Utajiri wenye uchungu

UTAJIRI WENYE UCHUNGU
0718069269

Sehemu ya Ishirini na Sita.

Kama fedha alikuwa nazo hivyo hakutaka kuona mpenzi wake akifa au hata akipata tatizo lolote lile, alichokifanya ni kujipanga kuhakikisha Aisha anafika salama nchini Marekani na mambo mengine kuendelea.

Alichotaka kutumia ni jeshi la Marekani ambalo lilikuwa nchini humo. Alitoa kiasi kikubwa cha fedha na kuzungumza na mkuu wa jeshi aliyekuwa katika kambi huko nchini Kuwait, alizungumza naye kwamba alihitaji msichana wake apewe ulinzi wa uhakika mpaka anafika salama nchini Marekani.

Kamanda huyo akamuahidi kwamba kila kitu kingekuwa poa, kama ni kumlinda, angemlinda mpaka anaingia nchini Marekani hivyo akampa kiasi cha dola milioni moja ambazo kwa Tanzania zilikuwa ni zaidi ya bilioni mbili.

Meli kubwa ya kijeshi ikaandaliwa, ilikuwa ni lazima msichana Aisha achukuliwe na kuingizwa humo, ila kabla ya kufika huko, ilikuwa ni lazima aingizwe katika boti moja ambayo ingepelekwa mpaka katika boti nyingine ya kifahari ambayo ndiyo ingekwenda mpaka katika manowari ya kijeshi ya jeshi la Marekani.

Alichokifanya Mike ni kuwasiliana na Bwana Malik Khalifa, bilionea mkubwa wa mafuta nchini humo na kumwambia kwamba alikuwa akihitaji boti ya kifahari hivyo kama litakuwa jambo la msingi amkodishe kitu ambacho hakikuwa na tatizo lolote lile.

“Dola laki tano, zipo?” aliuliza Bwana Khalifa.

“Zipo! Wewe tu.”

“Ila nataka niweke masharti pia,” alisema Mike.

“Yapi hayo?”
“Kusiwe na mtu mwingine zaidi ya nahodha mmoja,” alisema Mike.

“Hakuna tatizo! Ila boti yangu itakuwa kwenye usalama?” aliuliza.

“Bila shaka! Hutakiwi kuhofia chochote kile, na kama bahati mbaya kukitokea tatizo, naomba nihusike katika matengenezo na malipo mengine,” alijibu Mike kwa kujiamini.

Hakukuwa na kingine kilichofanyika zaidi ya malipo kufanyika na moja kwa moja mzee Khalifa kuagiza boti yake ya kifahari, yenye kila kitu ndani na kwenda huko tayari kwa kumchukua mtu ambaye hakuambiwa ni nani.

Wakati Mike akifanya mipango yote hiyo, tayari alikwishawasiliana na Kurt na kumwambia kuhusu mpango uliokuwepo kwani alijua fika kwamba watu hao wangetaka kwenda nchini Marekani kwa kutumia gari kupita katika nchi nyingine mpaka China ambapo wangechukua ndege kitu ambacho alikuwa na uhakika kwamba wangeweza kukamatwa njiani.

****

Kurt akakiinua kichwa chake na kuwaangalia watu wote waliokuwa ndani ya gari hilo. Yeye ndiye aliyekuwa akisubiriwa, kila mtu alitaka kujua nini kilimjia kichwani mwake ili wafanye kila liwezekanalo na kutoka mahali hapo.

“You are a pregnant woman,” (Wewe ni mwanamke mjauzito) alisema Mike huku akimwangalia Aisha.

“What do you mean?” (Unamaanisha nini?)

“You are pregnant, you are going to have a baby after few minutes,” (Una mimba, unakwenda kujingua mtoto dakika chache zijazo) alisema Mike, kila sentensi aliyoongea mahali hapo, hakukuwa na aliyeielewa.

