa upande wa Dylan, aliogopa kumwambia msichana huyo ukweli kwa sababu tu kwa muonekano wake alionekana kuwa mtoto wa tajiri ambaye hakustahili kabisa kuwa naye.
Urafiki huo ukaendelea mpaka walipoingia chuoni, kwa miaka miwili, hawakuwa wameonana tena, kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya ni kuwasiliana kwenye simu tu. Wakati Dylan akifaulu mtihani wake na kujiunga na Chuo cha Boston University School of Business kilichokuwa Massachusetts kwa ajili ya kuchukua masomo ya kitabibu huku Catherine akijiunga na Chuo Kikuu cha Harvard kilichokuwa hukohuko Massachusetts na kuchukua masomo ya sheria.
Hiyo ilionekana kuwa nafasi yao ya kuonana, wote walikuwa katika jimbo moja japokuwa vyuo vilikuwa mbalimbali mno lakini wakapanga kwamba ilikuwa ni lazima waonane kwani kwa kufanya hivyo ukaribu wao ungekuwa mkubwa na kuzoeana zaidi.
Kwa kuwa mchezo wa kikapu ulikuwa kwenye damu yake, Dylan akapata wakati mgumu sana, kila alipowaona watu wakicheza katika timu ya chuo, akapata hamu ya kutaka kucheza nao.
Hakukuwa na mtu aliyejua uwezo wake, wengi walipomuona, walimdharau na kumtania alikuwa na urefu wa bure na wakati hakuwa na uwezo wowote ule katika kucheza mpira wa kikapu.
Maneno hayo yalimkwaza sana lakini aliendelea kuvumilia mpaka pale alipoona kwamba uvumilivu umemshinda hivyo alitakiwa kuwaonyeshea watu hao yeye alikuwa nani katika mchezo huo.
Alipoomba kujiunga na timu ya chuo kwa upande wa mchezo wa kikapu, wengi walimpuuzia, walimdharau kwa kumuona hajui lakini alipopewa nafasi, kila mtu alishika mdomo kwa mshangao, katika maisha yao, hawakuwahi kumuona mchezaji aliyekuwa na uwezo mkubwa kama aliokuwa nao Dylan.
Siku hiyo alipoonyesha uwezo mkubwa uwanjani, wasichana wakashindwa kuvumilia, wengi wakaanza kujigonga huku wakitamani mvulana huyo atoke nao kimapenzi. Hilo lilikuwa suala lililomnyima furaha sana Dylan, hakutaka kuwa na msichana yeyote, katika maisha yake kipindi hicho, alihitaji kuwa peke yake kwani hakukuwa na kitu alichokipenda kama kutokuwa na msichana yeyote.
Hakuwahi kufanya mapenzi na msichana yeyote na wala hakuwahi kuwa kwenye uhusiano na msichana yeyote yule, kile alichokipenda moyoni mwake ni kuwa peke yake tu, alijitahidi kusoma, kucheza kikapu ili mwisho wa siku kufanikiwa na kuwa bilionea.
“Catherine.....” aliita Dylan kwenye simu.
“Nipo hapa...”
“Kuna kitu nataka kukwambia....”
“Kitu gani tena...”
“Ooh! Au basi...”
“Hapana! Niambie kitu gani!’
“Kuna kitu kinanisumbua tangu utotoni, sina raha nacho kabisa, kinanitesa na kuniua moyoni mwangu,” alisema Dylan kwa sauti ya chini.
“Kitu gani jamani?”
“Nikuulize swali?”
“Niulize...”
“Unanipenda?”
“Ndiyo, tena sana...”
“Ila...au subiri...naomba nikwambie siku nyingine, ila jua kwamba ni kitu kinachoniumiza sana moyoni mwangu...” alisema Dylan, hakutaka kusikia Catherine angesema nini, alichokifanya ni kukata simu, kilichofuatia ni sauti ndogo ya kilio cha kwikwi.