Alichokifanya ni kuinama chini ya kiti chake, kule kulikuwa na mfuko mkubwa ambao walitumia kubebea nguo nyingine mara baada ya kutoka katika eneo la tukio kwani wasingeweza kwenda na nguo hizohizo.

Alichokifanya ni kutoa nguo hizo na kisha kisha kumpa Aisha aziweke kwenye tumbo lake na kujifanya mwanamke mjauzto aliyekuwa katika hatua za mwisho kabisa kujifungua.

“Nitaweza?” aliuliza Aisha.

“Utaweza tu, ila sasa....”

“Ila nini?”

“Nataka kupewa maelekezoyote, itakuwaje kama nikionekana?” aliuliza Aisha.

“Sikiliza, utakapokuwa kwenye maumivu, wala usiuonyeshe uso wake, jifanye kama una maumivu makali, upo kwenye uchungu huku ukilalamika, ukifanya hivyo, tutafanikiwa. Shawn, huyu atakuwa mke wako,” alisema Kurt.

“Unasemaje?”
“Usihofu, mi kwa muda tu.”

Hakukuwa na cha kusubiri, kwa sababu walikuwa kwenye foleni ya kusubiri kupekuliwa, Kurt akamwambia Aisha afanye kama alivyomwambia, akachukua nguo na kuziweka kwenye tumbo lake kisha kuchukua maji na kummwagia kichwani kidogo ili yatakapoanza kutiririka lionekane kama jasho.

“Tayari?”
“Ndiyo!”

Alichokifanya Kurt ni kutoka katika foleni ile, mbele yao kulikuwa na magari zaidi ya ishirini, polisi wote walioliona gari hilo likitoka na kwenda kule walipokuwa walibaki wakishangaa, walichokifanya ni kuandaa bunduki na mbwa wao.

Kurt hakutaka kuchelewa, alitakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kila kitu kinakuwa kama kinavyotakiwa. Alipofika kwa polisi wale, akashusha kioo na kuanza kuwaangalia.

“Naomba mtusaidie, tusaidieni huyu mwanamke atakufa,” alisema Kurt huku akionekana kuwa na haraka na wasiwasi umemjaa.

“Kuna nini?”
“Yupo kwenye hali mbaya, anakufa, anataka kujifungua, yupo kwenye hatua za mwisho kabisa,” alisema Kurt huku akilichezesha gari lile, yaani kwenda mbele kidogo na nyuma kidogo kuonyesha kwamba walikuwa na haraka na kweli mwanamke huyo alihitaji msaada.

Polisi wawili wakachungulia ndani ya gari, macho yao yakatua kwa Aisha, hawakuweza kuuona uso wake kwani kila wakati alikuwa akiuficha huku akilalamika kwa maumivu makali ya tumbo ambalo lilionekana kuwa kubwa.

Waarabu walithamini hali za wagonjwa, kitendo cha kumwona Aisha akiwa kwenye hali ile, wakachanganyikiwa, na kwa jinsi Kurt alivyojifanya kuwa na haraka ya kuruhusiwa na kuondoka, wakazidi kuchanganyikiwa zaidi na kuamini kwamba kweli mwanamke huyo alikuwa mjauzito.

“Tunaomba tupite jamani, damu zishaanza kumtoka,” alisema Kurt huku akiwaangalia polisi wale nyusoni mwao.

Ilikuwa ngumu kuamini kwamba Aisha hakuwa na mimba, maigizo waliyoyafanya mahali hapo, yalithibitisha kwamba watu hao walikuwa majasusi waliosomea.

Polisi hawakujua hilo, walichokifanya ni kuruhusu gari hilo lipite haraka iwezekanavyo ili liwahi katika Hospitali ya Khatourm ambayo haikuwa mbali na hapo walipokuwa.

Kurt akakanyaga mafuta na kuondoka mahali hapo kwa mwendo wa kasi. Hakukuwa na aliyeamini kwamba wangeweza kuvuka kirahisi namna hiyo. Baada ya kufika mbele kabisa, Aisha akarudi katika hali yake ya kawaida na kutoa nguo zile.

“Tumevuka...” alisema Kurt huku akionyesha tabasamu, tayari gari hilo likaanza kuingia katika jangwa dogo la El Shimareek lililokuwa Mashariki mwa jiji la Kuwait.

“Siamini...”

“Amini! Upo na watu wenye akili nyingi, ni lazima tutafika Marekani!” alisema Kurt.

“Marekani?”
“Ndiyo! Ooh! Samahani, hatukukwambia aliyetutuma,” alisema Kurt.

“Nani aliwatuma?”
“Mike!”
“Mike?” aliuliza Aisha huku akionekana kushtka.

“Ndiyo! Amesema ni lazima tukufikishe kwake kwa gharama zozote zile, hayupo tayari kukuona ukiuawa,” alisema Kurt huku akimwangalia Aisha machoni.

Moyo wa Aisha ukanywea, hakuamini kusikia kwamba mpenzi wake, aliyekuwa na mimba yake, Mike ndiye aliyefanya mipango yote hiyo. Kwa kuonyesha hivyo tu, akagundua jinsi mwanaume huyo alivyokuwa na mapenzi mazito kwake.

Akashindwa kuvumilia, alikuwa na furaha mno, hapohapo machozi ya furaha yakaanza kumtiririka mashavuni mwake.

“Mike ndiye aliyefanya hivi?” aliuliza Aisha.

“Ndiyo! Anakupenda sana, ni lazima tufanye kazi yake,” alisema Kurt huku safari ikiendelea.

Safari iliendelea zaidi, walipita katika jangwa hilo ambalo lilikuwa na lami mpaka walipopofika katika mji mwingine wa El Salmiya ambapo tayari muda ulikuwa umekwenda na hivyo kutakiwa kupumzika hapo.

Walichokifanya ni kuchukua vyumba katika hoteli moja huku wakiingia na Aisha ndani ya hoteli hiyo na yeye kuchukua chumba huku akiwa amevalia baibui na nikabu na kujitambulisha kama mfanyabiashara kutoka Iraq.

Hakukuwa na mtu aliyehofia chochote kile wala kumgundua msichana Aisha mpaka kipindi alipokwenda chumbani kwake. Huko, kitu cha kwanza ni kutulia kitandani na kuanza kuyafikiria maisha yake.

Mpaka kipindi hicho, bado hakuamini kama kwelia linusurika kuuawa kwa kupigwa mawe, hapo ndipo aipoamini kwamba mpenzi wake, Mike alimthamini na jicho lake lilikuwa kwake.

“Nashukuru kwa kuniokoa,” alisema Aisha wakati akizungumza kwenye simu.

“Usijali mpenzi. Bado ninakuhitaji wewe na mtoto wangu, siwezi kuruhusu jambo baya lolote kwenu,” alisikika Mike.

Usiku wa siku hiyo Aisha na wanaume wale wakalala ndani ya hoteli hiyo. Siku iliyofuata, akaamka tayari kwa kujiandaa. Hakukumbuka kuswali, alichokifanya ni kuelekea bafuni, akaoga, alipomaliza, akarudi chumbani na kuanza kujiandaa huku tayari ikiwa ni saa kumi na mbili asubuhi.

“Ngo ngo ngo ngo...” ulisikika mlango ukigongwa kwa nguvu.

Aisha akashtuka, hakujua ni nani alikuwa akigonga mlango kwa nguvu kiasi hicho. Kwanza akaogopa kwa kuhisi kwamba inawezekana ni mtu mbaya hivyo akasubiri. Baada ya kusikia mtu akiita na sauti ilikuwa ni ya Kurt, akaenda kuufungua mlango.

“Kuna nini?” aliuliza Aisha huku akimwangalia Kurt usoni.

“Kuna polisi wamekuja, wapo wengi na wamezingira hoteli,” alijibu Kurt.