****
Mapenzi yalimuumiza mno, kila siku alikuwa mtu wa kumfikiria Dylan tu, alimpenda mvulana huyo na alikuwa tayari kwa kila kitu. Kitendo cha kumwambia kwamba kulikuwa na kitu alitaka kumwambia lakini akanyamaza, kilimpa mawazo mengi Catherine kiasi kwamba alibaki akiwa na mawazo tele.
Hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuanza kumpigia tena, simu iliita, iliita na kuita lakini haikupokelewa kabisa. Hakutaka kukubali, hakutaka kuona anashindwa, aliendelea kumpigia lakini ikatokea kipindi ambacho simu hiyo haikuwa ikipatikana kabisa.
Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakutaka kubaki chuoni, kitendo cha mvulana huyo kutokupokea simu kilimchanganya sana, alichokitaka kusikia ni kile ambacho Dylan alitaka kumwambia.
Chuoni hakukukalika tena, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika stesheni ya treni za umeme na kupanda moja ambayo alitaka impeleke kutoka katika Jiji la Cambridge mpaka Boston alipokuwa akisoma Dylan.
Ndani ya treni alikuwa na mawazo mengi, hakuonekana kuwa na raha kabisa, mapenzi yalikichanganya kichwa chake. Hakukuwa na kitu kingine alichokifikiria zaidi ya Dylan tu.
Baada ya dakika thelathini, treni ikaanza kuingia katika Jiji la Boston, kwa haraka sana Catherine akasimama na kwenda mlangoni, alikuwa na presha kubwa ya kutaka kuteremka, amuwahi rafiki yake wa kiume na kuzungumza naye.
Treni iliposimama, hakutaka kubaki ndani ya treni ile, akatoka na kuanza kuondoka. Alitoka ndani ya jengo la kituo hicho na kufuata teksi moja na kuingia ndani, dereva aliyekuwa nje akisubiri abiria, akaingia ndani.
“Where to?” (Unakwenda wapi?) aliuliza dereva mara baada ya salamu.
“Boston University..”
Dereva akawasha gari na kisha kuanza safari ya kuelekea huko. Njiani, hakutaka kuzungumza kitu chochote, bado aliendelea na jitihada zake za kumtafuta Dylan kwenye simu pasipo mafanikio yoyote yale.
Walichukua dakika ishirini ndipo wakafika katika geti la chuo hicho na kusimamisha teksi, harakaharaka Catherine akalipa na kuteremka. Idadi kubwa ya wanachuo ilikuwa katika eneo la chuo hicho, kila mmoja alionekana kuwa bize huku wengi wakiwa wamekaa kimakundi-makundi wakijadiliana.
Hakutaka kujali sana, alichokifanya ni kuelekea ndani kabisa ambapo huko akaanza kumuulizia Dylan. Jina la mvulana huyo lilikuwa kubwa, uwezo wake darasani ulimfanya watu wengi kumfahamu, wengi walimuita kwa jina la kompyuta kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao.
“Mmh! Sijui kama yupo...”
“Kwani leo hajaonekana?”
“Nilimuona kwenye uwanja wa kikapu, baada ya hapo, kuna watu walimfuata, sijui ameelekea wapi,” alisema mwanaume aliyeulizwa na Catherine.
“Wanaume gani?”
“Siwafahamu, walikuwa na miili mikubwa, sidhani kama kuna usalama...”
“Sawa! Nashukuru!”
Japokuwa alimkosa Dylan chuoni lakini hakutaka kuondoka Boston, lengo lake kubwa lililomtoa Cambridge na kumpeleka Boston lilikuwa ni kuonana na mvulana huyo tu. Alihisi kulikuwa na tatizo, hakuwa tayari kuondoka na kurudi chuo, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumuona.
Ilipofika saa mbili usiku, akasikia simu yake ikiita, kwanza akahisi kwamba walikuwa wazazi wake ambao walikuwa na kawaida ya kumpigia simu kila siku usiku, alipoichukua simu na kuangalia kioo, hakuamini, alikuwa Dylan.
“Halo Dylan...” aliita Catherine.
“Upo wapi? Chuo au nyumbani?” ilisikika sauti ya Dylan.
“Nipo hotelini...”
“Hotelini?”
“Ndiyo!”