“Unasemaje?” aliuliza Aisha huku akirudi chumbani, akaelekea dirishani na kuchungulia, kweli, idadi kubwa ya polisi walikuwa wamefika hotelini hapo, walikuwa na bunduki, walitaka kumchukua Aisha, walisikia taarifa kwamba msichana huyo alikuwa humo, na walikuwa mahali hapo kwa ajili yake, Aisha akabaki akiwa na hofu kubwa.

“Tutaondoka vipi?” aliuliza Aisha huku akiwa amechanganyikiwa kama kichaa, macho yake yakaanza kuwa mekundu.

Je, nini kitaendelea
 
NYEMO CHILONGANI
UTAJIRI WENYE UCHUNGU
0718069269

Sehemu ya Ishirini na Saba.

Msako wa kumtafuta Aisha bado ulikuwa ukiendelea mitaani, kile kilichotokea kiliitikisa nchi ya Kuwait, na si Kuwait peke yake bali hata nchi nyingine za Kiarabu, zote zilitikisika.

Mitaani watu waliendelea kuwa makini kwani kile kiasi cha fedha kilichokuwa kimeahidiwa kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake kiliwachanganya watu wengi.

Baada ya polisi kuendelea na msako, wakapata taarifa kwamba mara ya kwanza msichana huyo na watu waliomchukua walikuwa wakielekea Khaitan lakini baadaye wakahairisha na hivyo kuanza kurudi Kuwait kwa ajili ya kuelekea katika Jiji la El Salmiya.

“Ni lazima twende huko. Kwanza walipita vipi njiani?” aliuliza mkuu wa polisi hapo Kuwait lakini hawakupata jibu.

Kilichowachanganya ni namna ya watu hao walivyojiachia njiani kwenda Khaitan mpaka kurudi tena Kuwait na kujiandaa kwenda huko El Salmiya. Walipita vipi katika vizuizi vilivyokuwa njiani na wakati kote huko kulikuwa na polisi waliokuwa wakipekua kila gari lililopita.

“Ilikuwaje mpaka wakapita hapa?” aliuliza mkuu wa polisi wa jiji hilo la Kuwait.

“Sina uhakika kama walipita hapa, tulipekua kila gari,” alijitetea polisi mmoja.

“Una uhakika?”
“Ndiyo! Hakukuwa na gari ambalo hatukulipekua!” alijibu.

“Sasa walipitaje?”
“Sidhani!”

Polisi waliokuwa hapo walibisha, kila walipokumbuka vizuri kama kulikuwa na gari lililopita pasipo kulikagua, hakukumbuka kufanya hivyo. Waliendelea kujiuliza na mwisho wa siku kukumbuka kwamba kweli kulikuwa na gari ambalo lilipita, hawakulikagua ndani bali waliwaona wanaume wakiwa na mwanamke mjauzito.

“Mlimwangalia mwanamke huyo?”
“Wapi?”
“Usoni!”

“Hapana! Alikuwa kwenye maumivu makali!” alijibu polisi.

“Na hao wanaume walikuwaje?”
“Ni Wamarekani!”
“Mungu wangu! Ndiyo wenyewe!”
“Unasemaje?”

Hakukuwa na cha kusubiri mahali hapo, polisi walionekana kuwa wapumbavu, kisa mwanamke kuwa mjauzito, hiyo haikustahili kabisa kuliruhusu gari hilo lipite kiholela pasipo kukaguliwa.

Walichokifanya ni kuingia garini na kuondoka. Sehemu pekee ambayo walijua kwamba watu hao walikuwa wakielekea ilikuwa ni jijini El Salmiya tu. Njiani, dereva aliendesha kwa mwendo wa kasi, tayari giza liliashaanza kuingia, kitu walichokuwa wakimuomba Mungu ni kuvuka salama katika jangwa dogo la El Shimareek ambalo kwa nyakati za usiku ambapo huwa na baridi kiasi, upepo huupelekea mchanga wa jangwa hilo barabarani na kuifunika barabara hiyo.

Ndani ya dakika chache walikuwa katika jangwa hilo, walichokiona kiliwafurahisha kwani japokuwa upepo ulikuwa ukipiga lakini changa haukuweza kuifunika barabara hiyo.

Safari iliendelea, walipofika katika Jiji la El Salmiya huku tayari ikiwa ni saa mbili usiku, kazi ikawa kutafuta hoteli ambayo walikuwa na uhakika kwamba watu hao walielekea.

Hoteli ya kwanza kabisa kufika ilikuwa ni Paradise, moja ya hoteli kubwa huko El Salmiya, walipofika hapo, swali la kwanza kabisa lilikuwa ni kuuliza kama kulikuwa na Wamarekani wamefika hapo, wakaambiwa hawakufika.

Waliendelea kutembelea hoteli mbalimbali na mwisho wa siku kufika katika Hoteli ya Sultan ambapo baada ya kuulizia wakaambiwa kwamba ndiyo, kulikuwa na Wamarekani watatu walifika hapo kupanga huku wakiwa na msichana wa Kiarabu.

“Ndiyo, walifika hapa saa mbili zilizopita!” alijibu mhudumu.

“Una uhakika?”

“Ndiyo!”

Walichokifanya polisi hao ni kuwasiliana na polisi wenzao, wakawapa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea na hivyo kutakiwa kufika mahali hapo. Kwa kuwa hawakutaka kugundulika kama walikuwa hapo, wakawaambia kwamba mara watakapokuwa wakija, wasiwashe ving’ora kwani wangewashtua watu hao.

“Hakuna kuwasha ving’ora, kuweni makini sana katika hilo,” alisema polisi huyo.

“Sawa mkuu!”

Baada ya dakika tano, polisi wengine wakafika hotelini hapo, walifanya kama walivyoambiwa kwamba hawakutakiwa kuwasha ving’ora vya magari yao. Walipofika, wakachukua bunduki zao na kujiandaa kwa kile ambacho wangeambiwa wakifanye.

Hakukuwa na muda wa kutafuta vibali vya kufanya upekuzi, walitumia vyeo vyao kuanza kupekua kila chumba. Walianzia vya ghorofa ya chini kabisa, vyumba vyote, hawakukuta mtu. Hawakukubali, wakapanda juu, kote huko hawakukuta mtu.

Walichanganyikiwa, hawakuamini kama walikuwa wakienda kushindwa. Waliambiwa kwamba kulikuwa na Wamarekani watatu waliingia wakiwa na msichana, sasa iweje waanze kupekua kila chumba wasiwaone watu hao?

Hawakutaka kukata tamaa, walichokifanya zaidi ni kuingia mpaka vyooni, kote huko, kila walipopita hawakuambulia kitu, watu hao hawakuonekana hata kidogo.

Hilo liliwachanganya sana, kila walipotaka kuondoka mahali hapo, ilikuwa vigumu sana, mioyo yao ilikataa kabisa hali iliyowapa uhakika kwamba watu hao walikuwa humo. Sasa ni sehemu gani walipokuwa? Kila walipojiuliza, walikosa majibu.

“Vipi?” aliuliza mkuu wa polisi.

“Hakuna mtu.”
“Hakuna mtu?”
“Ndiyo mkuu!”
“Mmeangalia kila vyumba?”
“Ndiyo! Tena hasahasa hivi walivyochukua wao, hakuna kitu,” alijibu polisi huyo.

Kuaminika ilikuwa ngumu sana, walikuwa na uhakika kwamba watu hao walikuwa ndani ya hoteli hiyo, sasa iweje polisi hao waseme kwamba waliwatafuta kila kona ikiwemo ndani ya vyumba walivyofikia lakini waliwakosa?

Mkuu wa kituo hakutaka kukubali hata mara moja, alichokifanya, yeye kama polisi wengine naye akaingia ndani ya vyumba hivyo kupekua, chumba kwa chumba, bafu kwa bafu, hawakutakiwa kuacha sehemu yoyote ile.