“Unafanya nini?”
“Nimekuja kukuona!”
“Kwa hiyo upo Boston?”
“Ndiyo!”
“Hoteli gani?”
“San Marino...”
“Sawa! Ngoja nije nikuone...”
“Kweli?”
“Ndiyo! Nipe dakika kadhaa, nina habari njema...”
“Ipi hiyo?”
“Usijali rafiki, nakuja...”
Catherine alijikuta akishusha pumzi ndefu na kuachia tabasamu pana, hakuamini kile alichokisikia kwamba mvulana aliyekuwa akimpenda alikuwa njiani kuelekea katika hoteli ile aliyokuwepo.
Tangu mara ya mwisho kuonana naye katika ikulu ya Marekani, hakuwahi kuonana naye tena mpaka kipindi hicho. Miaka miwili ilikuwa imepita, hakuwahi kumuona zaidi ya kuwasiliana naye kwenye simu tu.
Baada ya dakika arobaini na tano, simu ya mezani ikaanza kulia, akaifuata, akaipokea, sauti aliyoisikia ni ya dada wa mapokezi ambaye alimpa taarifa kwamba kulikuwa na mgeni wake aliyetaka kumuona.
“Mwambie aje...”
Catherine akajiweka vizuri chumbani kwake, akavaa nguo ya kulalia harakaharaka kwani siku hiyo, tena katika usiku kama huo ndiyo ilikuwa yenyewe ya kumfanya Dylan awe mpenzi wake kwa namna alivyojipanga kumtega hasa kwa mikao ya ajabu-ajabu kitandani.
Baada ya dakika kadhaa, akasikia mlango ukigongwa, kwa kuwa alikuwa ameshauacha wazi, akamkaribisha mgongaji, Dylan akaufungua mlango na kuingia ndani. Hali aliyomkuta msichana huyo haikuwa ya kawaida, alivalia nguo ya kulalia iliyoonyesha maungo yake ya ndani, mpaka nguo ya ndani, nyekundu aliyoivaa, ilionekana vizuri.
“Karibu Dylan,” alisema Catherine kwa sauti nyembamba ambayo aliamini ingezisismua ngoma za masikio ya Dylan.
Dylan akameza mate, akabaki akimwangalia Catherine kwa macho yenye matamanio lakini usiku huo alitaka kupinga kufanya naye kitu chochote kile, hakuwa mpenzi wake japokuwa alijisikia hali ya tofauti sana moyoni mwake.
“Kuna nini mpe...Dylan?” aliuliza Catherine.
“Sikiliza, nimechaguliwa kujiunga na timu ya mpira wa kikapu ya Boston...” alisema Dylan huku akitoa tabasamu pana.
“Unasemaje?”
“Ninakwenda kuwa bilionea Catherine, ninakwenda kutajirika...” alisema Dylan kwa sauti kubwa, Catherine aliyekuwa kitandani akasimama na kumsogelea, kilichofuatia ni kumkumbatia kwa nguvu kana kwamba hakutaka atoke mikononi mwake.
“Dylan....” aliita Catherine.
“Nipo hapa...”
“Ninakupenda sana...” alisema Catherine.
“Unasemaje?”
“Ninakupenda...”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Masikini mimi?”
“Ndiyo! Ninakupenda sana, naomba uwe wangu...”
“Niwe wako mimi?”
“Ndiyo!”
“Hapana Catherine...”
“Kwa nini?”
“Sikiliza Catherine, nina maana yangu kukwambia hivyo...” alisema Dylan.
Dylan akajitoa katika mikono ya Catherine, japokuwa msichana huyo alitamani waendelee kukumbatiana lakini kwa Dylan hakutaka kabisa kuendelea kuwa hivyo kwani isingeleta picha nzuri na wakati hakutaka kabisa kuwa mpenzi wake.
“Naomba uniache Catherine, siwezi kuwa mpenzi wako...” alisema Dylan huku akimtoa msichana huyo mikononii mwake, maumivu aliyoyasikia Catherine moyoni mwake, hayakuweza kusimulika.
Je, nini kitaendelea?