“Watapatikana tu,” alisema polisi huyo huku wakiendelea kupekua kwenye kila chumba.

****

Hali ilikuwa ni ya hatari sana, nje kulikuwa na polisi na walitakiwa kuondoka mahali hapo haraka iwezekanavyo. Mtu aliyekuwa akihitajika alikuwa Aisha tu, huyo ndiye alikuwa mzigo ambao wao waliutaka lakini hata hao polisi waliutaka pia.

Walikusanyana ndani ya chumba kile na kupanga mikakati ya kuondoka hotelini hapo. Silaha walikuwa nazo, lilikuwa jambo jepesi sana kutumia silaha lakini kutokana na hali iliyokuwepo, hasa wingi wa polisi wale, hakukuwa na uwezekano wa kufanya hivyo.

“Ni lazima tushuke chini,” alisema Kurt.

“Tutashuka vipi?” aliuliza Shawn.

“Subiri!”

Alichokifanya Kurt ni kuchungulia nje kupitia dirishani, alitaka kuangalia kama kulikuwa na uwezo wa kutoka ndani ya chumba kile. Chumba cha tatu kutoka hapo walipokuwa kulikuwa na bomba moja la maji ambalo lilishuka chini, iwe isiwe, ilikuwa ni lazima watumie bomba lile kushukia chini.

“Ni lazima tushuke kupitia bomba lile,” alisema Kurt.

“Lile kule?”
“Ndiyo!”

Kwao halikuwa tatizo lakini kwa Aisha ilikuwa ni tatizo kubwa. Walichotakiwa kufanya kilikuwa ni kutoka hapo chumbani kupitia dirishani, wapite kupitia ukuta ule, nje nje, dirishani kwa dirishani mpaka watakapolifikia lile bomba na kuteremkia chini.

“Nitaweza kweli?” aliuliza Aisha.

“Usijali! Utaweza tu,” alisema Kurt.

Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, walichokifanya ni kutoka ndani ya chumba kile na kutoka nje kupitia dirisha lile. Mtu wa mbele alikuwa Kurt, aliyefuata alikuwa Aisha, aliyefuata alikuwa Shawn na wa mwisho alikuwa Sam.

Waliambaa katika ukuta ule huku wakiwa wamefunga dirisha. Aisha aliogopa, kule alipokuwa akipitishwa, tena ghorofani kulionekana kuwa na hatari kubwa lakini hakutaka kubaki.

Aliyafumba macho yake kwa kuhisi kwamba kama angeyafumbua basi angejisikia kizunguzungu na kuanguka chini. Waliendelea kuambaa mpaka walipolifikia bomba lile ambalo Kurt akalidandia, wengine wakafuata na kuanza kuteremka chini.

Japokuwa polisi walikuwa wamezunguka hoteli ile lakini hawakuzunguka katika upande ambao bomba lile lilipokuwa kwani chini ya bomba lile kulikuwa na choo, mbali na hiyo, karibu na choo kile kulikuwa na sehemu iliyokuwa na nyaya nyingi za umeme ambazo zilitumika katika hoteli ile.

Waliteremka kwa kasi kubwa huku wakimsisitizia Aisha afanye hara, kasi yao ya kushuka kupitia bomba hilo walitumia dakika tano tu, wakawa chini na hivyo kuuanza kuelekea katika choo kidogo ambacho kilionyeshwa kutokutumiwa mara kwa mara.

“Tuingieni chooni, hakuna usalama, huko, tutaruka kupitia dirishani na kwenda upande wa pili,” alisema Kurt na wote kufanya kama walivyoambiwa.

Wakaingia ndani ya choo kile, hakikuwa kisafi, kilitelekezwa. Ndani ya choo kile kulikuwa na kidirisha kidogo kilichokuwa na nondo zilizochoka, hakukuwa na muda tena, alichokifanya Kurt ni kuanza kuzipiga nondo zile, zikachomoka na hivyo kubebana na kuanza kutoka nje.

“Kuna nini huko?” aliuliza Shawn.

“Kuna nyaya za umeme tu, kule mbele naona kuna ukuta wa hoteli,” alijibu Shawn.

“Na nyaya zinapitika?”
“Ndiyo! Ila tunatakiwa kuwa makini mno,” alijibu Kurt.

“Basi twendeni hivyohivyo, haina jinsi.”

Kurt akarukia upande wa pili, Shawn na Sam wakambeba Aisha na hatimaye naye akapita katika dirisha lile na kulrukia chini. Kilichoendelea ni kuanza kuelekea kule kulipokuwa na ukuta, tena huku wakipita katikati ya nyaya za umeme.

“Inatakiwa kuruke ukutani,” alisema Kurt.

“Ila kuna nyaya za umeme.”
“Hakuna tatizo, tuzime umeme.”

Walikuwa majasusi ambao walifahamu mambo mengi, wanapokuwa kambini, hufundishwa masuala ya kompyuta, jinsi ya kucheza na programming na software kwa ujumla, mbali na mambo ya kompyuta, pia walifundishwa kuhusu umeme.

Kurt akakifuata chombo kilichokuwa kimekusanya nyaya nyingi za umeme na kuanza kuzikatakata nyaya muhimu kwa kutumia kisuu chakke kidogo kilichokuwa na plastiki hasa zile nyaya zilizokuwa zikipitisha umeme.

Mara umeme ukakatika hotelini. Hakuishia hapo kwani baada ya umeme kukatika tu, jenereta likajiwasha. Kwa haraka sana akalisogelea na kisha kulizima.

“Tuna sekunde thelathini kuruka ukuta ule,” alisema Kurt.

“Sawa. Tufanyeni haraka.”

Ndicho walichokifanya, mtu wa kwanza kupanda juu alikuwa Kurt, alipofika juu, akazing’oa zile nyaya zilizokuwa zimepitishwa na kisha kuanza kumvuta Aisha. Walifanya hivyo kwa kusaidiana mpaka wote wakawa juu ya ukuta ule, wakarukia upande wa pili ambapo kulikuwa ni ufukweni, walichokifanya ni kuanza kuambaaambaa huko.

Walikuwa wakikimbia kwa kasi kuelekea upande wa Kaskazini, kulikuwa na giza lakini hawakutaka kusimama, ilikuwa ni lazima watoroke kwani kesho yake asubuhi, boti ya kifahari ilitakiwa kufika mahali hapo, iwachukue na kuondoka zao.
Wakati wakiwa kwenye kasi, mara wakasikia mlio wa risasi moja ikipigwa hewani, hawakujua ni nani alikuwa ameipiga kwani giza lililokuwepo mahali hapo halikuwapa uwezo wa kuona kilichokuwa mbele.

“Simameni hapohapo,” ilisika sauti ya mwanaume mmoja ambaye hawakuwa wakimuona, wakasimama.

Ghafla wakatokea wanaume wawili waliokuwa na bunduki, wakaanza kuwasogelea, walipokuwa mbali kama hatua nane, wakawaambia walale chini, harakaharaka wakalala.

“Nyie ni wakika nani?” aliuliza mwanaume mmoja kwa sauti ya juu.

“Wakimbizi...tumetoka Iran,” alijibu Aisha hata kabla Kurt hajajibu.

“Kwa nini mnapitia baharini?” aliuliza mwanaume yule huku akianza kusogea kule walipokuwa wamelala.

“Tumeamua, tunaogopa kurudishwa nyumbani! Tusaidie ndugu zako,” alisema Aisha huku akijifanya kulia.

“Na hawa ni wakina nani?”
“Kaka zangu!”

Jamaa huyo hakuishia hapo, akasogea zaidi na kumgusa Kurt kwa bunduki yake. Kurt akanyamaza, hakutaka kuzungumza kitu, alikuwa akimhesabia hatua tu.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Mungu akipenda
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom